Mbinu zitakazosaidia kutokomeza ukeketaji Tanzania

February 7, 2023 11:00 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Adhabu na kifungo kwa wazee na mila na wazazi wanaoshiriiki kwenye ukeketaji vyapendekezwa.
  • Wanajamii watakiwa kutoa ushirikiano kumaliza ukeketaji nchini.

Dar es Salaam.Mtandao wa kupinga ukeketaji Tanzania (TCAFGM) umetoa mapendekezo kwa Serikali, wanajamii na wadau mbalimbali juu ya jinsi ya  kutokomeza vitendo vya  ukeketaji vinavyoendelea kwenye baadhi ya maeneo nchini.

TCAFGM  imependekeza kufanyika kwa maboresho ya sheria  na kanuni za adhabu mbalimbali ikiwemo kuongeza adhabu kwenye makosa ya ukeketaji katika kifungo au faini.

Getrude Dyabene  ambaye ni Mratibu wa mtandao  huo aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo hayo leo Januari 7, 2023 jijini Dar es Salaam amewaambia wanahabari maboresho ya sheria yajumuishe  adhabu kwa wazazi, wazee wa mila na wote wanaohusika na vitendo hivyo.

“Tunataka hadi wale wanaoshiriki kusherekea hizo sherehe wakamatwe…wazazi na wazee wamila ndio wenye ushawishi katika kuendeleza mambo ya ukeketaji na wao wakamatwe,” amesema Dyabene.

Mbali na mabadiliko ya sheria hizo mtandao huo unaishauri Serikali kutekeleza kwa vitendo mpango kazi wa kikanda wa nchi tano  kuhusu ukeketaji unaovuka mipaka. (The regional cross border declaration action plan).

Mpango kazi huo utapanua mawanda ya ufanyaji  kazi wa jeshi la polisi na wanaharakati kuripoti na kuwakamata wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili ndani na nje ya nchi.

“Serikali kusimamia kikamilifu sheria kuhakikisha watekelezaji wa vitendo vya ukeketaji wanakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi, “ amesema Dyabene.


Soma zaidi


Mbali na jitihada za wadau binafsi katika kupambana na  ukeketaji TCAFGM imeitaka Serikali kudumisha ushirikiano na taasisi zisizo za kiserikali pamoja na mashirika rafiki ya kimataifa ili kutokomeza kitendo hicho cha kikatili kwa wasichana.

Aidha, viongozi wa ngazi za juu ikiwemo wabunge na wakuu wa wilaya wanaotokea kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na ukeketaji wametakiwa  kuunga mkono jitihada zinazoendelea ili kunusuru mabinti na wanawake na athari zitokanazo na janga hilo.

“Ukienda Mara hadi waheshimiwa Wabunge hawakusapoti, wanasema hawawezi kuongelea hayo masuala ila hatuyapendi,” ameongeza mratibu huyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum , Mikoa yenye takwimu za juu za ukeketaji ni pamoja na Manyara  asilimia 58, Dodoma (asilimia 47),Arusha (asilimia 41), Mara (asilimia 32); na Singida asilimia 31.

Wanajamii amkeni

Mtandao huo umewaataka wanajamii wote kwa ujumla kusimama kwa pamoja kupinga vitendo hivyo vyenye kunyanyasa wanawake na mabinti  na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa na ushahidi  watakapohitajika.

 Kwa jamii ambazo bado hazina elimu kuhusu madhara ya ukeketaji Mtandao huo umewataka wadau mbalimbali kushirikiana kupeleka elimu ili kupunguza ukeketaji kwenye maeneo hayo.

Enable Notifications OK No thanks