Ripoti: Mapato ya Serikali kuzidi makisio mara kwa mara ni udhaifu
- Ripoti ya WAJIBU yaeleza kuwa makusanyo halisi ya bajeti hayatakiwi kuzidi makisio kwa asilimia 5.
Licha ya Serikali ya Tanzania kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato hadi kuzidi makisio ya bajeti katika baadhi ya maeneo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ripoti mpya ya uwajibikaji iliyotolewa na taasisi ya WAJIBU Institute of Public Accountability inaeleza kuwa kitendo cha mapato kuzidi makisio ni udhaifu wa kimipango.
Kwa kawaida, wengi huchukulia kitendo cha makusanyo kuzidi makisio ya bajeti kwa miaka zaidi ya miwili mfululizo ni kama mafanikio makubwa, jambo ambalo Wajibu wamesema si sawa kwa kuwa linaashiria udhaifu katika uandaaji wa makadirio ya bajeti.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwajibikaji na Usimamizi wa Mapato na Matumizi 2022/23 Serikali ya Tanzania ilipanga kukusanya Sh41.48 trilioni mwaka 2022/23 lakini baadaye ilifanikiwa kukusanya Sh41.88 trilioni ikiwa ni juu zaidi ya makisio ya awali.
Katika uchambuzi wa ripoti ya CAG, taasisi hiyo inayoongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Mzee Ludovic Uttoh imeeleza kuwa tofauti kati ya makisio ya bajeti na makusanyo halisi hayatakiwi kuzidi asilimia 5 kulingana na viwango vya mfumo wa Benki ya Dunia wa kupima Hali ya Uwajibikaji wa Fedha za Umma (PEFA).
Ni tatizo la muda kidogo
Hata hivyo, katika ripoti hiyo pia Wajibu wamebaini ongezeko la mapato halijatokea kwa mwaka mmoja tu isipokuwa ni swala ambalo limekuwa likijirudia mara kwa mara.

Kwa mwaka 2022/23, ripoti ya Wajibu imeeleza kuwa ongezeko la ukusanyaji wa mapato limetokana na ongezeko la mikopo ya nje yenye masharti nafuu, mikopo ya ndani na makusanyo katika Serikali za Mitaa.
“Mikopo ya nje yenye masharti nafuu ilizidi makisio yaliyowekwa kwa asilimia 55.7, mikopo ya ndani ilizidi makisio kwa asilimia 6 na makusanyo ya Serikali za Mitaa yalizidi makisio kwa asilimia 20.8. Makusanyo halisi katika maeneo haya matatu yamezidi makadirio kwa zaidi ya asilimia 5 jambo ambalo linaashiria udhaifu katika uandaaji wa makadirio ya bajeti,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.
Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mtandaoni juu ya usimamizi wa fedha za umma ambao kwa sehemu kubwa ulichagizwa na baadhi ya masuala yaliyoibuliwa kwenye ripoti hizo za Wajibu kiasi cha kuziibua mamlaka kuelezea kiundani mambo hayo.
Miongoni mwa mambo hayo ni habari iliyochapishwa Julai 21, 2024 na gazeti la Nipashe ikielezea kuwa Sh1.7 trilioni zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kutumiwa na Serikali bila kuzirejesha.
Soma zaidi: BoT yapandisha riba ya benki kuu hadi asilimia 6
Hata hivyo, BoT iliwaeleza wanahabari Julai 22 kuwa kiasi hicho cha fedha kilitolewa kwa Serikali kama mkopo wa muda mfupi kwa Serikali ambao unakatwa kidogo kidogo pale mkopwaji anapoweka fedha.
Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT Agathon Kipandula katika mkutano huo na wanahabari alifafanua kuwa kiasi cha Sh1.7 trilioni ni mkopo wa muda mfupi unaotolewa kisheria.
BoT ndiyo benki ya Serikali na taasisi zake pamoja na benki za biashara.
“Kwa ujumla sheria yetu inatutaka tukopeshe Serikali sio kama mkopo wa ‘kufinance’ (kugharamia bajeti) lakini kama mkopo wa kuoffset (kukabiliana) ile ‘fractuation’ (mabadiliko) iliyopo kwamba umekusanya Sh10,000, unataka kulipa Sh15,000 halafu Sh5,000 inakuwa mkopo,” amesema Kipandula.
Sheria ya BoT. alieleza iko wazi kupitia ripoti ya CAG na kulingana na sheria Serikali ina uwezo wa kukopa kwa muda mfupi ndani ya siku 180 inakuwa imesharudisha deni.