Lhrc yajitosa tume ya kufuatilia mfumo wa haki jinai Tanzania

February 2, 2023 12:02 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Waanisha taasisi zilizosahaulika ambazo zinazotakiwa kumulikwa.
  • Wasema haki jinai ni jambo la kupewa kipaumbele kwa sasa. 
  • Wagusia pia sheria ambazo zinakandamiza haki jinai. 

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu kuunda Tume ya Maboresho ya Taasisi za Haki Jinai nchini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimependekeza tume hiyo izifikie taasisi nyingi ikiwemo Jeshi la Uhamiaji ili ipate matokeo mazuri yatakayosaidia kulinda haki za raia.

Taasisi nyingine zilizopendekezwa  kufanyiwa mapitio na tume  teule ni  Shule ya Maadilisho (Approved schools), Ofisi ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Kamati ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu.

Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo hayo mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam leo Februari 2, 2023 amesema licha ya nia ya dhati ya Rais Samia kuimarisha mifumo ya haki jinai nchini ni vyema kuzingatia mapendekezo ya maboresho ya taasisi hizo ili kulinda haki za binadamu.

“Haki jinai tunakutana nazo kila siku, ni kitu cha msingi ambacho kinatakiwa kupewa kipaumbele, tume itoe nafasi kwa watu kutoa maoni kwa ajili ya kufanya maboresho kwenye mfumo wa haki jinai,” amesema Wakili Henga.


Soma zaidi


Sheria nazo zimulikwe

Wakili Henga amesema tume hiyo isiishie tu kwa taasisi husika bali izifanyie pia tathmini  baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikichangia ukiukwaji wa haki jinai. 

LHRC imezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya ya mwaka  2015, Sheria ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (2007), Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi (Sura 200) na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.

Nyingine ni Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya mwaka 2008, Kanuni ya Adhabu (Sura 16 ), Sheria ya Makosa ya Mtandaoni (2015), Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ( 2016) na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka  2009.

Amesema sheria hizo zikipitiwa na kuboreshwa ili kuendana na mazingira ya sasa zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa mfumo wa haki jinai nchini. 

Januari 6, 2023 Rias Samia aliteua Tume ya kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, inayoongozwa na Mwenyekiti Jaji Mohamed Othman Chande na Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue.

Tume hiyo iliyozinduliwa Januari 31, 2023 oitafanya kazi kwa miezi minne na kuja na mapendekezo ya nini kifanyike kuboresha mfumo wa haki jinai katika taasisi zinazohusika kutoa haki ikiwemo mahakama na Jeshi la Polisi. Pia itaangazia mapungufu yaliyomo ndani ya taasisi hizo na yanavyoathiri utolewaji wa haki kwa wananchi.

Enable Notifications OK No thanks