Serikali yajibu madai ya Air Tanzania kuzuiwa kuingia Ulaya
- Yasema mazungumzo bado yanaendelea kupata kibali cha kuruka katika nchi za umoja huo.
- Msigwa awatoa hofu Watanzania.
Arusha. Serikali ya Tanzania imetolea ufafanuzi taarifa ya Shirika la Ndege Tanzania ( ATCL) kuzuiwa kuingia katika anga la nchi za Umoja wa Ulaya (EU) ikisema bado wapo kwenye mazungumzo.
Taarifa hiyo, iliyosambaa katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vinaitaja Air Tanzania kuwa miongoni mwa ndege zilizozuiwa kuingia katika anga la nchi hizo kwa sababu za kiusalama zilizoainishwa na Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA).
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliyekuwa akizungumza na vyombo vya habari usiku wa Novemba 13, 2024 amesema Air Tanzania haijazuiwa kuingia katika nchi hizo kwa kuwa bado haijaanza safari za kwenda huko.
Aidha, Msigwa ameongeza kuwa kwa sasa kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya ATCL na mamlaka za anga za Umoja wa Ulaya ili kukamilisha taratibu za kupata kibali cha kutua katika nchi hizo.
“Shirika (ATCL) lipo katika mchakato kwa kushirikiana na mamlaka za Umoja wa Ulaya kupata kibali cha kuruka ua kutua katika anga la ulaya, hiyo isiwe tafsiri ya kuziwa,”amesema Msigwa.
Msigwa amebainisha kuwa tayari wataam wa anga kutoka nchi hiyo wapo nchini Tanzania kukamilisha maongezi hayo ili kupata vibali vya ndege hiyo kutua akatika anga la nchi hizo.
Aidha, Msigwa amewatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa hiyo akisisitiza kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na unafanyika kila shirika hilo linapotakan kupanua mawanda ya usafirishaji.
“Watanzania ningependa kuwatoa hofu, jitihada za shirika letu(Air Tanzania) kupanua wigo wa huduma zake kutua katika maeneo mbalimbali duniani kusafirisha abiria, mizigo na vitu vingine vingi,”ameongeza Msigwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya EU jumla ya mashirika 129 ya ndege yamepigwa marufuku kutoka anga la umoja huo yakiwemo mashirika 100 ya ndege yaliyoidhinishwa katika Majimbo 15, kwa sababu ya uangalizi duni wa usalama na mamlaka ya usafiri wa anga.
Mashirika 22 ya ndege yaliyoidhinishwa nchini Urusi, pamoja na mashirika saba ya ndege kutoka mataifa mengine ikiwemo Air Tanzania (Tanzania), Air Zimbabwe (Zimbabwe), Avior Airlines (Venezuela), Blue Wing Airlines (Suriname), Iran Aseman Mashirika ya ndege (Iran), Fly Baghdad (Iraq) na Iraqi Airways (Iraq).
SGR haitaendeshwa kwa dizeli
Katika hatua nyingine Msigwa amekanusha taarifa za Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuagiza vichwa vya treni vinavyotumia dizeli.
Msigwa amesema TRC haina mpango wa kurudi kwenye matumizi ya dizeli licha ya changamoto ndogo ndogo za kukatika kwa umeme kunakosababisha treni hiyo kukwama mara kadhaa.
“Changamoto ndogondogo zimejItokeza najua ndiyo kwanza tumeanza treni hii ya umeme, kutakuwa na changamoto mbili tatu lakini haina maana tutakuwa tumeshindwa kabisa mradi huu mkubwa na wa kimkakati,” amesema Msigwa.
Kwa muda wa miezi minne tangu kuzinduliwa kwa reli hizo Watanzania wameshuhudia kukwama kwa shughuli za usafirishaji wa reli hizo huku sababu zikitajwa kuwa ni hitilafu ya umeme na uhujumu wa miundombinu hiyo.
Kukwama huko kumesababisha baadhi ya Watanzania na wanasiasa wa upinzani kukosoa ufanisi wa reli hizo licha ya kuwa njia ya usafirishaji inayotegemewa na wengi siku za hivi karibuni.