Picha ya mwaka 2018 inavyotumika kutoa 'tiba' feki ya covid -19

Mwandishi Wetu 2322Hrs   Mei 08, 2020 NuktaFakti
  • Ilichapishwa kwa mara ya kwanza Mei 29, 2018 lakini imeibuka tena wakati wa corona.
  • Picha hiyo  imetoa yanayodai kuwa ni maelekezo ya namna ya kujitibu vidonda hivyo ili kuepuka madhara zaidi.

Dar es Salaam. Tangu ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) uibuke ulimwenguni kumekuwa na nadharia mbalimbali za jinsi ugonjwa huo ulipoanzia au hata  unavyosababisha madhara kwa watu walioambukizwa.

Nadharia hizo zimesababisha baadhi ya watu kutumia mitandao ya kijamii vibaya kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu athari za COVID-19 kwa kujua au kutokujua.

Kwa sasa, ipo picha inayoonyesha sehemu ya mdomo na koo la mtu lenye vidonda lukuki huku ikiwa na ujumbe unaoelezea kuwa ni moja ya dalili ya Corona.

Pia picha hiyo imetoa maelekezo yanayodai kuwa ni namna ya kujitibu vidonda hivyo ili kuepuka madhara zaidi.

Picha ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na maelekezo ya namna ya kujitibu vidonda mdomoni  ili kuepuka madhara zaidi lakini imebainika kuwa siyo kweli. Picha|Mtandao.

Nukta Fakti imebaini kuwa taarifa hiyo si ya kweli na inalenga kupotosha na kuibua taharuki kwa watu wakati huu dunia ikiendelea kupambana na kutokomeza ugonjwa huo hatari.

Kwanini ni uzushi?

Timu ya Nukta Fakti imebaini kuwa picha hiyo inayozagaa mtandaoni hasa WhatsApp na Facebook imekuwepo zaidi ya miaka miwili iliyopita  kabla ya kuripotiwa kwa ugonjwa wa Corona mwishoni mwa mwaka 2019.

Matokeo ya utafiti uliofanywa kupitia dhana za kidijitali (Reverse Image), unaonyesha kuwa picha hiyo ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika mtandao wa kijamii wa Reddit Mei 29, 2018.

Picha hiyo iliambatana kichwa habari “Is this normal looking strep throat? Lots of white spots on tonsils and even on the back of my throat,” ikiwa na maana kuwa “Hii ni kawaida kwa koo kuoneka hivi? Madoa mengi meupe kwenye mdomo na hata nyuma ya koo”

Habari na picha zilizotumika katika mtandao wa Reddit hazikuwa na uhusiano wowote na athari za Corona kwa viungo vya mwanadamu.


Zinazohusiana:


Baada ya siku chache, mtu aliyetuma ujumbe huo kwenye mtandao huo alituma tena ujumbe ya majibu yake baada ya kupata vipimo  kutoka hospitali kuwa madaktari walibaini ni tatizo linalosababishwa na bakteria aina ya MRSA.

Kwa mujibu  wa taasisi ya magonjwa ya Marekani (Centers for Disease Control and Prevention), MRSA ni aina ya bakteria ambaye husababisha aina mbalimbali za dawa za kuua bakteria (antibiotics) kushindwa kufanya kazi.

Pia Dk Gaudence Mathew kutoka hospitali ya Decca Poliyclic iliyopo jijini Dodoma ameiambia Nukta Fakti kuwa vindonda hivyo havina uhusiano na virusi vya COVID-19.

“Siyo kweli na huwezi tambua hizo tonsesi ni za corona au la. Hizo tonsesi zinaonekana siyo za leo ni za muda mrefu,” amesema Dk Mathew.

Daktari wa epidemioloji na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Jamii Dkt Fernando De La Hoz kutoka Chuo Kikuu Cha Colombia aliliambia Shirika la Habari la AFP hivi karibuni kuwa vidonda hivyo kwenye picha vinaonekana vinahusiana na bacteria

“Hi siyo aina ya virusi vya corona," amesema Dkt Fernando.

Hii inaonyesha siyo kila kitu unachokiona mtandaoni kinaukweli kabla ya kusambaza jiulize mara mbili.

Endelea kuzingatia masharti yote yanayotelewa na Serikali pamoja na wahudumu wa afya ikiwemo kunawa mikono na sabuni na maji yanayotirirka kila mara, vaa barakoa na jizuie na Safari zisizo za lazima.

Related Post