Rais Samia awataka mabalozi kufanya kazi kwa matokeo, si matukio
- Asisitiza kufanya kazi kwa kutanguliza na kulinda maslahi ya Tanzania.
- Aitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuunda mfumo wa kufuatilia shughuli za mabalozi.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewataka mabalozi wanaoiwakilisha nchi katika maeneo mbalimbali kufanya kazi zenye matokeo chanya kwa maslahi ya Taifa, huku akikemea tabia ya kusubiri matukio pekee.
Kwa mujibu wa Rais Samia baadhi ya mabalozi hawatekelezi majukumu yao ipasavyo bali hushiriki katika baadhi ya matukio yanayoihusu nchi husika kama sherehe za uhuru ama wakati wa kupokea ujumbe wa Tanzania.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha mabalozi aliowateua Agosti 11, 2023 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, amewaambia Tanzania inataka kuona matokeo chanya ya kazi zao na si kuketi ofisini pekee huku wakilipwa fedha.
“Kwa ujumla niseme nendeni mkafanye kazi kwa matokeo, msisubiri matukio ili kupata kazi ya kufanya, mtengeneze mpango kazi tuone matokeo ya kazi mnayoifanya kule, vinginevyo hatuna rasilimali za kumpa mtu aende huko kukaa na familia yake, ana-’enjoy’ tu … pesa yetu ilipe kinachotokea kule” amesisitiza Rais Samia.
Ili kurahisisha ufuatiliaji wa shughuli za mabalozi Rais Samia ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje kutengeneza mfumo maalumu unaoonesha kazi na ufuatiliaji unaofanywa ambao utakuwa unafuatiliwa na Rais, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu.
Soma zaidi
-
Rais Samia aagiza matumizi namba moja ya utambulisho Tanzania
-
Ujuzi wa kidijitali unaoweza kuwatoa vijana kimaisha
Rais nchi za SADC aomba kubadilishiwa balozi
Tukio lilivotuta hisia za wengi katika hafla hiyo ni pale Rais Samia alipobainisha kwamba kutokana na utendaji mbovu wa aliyekuwa balozi wa Tanzania katika moja ya nchi zilizopo kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Rais wa nchi hiyo alimuomba ambadilishe.
“Nilishakutana na Rais mwenzangu ndani ya nchi za kiafrika, ndani ya Sadc, akaniambia nimbadilishie balozi, akisema uliyeniletea hata kazini haendi, mikutano hashiriki, yupo yupo tu, hatuelewi, Tanzania hatujawazoea hivyo, sasa labda umbadilishe, nikamwambia nimekusikia,” amesema Rais Samia.
Mabalozi walioapa
Miongoni mwa mabalozi walioapa hii leo ni pamoja na Balozi Gelasius Byakanwa aliyepangiwa nchini Burundi, Balozi Habib Awesu Mohamed nchini (Qatar), Balozi Imani Njalikai (Algeria),na Ramson Mwaisaka (Rwanda).
Wengine ni Hassan Mwamweta (Ujerumani), na Mohamed Juma Abdallah (Saudi Arabia), ambao wamesisitzwa kulinda na kutanguliza maslahi ya Tanzania.
Latest



