Serikali mbioni kutoa mwongozo uendeshaji vituo vya teknolojia na ubunifu
- Mwongozo huo utaweka utaratibu wa uendeshaji na uendelezaji wa kazi za wabunifu Tanzania.
- Utasaidia kuzitambua kazi hizo ili zilete matokeo chanya kwenye jamii.
- Costech, Brela waagizwa kulinda kazi za wabunifu zisiibiwe.
Dar es Salaam. Serikali imesema imeanza mchakato wa kuandaa mwongozo maalum utakaosimamia uendeshaji wa vituo vya teknolojia na ubunifu utakaosaidia kuwatambua rasmi wabunifu na kuendeleza kazi zao ili zilete matokeo chanya kwenye jamii.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na ubunifu lakini zimeshindwa kutambulika rasmi na hivyo Serikali inajipanga kuweka utaratibu maalum ikiwemo kuandaa mwongozo utakaowatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali za jamii.
“Mwaka jana tuliandaa mashindano maalum ya ubunifu na walipatikana washindi wa kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalum wenye utaratibu wa kuendesha vituo vya teknolojia na ubunifu,” amesema Ole Nasha.
Naibu Waziri huyo alikuwa akizungumza jana katika kongamano maalum la ubunifu lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( Costech) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).
Zinazohusiana:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
- Haya yatasaidia kukuza ubunifu wa teknolojia Tanzania
Wakati Serikali ikiandaa mwongozo huo, Ole Nasha ameitaka Costech kuandaa kongamano la kila mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wabunifu ili kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali ya kukuza ubunifu Tanzania.
Pia ameiagiza Costech kukaa pamoja na Wakala ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Biashara (BRELA) ili kuhakikisha wabunifu wanawekewa utaratibu maalum kwa ajili ya kulinda kazi zao zisiibiwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari-Maelezo, wabunifu na wagunduzi nchini wanatakiwa kutambua kuwa masuala ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na watumie fursa zinazotolewa na Costech ili kuifikia jamii.
Kwa muda mrefu, wabunifu hasa wanaojihusisha na ujasiriamali wa teknolojia wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji, mrundikano wa kodi na upungufu wa vituo vya kuendeleza kazi zao.
Huenda jitihada zinazochukuliwa na Serikali zitawasaidia wabunifu hasa vijana wenye ndoto ya kutumia teknolojia rahisi kuboresha hali za jamii zao iwapo tu hazitakuwa na madhara hasi katika ukuaji wa sekta ya teknolojia na ubunifu nchini.
Latest
