Serikali: Hakuna Mtanzania aliyekwama Lebanon

October 9, 2024 12:29 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya Israel na vikosi vya Hezbollah.

Arusha. Serikali ya Tanzania imesema hakuna mtanzania aliyekwama nchini Lebanon kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo kati ya vikosi vya Hezbollah na Jeshi la Israel.

Hezbollah, ambacho tafsiri yake ni “Chama cha Allah” ni chama cha siasa kinachofuata nadharia za Kishia chenye makao yake nchini Lebanon ambacho kiliibuka baada ya Israel kuivamia Lebanon mwaka 1982, na kinafungamana na Iran.

Israel na Hezbollah wamekuwa na mapigano yanayochukua muelekeo mpya wa kuwa vita kamili tangu uvamizi wa Hamas uliofanyika Oktoba 7, 2023 huko Gaza.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa Oktoba 8, 20204 inabainisha kuwa haijapokea taarifa zozote kuhusu kukwama kwa raia wa Tanzania wanaoishi Lebanon.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inafuatilia kwa karibu hali ya usalama inayoshuhudiwa Mashariki ya Kati, hususan nchini Lebanon. Wizara haijapata taarifa zozote kuhusu raia wa Tanzania ambao wanaweza kuwa wamekwama kutokana na hali hiyo,” imesema taarifa ya wizara hiyo. 

Taarifa ya wizara hiyo inakuja wakati ambapo nchi hizo mbili zimeripotiwa kuwa katika mapigano yaliyosababisha uharibifu wa mali, miundombinu huku maelfu ya watu wakihofiwa kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa Reuters, vita hivyo vinahisiwa kusababisha zaidi ya vifo 1,000 huku mamilioni ya raia wakilazimika kukimbia makazi yao.

Kufutia hali hiyo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema itaendelea itatoa taarifa muhimu kwa raia wote wa Tanzania wanaoishi Lebanon.

Aidha, Tanzania imesema inajiunga na jamii ya kimataifa katika kuwashauri wahusika wote katika mzozo kuingia katika juhudi za kidiplomasia kwa moyo wa dhati na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha ongezeko la vurugu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks