Tanzania itakavyofaidika na uwekezaji kutoka Uingereza

Lucy Samson 0356Hrs   Machi 23, 2023 Habari

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba (wa pili kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna wa Biashara wa Uingereza anayesimamia Kanda ya Afrika, John Humphley ( wa pili kulia), baada ya kumaliza mazungumzo ya kikazi katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Jijini London, Uingereza. katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dk  Asha-Rose Migiro. Picha | Wizara ya Fedha na Mipango. 


  • Shirika la bill lasema lipo tayari kuongeza uwekezaji Tanzania.
  • Uwekezaji huo utalenga uwekezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele.
  • Utachochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa Watanzania.

Dar es Salaam. Shirika la Kimataifa la Uwekezaji la Uingereza (BII), limesema litaongeza kiwango cha uwekezaji katika miradi ya kipaumbele  ili kukuza na kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Shirika hilo limetoa ahadi hiyo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kutoa wito kwa shirika hilo kuongeza uwekezaji wake nchini Machi 22, 2023 alipokutana na menejimenti ya shirika hilo Jijini London, nchini Uingereza.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, kilimo, utalii, madini, viwanda na huduma pamoja na rasimali za asili kama vile gesi na maji kwa ajili ya kuzalishaji wa nishati.

Ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, madini pamoja na hali ya amani nchini, ambavyo kiujumla vinaweka mazingira ya kuvutia kiuwekezaji,” amesema Waziri Nchemba. 

Kati ya miradi ya kipaumbele iliyoanishwa ni pamoja na program ya uchumi wa bluu inayohitaji uungwaji mkono wa taasisi za fedha za kimataifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa BII, Chris Chijiutomi ameihakikishia Tanzania kuwa iko shirika lake liko tayari kuongeza uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwa ni sera ya Serikali ya Uingereza ya misingi ya kuanzishwa kwa shirika hilo.

Chijiutom amesema BII bado ina mtaji wa kutosha kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kwa  kushirikiana na sekta binafsi.

BII lina mtaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 11(Sh25.7 trilioni) lakini imewekeza Tanzania Dola za Marekani milioni 215 (Sh503.3 bilioni).


Soma zaidi:


Ameitaka Tanzania kuainisha miradi ya kipaumbele ambayo shirika hilo litachambua na kutoa fedha kwa kushirikiana na sekta hiyo binafsi.

Kufutia ahadi hiyo Waziri Nchemba ameialika timu ya wataalamu kutoka BII kuitembelea Tanzania na kufanya mazungumzo na taasisi, mashirika mbalimbali pamoja na sekta binafsi ili kuangalia maeneo ya kuwekeza kwa faida ya pande zote zinazohusika.

Ziara ya Waziri Nchemba nchini Uingereza ni muendelezo wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutafuta fedha kwa ajili ya miradi na uwekezaji  katika  sekta mbalimbali nchini.

Hivi karibuni waziri huyo alisaini mikataba mbalimbali ya uwekezaji ukiwemo  mkopo wa Sh647.5 bilioni kutoka kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa  (AFD), uliolenga kufadhili mradi wa umeme wa maji wa Kakono mkoani Kagera.

Related Post