Wawekezaji kutoka China kuyaongezea thamani madini ya Tanzania

Mwandishi Wetu 0920Hrs   Julai 24, 2019 Habari
  • Wamepewa leseni tatu za kujenga mitambo ya kusafisha dhahabu na kuyeyusha madini mbalimbali.
  • Serikali kutoa leseni mbili kwa ajili ya uchimbaji mkubwa wa madini. 
  • Ujenzi wa vituo vya kuuzia madini waongeza mapato na biashara ya dhahabu. 

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema tayari wametoa leseni tatu kwa wawekezaji kwa ajili ya kuyaongezea thamani madini ya Tanzania ili kunufaika na soko la kimataifa. 

Leseni hizo ni za ujenzi wa kinu cha kuyeyusha madini na vinu viwili vya kuchenjulia dhahabu kwa kampuni za China.  

Biteko aliyekuwa akizungumza leo (Julai 24, 2019) Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya makabidhiano ya dhahabu kilo 35.34 na fedha baina ya Kenya na Tanzania zilizokamatwa nchini humo, amesema wameanza kuchukua hatua ili kuhakikisha madini yanaongezewa thamani nchini kabla hayajasirishwa nje ya nchi. 

“Ulieleza kwa uchungu wakati ule, lazima tuongeze thamani yetu ndani ya nchi, sisi tuliamua kuchukua hatua haraka sana na wakati ule tulimtuma Naibu Waziri akaenda Uchina na Katibu Mkuu walienda kutembelea makampuni ya smelter, tukapata wawekezaji 37 waliokuja nchini wanaotaka kujenga smelters na refinery. 

“Tayari tumetoa leseni mbili za refinery kwa ajili ya dhahabu lakini tumetoa leseni moja kwa ajili ya kutengeneza smelter,” amesema Biteko mbele ya Rais John Magufuli. 

Agosti 2016, Rais Magufuli alipiga marufuku kusafirishwa kwa mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi na kuagiza shughuli za kuchenjua madini zifanyike nchini. 

Wachimbaji wa madini nchini Tanzania walikuwa wakisafirisha makinikia kwenda Mashariki ya Mbali na Ulaya kwa ajili ya kuchenjuliwa, jambo ambalo liliibua utata wa siri iliyopo kwenye mchanga huo kupelekwa nje ya nchi. 


Soma zaidi:


Leseni za uchimbaji wa madini zaongezeka

Katika hatua nyingine, Biteko amesema tangu mwaka 2010 hawajawahi kutoa leseni ya uchimbaji wa madini yenye gharama kubwa ambayo uwekezaji wake ni dola za Marekani milioni 100, lakini sasa leseni hizo zitatolewa ili kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo. 

“Katika kipindi chako Mhe. Rais tunazo leseni mbili tutazitoa kwa ajili ya uchimbaji mkubwa, lakini uchimbaji mdogo tumeshatoa jumla ya leseni 2,673, leseni za uchimbaji wa kati 32 na leseni za utafiti 105,” amesema Biteko.

Biashara ya dhahabu nayo yaimarika

Kutokana na hatua ambazo Serikali imechukua katika sekta hiyo ikiwemo ujenzi wa vituo vya kuuzia madini katika maeneo mbalimbali nchini, dhahabu inayouzwa na mapato ya Serikali yameongezeka. 

“Nieleze tu Mhe. Rais toka ulivyosema masoko yaanzishwe, Tanzania leo dhahabu tunayoipata ambayo tulikuwa tunaipata kwa mwaka mzima tunaipata kwa siku moja baada ya masoko haya kuanzishwa,” amesema Biteko. 

Akitolea mfano wa soko la Chunya mkoani Mbeya, kwa mwaka mzima ilikuwa inapatikana dhahabu ya kilo 12 tu, lakini baada ya kufunguliwa kwa soko hilo Machi, 2019, kilo 270 zimefanyiwa biashara. 

“Kule Geita dhahabu nyingi inapatikana, leo ninavyozungumza zaidi ya kilo 736 zimeuzwa na zaidi Sh136.7 bilioni zimefanyiwa biashara kwenye masoko yote nchini na Serikali imepata mrabaha na clearance fee Sh7.7 bilioni,” amebainisha Biteko na kuongeza kuwa wataendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

Rais Maguli akizungumza katika hafla hiyo, amevitaka vyombo vya ulinzi kushirikiana na Wizara ya Madini katika kulinda na kuzuia uhalifu wa rasirimali za madini ili ziwafaidishe Watanzania. 

Related Post