Zitakavyotumika zaidi ya Sh48 bilioni za tozo ya miamala ya simu

August 20, 2021 11:07 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tangu tozo hizo zianze, Serikali imekusanya Sh48.5 bilioni.
  • Fedha hizo zimepelekwa kujenga madarasa, vituo vya afya na miundombinu.
  • Serikali yawataka wananchi kuwa wavumilivu ikishughlikia malalamiko yao.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema katika katika kipindi cha wiki nne tangu tozo mpya za miamala ya simu zianze kutumika, Serikali imefanikiwa kukusanya Sh48.5 bilioni ambazo zimepelekwa kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya.

Dk Nchemba aliyekuwa akizungumza leo Agosti 20, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema fedha zilizopatikana baada ya ukusanyaji wa tozo tangu sheria ilipoanza kutumika mwezi mmoja uliopita,  zimetumika kuboresha sekta ya afya,  elimu na miundombinu.

Amesema kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh22 bilioni zimepelekwa kujenga vituo vya afya kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya afya.

“Leo tumepeleka tena zaidi ya Sh15 bilioni kwa ajili ya ujenzi huo pia, zaidi ya bilioni 7 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa,” amesema Dk Nchemba.

Aidha, amesema kwa upande wa Zanzibar, ndani ya wiki hizo nne wameweza kukusanya Sh1.6 bilioni. 

Akizungumzia kuhusu malalamiko ya watu kuhusu tozo hizo kuwa zinawaumiza, amesema wananchi wawe wavumilivu wakati Serikali inashughulikia suala hilo.

“Vikao vya kujadili kuhusu tozo hizo bado vinaendelea na siyo muda mrefu tutatoka tamko la uamuzi wa mwisho ambao hautaathiri shughuli za  maendeleo ya wananchi,” amesema waziri huyo.

Tozo hizo ziko chini ya Sheria ya Fedha mwaka 2021. Picha| K15 Photos. 

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan aliguswa na malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu na aliwaagiza mawaziri husika akiwemo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile kutafuta suluhisho.

Dk Nchemba ameendelea kusisitiza kuwa tozo hizo ziko kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge baada ya kujadiliwa kwa kina  akibainisha kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi. 

Katika tozo hizo, watumiaji wa simu wanatozwa Sh10 hadi Sh200 kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio. Pia, kutoza Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kifedha unaofanywa kwa njia ya simu.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu amesema tayari wamepokea Sh22.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 90  katika tarafa ambazo hazina vituo hivyo katika jumla ya halmashauri 82 za Tanzania Bara.

“Kupitia tozo za miamala ya simu tutaweza kujenga vituo vya afya zaidi ya 207 katika Tarafa ambazo hazijawahi kuwa na vituo hivyo,” amesema Waziri Ummy.

Pia Tamisemi imepokea Sh7 bilioni zilizotokana na tozo ambazo zitapelekwa katika ukamilishaji wa maboma ya madarasa takriban 560. 

Enable Notifications OK No thanks