Vituo vya redio vyaongezeka Tanzania vikiandamwa na changamoto ya ubora wa maudhui

Nuzulack Dausen 0210Hrs   Februari 18, 2020 Habari
  • Hadi Desemba mwaka jana kulikuwa na vituo 183 vya redio nchini kutoka vituo 158 mwaka 2018.
  • Redio ni moja ya vyanzo vikubwa vya habari kwa Watanzania.

Dar es Salaam. Licha ya kuongezeka kwa changamoto za kifedha zinazoendelea kuvikabili vyombo mbalimbali vya habari duniani, idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 25 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza katika ripoti mpya ya mawasilino ya robo ya mwisho ya mwaka 2019 kuwa hadi Desemba mwaka jana kulikuwa na vituo 183 vya redio nchini kutoka vituo 158 mwaka 2018.

Uchambuzi wa mwenendo wa takwimu za vituo vya redio uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) unaonyesha kuwa vituo vingi vya redio vilizaliwa mwaka 2016 baada ya vituo 42 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.

Hata hivyo, mwaka 2018 ndiyo mwaka ambao vituo vichache zaidi vilianzishwa ndani ya mwaka mmoja kutokana na kuongezeka kwa vituo viwili tu vya redio kutoka 156 mwaka 2017 hadi 158 mwaka 2018.


Kwa takwimu hizo, ongezeko la vituo vya redio mwaka jana ndiyo la pili kwa kubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka sita iliyopita.

Hata hivyo, takwimu hizo hazihusishi vituo vya redio vya mtandaoni na haziweki bayana aina ya vituo hivyo katika makundi kama vya kijamii, kidini au kitaifa.


Zinazohusiana:


Hivi karibuni Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa Dk Harrison Mwakyembe alisema hadi Februari 12 kulikuwa na vituo vya redio 204 vikiwemo 21 vya mtandaoni.

Redio ni moja ya aina ya vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi zaidi nchini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za hivi karibuni.

Ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Repoa wa Afrobarometer wa mwaka 2017 inabainisha kuwa redio ndiyo chanzo maarufu cha habari miongoni mwa Watanzania baada ya matokeo kubainisha watu 45 kati 100 hupata habari kupitia redio kila siku.

Licha ya utafiti kueleza kuwa sehemu kubwa ya watu Tanzania hupata habari kutoka redioni, Kitabu cha ubora wa habari cha mwaka 2017 (Yearbook in Media Quality in Tanzania 2017: What do we know?) kinabainisha kuwa habari za redioni bado zina ubora hafifu.

Related Post