Zifahamu kozi sita zitazopewa kipaumbele mkopo wa HESLB ngazi ya Diploma 2023 – 24

October 4, 2023 1:05 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kozi za afya na sayansi shirikishi.
  • Serikali yasema hatua hiyo itaongeza wataalamu nchini.
  • Wanafunzi watakiwa kuchangamkia fursa na kusoma kwa bidii.

Dar es Salaam. Serikali imezindua mwongozo wa utoaji mikopo katika ngazi ya diploma unaotarajiwa kunufaisha wanafunzi 8,000 nchini huku kipaumbele kikiwekwa katika kozi sita ikiwemo fani ya afya na sayansi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo leo Oktoba 4, 2023, amesema Sh48 bilioni zimetengwa kufanikisha utoaji wa mikopo hiyo.

“Ni vizuri kabla hujaomba kaangalie, usiseme tu ni maeneo ya afya, tumenyumbulisha na kuanisha maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi ambayo mara nyingi Serikali ikitaka kuajiri watu haiwapati,” amesema Mkenda jijini Dar es Salaam.


Bofya hapa kusoma muongozo wa utoaji mikopo kwa ngazi ya diploma mwaka 2022/2023 


Kozi nyingine zilizopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo hiyo ni ualimu wa Sayansi, Hisabati na  Mafunzo ya  Amali, Usafiri na usafirishaji, Uhandisi na nishati, Madini na sayansi ya ardhi pamoja na Kozi ya kilimo na mifugo.

Kuzinduliwa kwa mwongozo huo kutawafuta machozi mamia ya wanafunzi wa vyuo vya kati waliokuwa wanashindwa kuendelea na masomo hayo kutokana na gharama za masomo katika ngazi hiyo kuwa juu.

Uamuzi wa Serikali kutoa mikopo kwa vyuo vya kati Tanzania uliotangazwa wakati wa bajeti ya mwaka 2023/24  ni miongoni mwa taarifa zilizopokelewa kwa shangwe na mamilioni ya Watanzania.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi watakaosoma kozi hizo kutaongeza upatikanaji wa wataalamu waliobobea katika taaluma hizo zenye umuhimu nchini.

“Serikali imejenga hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kote ambavyo vinahitaji wataalamu, nasisi tumeambiwa mfano kupata wataalamu wa  clinical dentist( daktari wa meno) ni kazi kubwa sana…

…Ni wataalamu tunawahitaji lakini kila mara hata Serikali ikitaka kuwaajiri inapata shida kuwapata,” ameongeza Mkenda.

Kwa upande wake rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) Maria John, amewataka wanafunzi wa vyuo vya kati kuchangamkia fursa ya kuomba mikopo hiyo, huku wakisoma kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kunufaika na mikopo waliyoitoa.


Soma zaidi:CAG aibua madudu zaidi bodi ya mikopo elimu ya juu Tanzania


“Unakuta wengine wakishapata hiyo mikopo hawasomi, wanalala tu au hawaingii darasani, wanafunzi wenzangu msifanye hivyo kwa sababu mwisho wa siku mtafeli na mkifeli mnajua hamuwezi kupata tena mkopo,” amesema.

Dirisha la maombi ya mikopo kwa vyuo vya kati litakuwa wazi kwa siku 15 kuanzia tarehe saba mpaka tarehe 22 mwezi huu, ambapo maombi yote yanatakiwa kutumwa kwa  nakala laini (soft copy) kupitia tovuti ya bodi ya mikopo 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks