Maduka ya simu Makumbusho yaibua mjadala mpana wa bei, ubora

September 22, 2019 4:55 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wafanyabiashara wamesema ubora wa simu unategemea bei na aina ya simu inayouzwa. 
  • Waranti za simu na wasambazaji wa vifaa vya simu nao waguswa. 
  • Wataalam watoa mbinu za kutambua simu feki na zisizo na ubora. 

Dar es Salaam. Kumekuwa na habari mtandaoni kuwa maduka ya simu ya Makumbusho ni miongoni mwa yale yanayouza simu za janja hasa za kama iPhone na Samsung kwa bei rahisi. 

Hata hivyo, imekuwa ni vigumu kufahamu kwa kiwango gani simu hizo ni nafuu na kwa ubora gani. 

Safari ya kuichambua biashara ya simu katika kituo cha daladala Makumbusho Jijini Dar es Salaam inaendelea  na leo tunaangazi ukaribu biashara hiyo ambayo ni nguzo muhimu katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini. 

Uchambuzi wa biashara hiyo uliofanywa na www.nukta.co.tz umebaini kuwa karibu maduka yote ya simu yaliyopo Makumbusho yanauza zaidi simu aina ya Iphone na Samsung. Hata hivyo, yapo baadhi yanayouza nembo nyingine kama Tecno, Infnix, Itel  na Huawei. 

Mbali na kuwa kuwa kuna simu nyingine zinazouzwa eneo hilo, umaarufu wa maduka hayo kwa sasa upo zaidi katika uuzaji wa simu za Iphone huku wauzaji wakieleza kuwa “ndiyo simu zinazotafutwa zaidi na vijana wanaoenda na wakati”. 

“Lazima ujitofautishe na wengine mimi nauza Iphone pekee,” anasema Andrew Thomas ambaye duka lake linatazamana na mlango wa kutokea wa kituo cha daladala cha Makumbusho. 

Sababu kubwa ya Iphone na Samsung kutawala biashara ya maduka hayo ni kutokana na aina ya wateja wanaotembelea maduka hayo ambao ni wa kipato cha kati (middle income) ambao kipato chao kinawaruhusu kununua simu za gharama kubwa na zenye hadhi. 

Wafanyabiashara wanaeleza kuwa ukaribu wa kituo hicho na maeneo ya Kijitonyama, Bamaga na Mikocheni ambako wanaishi watu wenye kipato kizuri, umerahisishia kufuata simu Makumbusho. 

Tony Mlangila, mfanyabiashara mwingine wa simu katika kituo hicho, anasema simu zinazonunuliwa zaidi ni Iphone 6S kwa sababu zina kioo na uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu vingi.

“Unajua mtu anajisikia fahari kama ana simu kubwa kuliko zile ndogo, halafu tena ikiwa Iphone ambayo bei yake inaimudu, basi utakuta hizo 6S zina wateja wengi,” amesema Mlangila. 

Baadhi ya watumiaji wa simu za Iphone wameiambia www.nukta.co.tz kuwa simu hizo zinajipatia umaarufu kwa sababu zinamfanya mtu aonekane wa hadhi ya juu na zinamuhakikishia usalama na usiri wakati atumiapo. 

Mtaalam wa Programu wa kampyuta kutoka Shirika la Code for Africa, Clemence Kyara anasema amekuwa akitumia Iphone kwa muda mrefu kwa sababu taarifa zake ziko mahali sahihi tofauti na simu zingine ambazo ni rahisi wadukuzi kupenya. 


Zinazohusiana:  


Ubora na bei za simu za Makumbusho zinaibua mjadala

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuwa simu zinazouzwa Makumbusho hazina ubora jambo linalofanya zisidumu kwa muda mrefu.

Malalamiko mengine ni pamoja na kuuziwa simu feki ambazo haziendani na bei wanayolipa au zingine kuharibika mapema kinyume na matarajio ya wanunuzi.

Suala hili la kuuziwa simu zisizo na ubora hasa Iphone limeibua pia mjadala kwenye mitandao ya kijamii ukiwemo wa Twitter.

Baadhi ya wachangiaji wa Twitter wamesema Iphone zinazouzwa Makumbusho siyo mpya bali ni zilizofanyiwa maboresho lakini zinauzwa kwa bei kubwa. 

“So mlisema zile iPhone za Makumbusho ni Refurbished? (zimeboreshwa). Kuna Rafiki yangu ananiaga hapa kwamba anaenda kununua🤦 Mna mshauri nini,” amesema @MoshaAzalina.

Wengine wamefikia hata hatua ya kuzifanyia mizaha simu hizo za Iphone zinazouzwa Makumbusho wakiamini hazina ubora na simu mpya haziwezi kupatikana katika eneo hilo, jambo ambalo wafanyabiashara wa bidhaa hizo Makumbusho wamelikanusha vikali. 

“Bro hii kwani inawahusu hadi wale wenye IPhone za makumbusho au ni wale walio nunua mcity tu… 😂,” ameandika @CharlieBihemo katika mtandao huo. 

 Wafanyabuashara wa simu Makumbusho wamesema ubora wa simu unategemea mambo mengi ikiwemo aina ya simu ambayo mteja anaitaka na kiasi cha pesa alichonacho. 

Mfanyabiashara mmoja wa simu ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wapo wateja wanaotaka simu zenye ubora mkubwa wakati kiasi cha pesa wanacholipa ni kidogo.

Anasema simu zinazouzwa Makumbusho ziko kwenye makundi matatu; simu mpya (new phones); zilizoboreshwa (refurbishment) na zilizotumika (used one) ambazo zinatoka katika nchi zilizoendelea kama China na Saudi Arabia. 

