Kutana na vijana wanaoipa thamani nyumba yako kwa 'taka'

Daniel Mwingira 0511Hrs   Januari 02, 2018 Biashara

Baadhi ya wateja wa Kichupa wakionyesha bidhaa walizonunua hivi karibuni. Bidhaa hizi za taka za chupa zimeanza kuwa maarufu nchini.

  • Huzitia nakshi taka za chupa kiasi cha kugeuka mapambo ya kuvutia katika makazi.

Dar es Salaam. Umeshawahi kupata nafasi ya kutafakari juu ya maisha yako hapa duniani? Umeshawahi kuutathmini mchango wako katika jamii inayokuzunguka au Taifa lako?

Kama bado unatafakari, huko Sakina Azimio mkoani Arusha kuna vijana wamebuni mradi wa kupunguza taka za chupa za kioo ambao mbali na kusaidia kupunguza uchafu nchini uinasaidia kuwaingizia kipato.

 Hatua ya vijana hao Gerald Josepht (28) mwenye Shahada ya uhusiano na viwanda kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Mafita Jordan (29) mwenye shahada ya manunuzi ya umma kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha, Erick Matemu (29) mbunifu kwenye sanaa na Alfred Simon ambaye ni muungoza watalii imelenga kutumia chupa ambazo awali zilikuwa hazina thamani yoyote.

Miaka ya hivi karibuni imezoeleka kuona chupa za plastiki zilizotumika zikiokotwa na kuuzwa kwa wingi kwa ajili ya kuzirejeresha. Ila siyo kawaida kuziona chupa za kioo zisizorudishwa baada ya kutumika zikiokotwa kwa wingi kama zile za plastiki na kuzifanya zizagae mitaani. Thamani ya chupa hizo huisha baada ya kinywaji kutumika.

Hata hivyo, vijana hao wa kikundi cha Visionary Youth Network kwao chupa za mvinyo, Whisksy, Konyagi shampeni ni zaidi ya kinywaji na mara nyingine hawajui watazipata wapi kutokana na mahitaji kukua.

Sehemu ya bidhaa zinazotengenezwa na kundi la vijana wa Visionary Youth Network. Bidhaa hizo huchorwa michoro mbalimbali ya kuvutia ili kuzipa thamani taka za chupa. 


Biashara rafiki kwa mazingira

Tofauti na kampuni zinazorejeresha chupa za vioo, wao wanazitumia kutengeneza mapambo ya kuvutia ambayo yanafaa kuwekwa sehemu yoyote ya nyumbani, ofisini, hotelini na kwenye kumbi mbalimbali za starehe na burudani.

Vijana hao, ambao ni wasanii wa uchoraji, huchukua chupa zilizotumika, huziosha na kuzipaka rangi kabla ya kuchora maua na maandishi yenye ujumbe wa aina mbalimbali jambo linalofanya chupa hizo zionekane kama zilitengenezwa maalum kwa ajili ya mapambo.

‘’Leo tumezipa thamani chupa za vioo kwa kuzitengezea urembo na kuziuza lakini pia tunatunza mazingira ili kuendana na malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi,” anasema Josephat.

“Hii ni kwa kuwa chupa za vioo haziozi hivyo kwetu kuzitumia kama mapambo ni furaha ili mazingira yawe mazuri zaidi.”

Josepht alipata wazo hilo la kuchora katika chupa za vioo baada ya kujitolea katika Shirika lisilo la kiserikali la Raleigh Tanzania lenye makazi yake Morogoro ambapo ili kutunukiwa cheti ilibidi kuja na mradi nje ya shirika hilo kupitia programu inayoitwa ‘Home action’.

Chupa hizo huzipata katika baa au hoteli ambazo huwa wanazitupa. Wakati mwingine, Josephat anasema husaidiwa na mtu anayefanya kazi katika hoteli ya kitalii ambaye huwakusanyia kidogo na kuwapelekea vinginevyo hutakiwa kuzinunua kutoka kwa waokota makopo.


Watumia teknolojia kuboresha Sanaa

Kutengeneza chupa moja mpaka ikamilike huchukua saa mbili ambazo ujumuisha kuiandaa chupa na kuanza kubuni mchoro wenyewe kwenye kompyuta na kuichapisha. Tofauti na wachoraji wanaotumia mkono kuchora, Josephat na wenzie hutumia teknolojia ya program ya kompyuta ya Adobe kusanifu maua na baadaye huchapisha michoro hiyo katika stika na kuibandika katika chupa.

Mara nyingi muda wa kukamilisha kuandaa chupa moja hutegemea na aina ya mchoro. Mchoro ukiwa na mambo mengi na rangi nyingi basi muda nao huwa mrefu

anasema Josepht.

Chupa iliyosanifiwa katika pambo maridhawa hugharimu kati ya Sh10,000 mpaka Sh15,000 inategemea na idadi ya oda husika ambayo mteja ameomba kutengenezewa.




Soko bado changamoto

Josephat anaeleza kuwa huwa wanachora pia kutokana na matukio iwe harusi, sendoff au sherehe yoyote. Mfano katika sikukuu hii ya Krisimasi iliyopita walikuwa na bidhaa maalum waliyoipa jina “Kichupa cha Krisimasi” ambacho walikiiuza sehemu mbalimbali nchini hadi jijini Dar es Salaam.

 ‘’Soko bado dogo lakini tunauza kidogo ingawa ndoto yetu ni kupata soko la kutosha katika sekta ya utalii ambapo Arusha ni kitovu chake,’’anasema Josephat anayesema kuwa tayari wameshauza zaidi ya oda zisizopungua 30 tangu Juni walipoanzisha biashara hiyo.

Kwa siku, kundi hilo lina uwezo wa kuzalisha chupa 12 kwa siku. Hata hivyo, uzalishaji huo huathirika kutokana na kukosa soko la uhakika na kwa mujibu wa Josephat kukiwa na oda nyingi wanaweza kuzalisha zaidi kiwango hicho kwa siku.

"Nawaomba wadau wote washirikiane nao kuanzi hao wa utalii mpaka serikalini hususan Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira walione wazo letu katika jicho la kipekee," anasema.

Kwa mujibu wa utafiti wa Joshua Palfreman wa mwaka 2013 zaidi ya tani 50,000 za vioo huzalishwa kila mwezi nchini hii ukiachana na bidhaa kama hizo zinazoingizwa kutoka nje.

Katika utafiti huyo unaoitwa Usimamizi wa Taka na Urejereshaji jijini Dar es Salaam (Waste Management and Recycling in Dar es Salaam, Tanzania), Palfreman anaeleza kuwa asilimia 90 ya taka za vioo hurejerezwa na kampuni kubwa za vinywaji na utengenezaji chupa kipitia Kioo Ltd wakati kiwango kilichosalia hurejerezwa waokota taka binafsi.  

Mapambo hayo ya chupa yanaweza kuwekwa pia katika kumbi za hoteli au baa kupendezesha mandhari. Picha zote kwa hisani ya Visionary Youth Network.

Related Post