Wanaosafiri nje ya nchi watengenezewa kifaa kutafsiri lugha

October 10, 2019 11:51 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link

Kifaa hicho kinamsaidia mtu yeyote anayetembelea nchi ya kigeni inayozungumza lugha asiyoielewa na kupata tafsiri ya kile kinachozungumzwa na wenyeji wake kwa lugha aliyoizoea. Picha|Mtandao.


  • Ni kifaa cha kutafsiri lugha cha “Translaty” chenye uwezo wa kutafsiri lugha zaidi ya 40.  
  • Kifaa hicho kinamsaidia mtu yeyote anayetembelea nchi ya kigeni inayozungumza lugha asiyoielewa na kupata tafisri ya kile kinachozungumzwa na wenyeji wake kwa lugha aliyoizoea.
  • Kinamsaidia mtu kuokoa muda na pesa ambazo mtu angetumia kujifunza lugha za kigeni kulingana na shughuli zake.

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wako katika mchakato wa kujifunza lugha mbalimbali duniani ili kufikia malengo yako ya kibiashara, kikazi au matembezi, sasa una kila sababu ya kutabasamu.

Teknolojia imekurahisishia maisha, huna haja ya kutumia muda mwingi kujifunza lugha za kigeni, kwa sababu unaweza kupata tafsiri ya lugha mbalimbali duniani kwa kutumia kifaa kidogo ambacho unakiweka kwenye mfuko wako. 

Wabunifu kutoka Japan wameduni kifaa cha kutafsiri lugha cha “Translaty” chenye uwezo wa kutafsiri lugha zaidi ya 40 ikiwemo Kichina, Kijapani, Kiarabu. 

Kifaa hicho kinamsaidia mtu yeyote anayetembelea nchi ya kigeni inayozungumza lugha asiyoielewa na kupata tafsiri ya kile kinachozungumzwa na wenyeji wake kwa lugha aliyoizoea. 

Kifaa hicho kinafanya kazi kwa mtu kuanza kuchagua lugha anayotaka kutafsiri akiwa amebonyeza kitufye chenye herufi ‘A’ katika kifaa hicho na kusikiliza maneno ya mtu anayeongea naye, kisha kitampa tafsiri anayotaka kwa lugha yake. 

Na wakati wa kumjibu mtu unayeongea naye, utabonyeza kitufye chenye herufi ‘B’ ili kifaa hicho kitafsiri maneno ya lugha ya mtu unayeongea naye.

Kifaa hicho kinatumia programu endeshi za iOs na Android kutafsiri lugha mbalimbali kwa mfumo rahisi wenye ubora mzuri wa sauti. 


Zinazohusiana: 


Mtaalamu wa masuala ya teknolojia ambaye amewahi kutumia kifaa hicho, Kizwalo Simbila anasema faida za kifaa hicho ni mkubwa kwani kinatafsiri kwa ufasaha lugha na kinampa mtu urahisi kuelewana na mwenzie kupitia teknolojia ya kisasa.

“Nilivyokitumia kwa mara ya kwanza ilinisaidia kwani mtu niliyekuwa nawasiliana naye hakuwa anaelewa lugha yangu hivyo ilimrahisishia kuelewa ninachomwambia. Ni teknolojia yenye manufaa makubwa kwa dunia nzima,” amesema Simbila.

Urahisi unaoletwa na teknolojia hii ni upungufu wa gharama na muda ambao mtu angeweza kupata kujifunza lugha nyingi kwa wakati mmoja kwa ajili ya shughuli zake anazofanya katika nchi anayokwenda. 

Kifaa hicho, ni muendelezo wa teknolojia ya kutafsiri lugha zinazotumiwa duniani ikiwemo ya Google Translate ambayo inatafsiri lugha mbalimbali kwa kutumia simu ya mkononi. 

Enable Notifications OK No thanks