Uzushi: WHO haijatangaza nafasi ya kazi kupambana na Corona
- Shirika hilo la afya duniani limezushiwa kuwa limetangaza nafasi ya kazi kwa watu kusaidia mapambano dhidi ya COVID-19.
- Shirika la Afya Duniani limesema fursa zote za ajira hutolewa na tovuti yake ya who.int na si vinginevyo.
- Yawataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa makini na matapeli wanaotumia COVID-19 kujinufaisha.
Dar es salaam. Upepo wa habari za uzushi kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona unaendelea kuvuma kila mahali duniani. Na sasa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limezushiwa kuwa limetangaza nafasi ya kazi kwa watu kufanyia kazi nyumbani katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.
Katika tangazo hilo ambalo linasambazwa katika mitandao ya kijamii linaeleza kuwa uzoefu hauhitajiki kwa mtu kupata kazi hiyo lakini habari hiyo haina ukweli wowote na ni uzushi uliotungwa na watu wenye nia mbaya.
Habari hiyo ilichapishwa kwa lugha ya Kiingereza katika mtandao wa Facebook ikisema “JOB AT WORLD HEALTH ORGANISATION, Help us fight CORONAVIRUS by working from home – No experience required SMS sending JOB, *Work 2-3 hours daily on mobile*, *and earn $5-$100 daily* Click Here And Apply Now. Vacancy till 31st July, 2020.”
Zinazohusiana:
Kwa tafsiri isiyo rasmi inamaanisha kuwa: Tangazo la kazi katika Shirika la Afya Duniani, Tusaidie kupambana na ugonjwa wa Corona kwa kufanya kazi nyumbani. Uzoefu hauhitajiki kinachotakiwa ni kutuma ujumbe wa simu kwenda KAZI (JOB) *Muda wa kufanya kazi ni saa 2-3 kwa siku kupitia simu yako ya mkononi na utalipwa kuanzia dola za Marekani 5 hadi 100 kila siku. Bonyeza hapa kisha uombe sasa. Mwisho wa kutuma maombi ni Julai 31, 2020.
Ukweli ni upi?
Taarifa hiyo siyo ya kweli ni ya uzushi au famba. Timu ya Nukta Fakti imebaini kuwa WHO halijawahi kutoa habari ya namna hiyo mahali popote pale.
Pia WHO tayari imekanusha habari hiyo na kuwataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kupuuza tangazo hilo la kazi kwa sababu taarifa zote za shirika hilo huchapishwa katika tovuti ya who.int na siyo mahali pengine.
Ili kukabiliana na habari za uzushi kama hizo, WHO imeanzisha jukwaa maalum ili kubaini na kupambana na taarifa za uzushi ambapo jukwaa hilo linatoa mafunzo ya kuwawezesha watu kujiweka salama wakati huu wa mlipuko wa COVID-19 dhidi ya matapeli na wapotoshaji.
Latest