Mfanyabiashara huyo ambaye duka lake linauza simu za Samsung na Iphone, anabainisha kuwa wanunuzi wa simu mpya ni wachache kwa sababu bei za simu hizo iko juu.

Kutokana na hali hiyo, wao kama wafanyabiashara huingiza sokoni zaidi simu zilizoboreshwa kiwandani kwa sababu zinaonekana kama mpya na bei yake inaweza kumfaidisha muuzaji na manunuzi. 

“Hizo zote zinapatikana ila kwa wauzaji wengi simu ambazo zinapendelewa ni refurb (zilizoboreshwa) kwa sababu zenyewe zinaenda kufanyiwa maboresho zinatoka kama mpya tena,” anasema.

Hata hivyo, wafanyabiashara wengine walioongea na nukta.co.tz wamesema wakati wa kuuza simu hizo, hawamwambii mteja daraja la simu kwa sababu uelewa wa wateja unatofautiana na lengo lao ni kupata faida. 

 Usambazaji na waranti za simu bado kitendawili

Ubora wa simu pia hutegemea na bei ya wasambaji wa mzigo kwa wafanyabiashara hao, kwa sababu biashara ya simu haina msambazaji mmoja. 

Lakini pia ubora wa simu hutegemea mzigo umetoka kwa nani, jambo linaloibua changamoto kwa wanunuzi na wauzaji ambao muda mwingine hawajui simu iko katika hali gani. 

“Biashara ya simu kwa ujumla haina ‘supplier’ (msambazaji) mmoja, ina suppliers wengi, sasa ukija sokoni kwenye ushindani, kama wewe supplier wako anauza kwa bei juu unakutana na mwingine ambaye supplier wake amempa kwa bei ya chini…utajikuta mwenzako anauza zaidi kuliko wewe,” amesema mfanyabiashara simu Makumbusho,  Tony Mlangila. 

Nukta imebaini kuwa sehemu kubwa ya bei za simu zinauzwa Makumbusho huanzia Sh200,000 hadi zaidi ya Sh3 milioni kutegemeana na upya, uwezo, ukubwa na aina ya simu unayonunua. 

Kwa mfano, Iphone6 ambazo zinanunuliwa sana zinauzwa kati ya Sh400,000 hadi Sh500,000 huku zile za Iphone 6 Plus ni Sh500,000 hadi Sh600,000. 

Mlangila amesema waranti za simu pia zinaweza kuathiri bei na ubora wa simu wanazouza sokoni. Baadhi ya simu haziji na waranti hasa zilizotumika, jambo linalowapa changamoto wanunuzi kusema simu za Makumbusho hazina ubora. 

Amebainisha kuwa wateja wengi hawaelewi hilo suala licha ya kuwa wanakuwa wametoa pesa kidogo lakini wanajitahidi kuwaweka sana kuhakikisha kile anachokipata mteja kinaendana na pesa aliyoitoa. 

“Kinaweza kutokea chochote hapo mteja anaweza akakuelewa au asikuelewe. 

“Kuna ishu ambazo zinatokea, supplier (msambazaji) anaweza kukuambia hii simu haiko kwenye warranti lakini mteja hakuelewi pengine kutokana na usumbufu ambao umejitokeza anaenda hadi kukuchukulia polisi huko unatupwa ndani,” amesema Mlangila. 

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamesema wanafanya kila namna kuhakikisha wanatoa huduma bora za simu ili kujenga mahusiano mazuri na wateja wao ili tatizo likitokea inakuwa rahisi kutafuta ufumbuzi. 

Licha ya changamoto zinazojitokeza haziwezi kuikwamishwa Makumbusho kuwa kitovu au kituo kikubwa cha simu za mkononi jijini Dar es Salaam ikizingatiwa ni eneo ambalo liko kimkakati. 

Wakati kituo hicho kikikuwa kwa kasi, wadau wanaojihusisha na biashara ya simu wanatakiwa kushughulikia baadhi ya changamoto zikiwemo za bei na ubora wa simu zinauzwa ili kuendelea kujenga uaminifu na  imani kwa watu.

Sababu kubwa ya Iphone na Samsung kutawala biashara ya maduka hayo ni kutokana na aina ya wateja wanaotembelea maduka hayo ambao ni wa kipato cha kati (middle income) ambao kipato chao kinawaruhusu kununua simu za gharama kubwa na zenye hadhi. Picha|Mtandao.

Jinsi ya kugundua simu feki

Mtaalam wa masuala ya teknolojia na mawasiliano (Tehama), Emmanuel Feruzi amesema zipo mbinu mbalimbali ambazo wanunuzi wa simu wanaweza kuzitumia ili kubaini simu yenye ubora au original (mpya) ikiwemo muonekano wa mbele wa simu husika.

Feruzi ambaye ni mtumiaji wa simu za IPhone kwa muda mrefu sasa, amesema simu hizo zinakua na muonekano mzuri unaong’aa tofauti na simu feki ambazo rangi yake inakuwa imefubaa. 

Wakati mwingine unaweza kupima ubora wa simu kwa uzito wake, kwa mujibu wa Feruzi, Iphone zina uzito fulani ambao ni tofauti na simu zingine, jambo linaloweza kumsaidia mtu anayetumia simu hizo kutotapeliwa kirahisi.

“Muonekano wa kioo (display) ya simu mpya ni mzuri lakini hizo feki utakuta kioo chake kimefifia yaani haivutii sana licha ya kuwa watengenezaji wanajitahidi kuziweka katika muonekano ambao unafanana sana na simu mpya,” amesema Feruz.

Mbinu nyingine ambayo ni ya kiufundi zaidi ni kuifungua simu hadi sehemu ya “setting” ili kupata taarifa za simu ikiwemo aina, watengenezaji, toleo na namba ya usajili.

Enable Notifications OK No thanks