Kinara kidato cha nne 1990 awapa changamoto wanafunzi wanaoendelea na masomo Tanzania

Daniel Samson 0603Hrs   Januari 31, 2019 Ripoti Maalum
  • Ni Mgaywa Magafu, Daktari wa magonjwa ya binadamu aliyekuwa mwanafunzi bora kitaifa kutoka shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera
  • Awakumbusha wajibu wa kusoma kwa bidii, kuachana na starehe ili kuongeza ufaulu na kufika katika kilelele cha ndoto zao.
  • Licha ya umasikini na kukosa ada ya shule, aliweka juhudi binafsi kujisome na kufanya kazi ndogo ndogo kutimiza malengo yake. 

Dar es Salaam. Ni siku ya mwisho ya mwezi Januari, ulikuwa na mengi ambayo yameleta furaha na majonzi kwa baadhi ya watu hasa wanafunzi, baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2018.

Januari 24, 2019, Necta ilitangaza matokeo hayo huku yakionyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 78.38 kutoka asilimia 77 mwaka 2017 licha ya changamoto za udangajifu na matokeo yasiyoridhisha ya masomo ya sayansi.

Matokeo hayo yameziacha shule na wanafunzi wanaoendelea na masomo katika tafakari ya namna ya kufanya vizuri katika masomo yao. Lakini wakipata hamasa ya watu waliofanikiwa wanaweza kupata nguvu ya kufanya vizuri katika mitihani ijayo ili kutimiza ndoto zao.

Nukta inakuleta mahojiano iliyofanya na mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 1990, Mgaywa Magafu ambaye alihitimu katika shule ya sekondari ya Ihungo ya mkoani Kagera ambapo alipata daraja la I la alama saba yaani A katika masomo yote nane. 

Magafu ambaye kitaaluma ni daktari wa magonjwa ya mlipuko amefanya kazi na mashirika mbalimbali duniani likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kuhakikisha binadamu wanakuwa na afya njema wakati wote. 

Daktari huyo ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma katika mazingira magumu nchini lakini alifanya kila linalowezekana kufikia malengo ya maisha yake, jambo linaloacha somo kwa wanafunzi waliopo shuleni.

“Elimu yangu imeniondolea mipaka katika akili yangu. Nimeishi na kufanya kazi Tanzania, Trinidad na Tobago, Botswana, Cambodia, Ghana, Liberia, Malawi, Nigeria na Ethiopia. Ni elimu na ubunifu wangu ndivyo vinavyoniwezesha kukubalika nchi zote hizi,” amesema Dk Magafu.


Zinazohusiana: 


Mahojiano haya yanaweza kuwa chachu kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo kupata hamasa ya kufufua matumaini ya kufanikiwa kielimu,  Fuatana nami katika mahojiano haya:

Nukta: Tueleza historia ya elimu tangu shule ya msingi hadi ulipohitimu masomo yako na kupata mafanikio ya taaluma uliyonayo sasa.

Dk Magafu: Nilianza elimu ya msingi mwaka 1980 katika shule ya msingi Rwamkoma wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara lakini nikamalizia elimu hiyo katika shule ya msingi Namalebe wilayani Bunda katika mkoa huo huo mwaka 1986. 

Masomo yangu ya sekondari ya awali niliyapata katika shule ya Ihungo iliyoko Bukoba toka 1987 hadi 1990. Baada ya Ihungo, nikwenda Shule ya Sekondari Ilboru Arusha kwa ajili ya masomo ya sekondari ya juu katika mchepuo wa fizikia, kemia na bailojia. 

Mwaka 1995 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sayansi ya Afya Muhimbili kwa ajili ya masomo ya udaktari na kumaliza mwaka 2000. Baadaye nikaendelea na masomo ya juu na kupata shahada mbalimbali za uzamili (Master degrees). 

Nilipata shahada ya uzamili ya afya ya jamii (magonjwa ya mlipuko na takwimu za afya) kutoka Chuo Kikuu Chuo cha Brussels (ULB) kilichopo Ubelgiji na shahada ya uzamili ya afya ya jamii (uongozi katika sekta ya afya) kutoka Kikuu Chuo cha Western Cape (UWC) Afrika Kusini.

Pia shahada ya uzamili katika mambo ya utafiti wa madawa na chanjo kutoka Chuo Kikuu cha Siena cha nchini Italia. Na mwisho nikapata shahada ya uzamivu (PhD) katika magonjwa ya mlipuko kutoka Kikuu Chuo Kikuu cha Nagasaki, Japan.

Dk Mgaywa Magafu akiongoza mafunzo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) jijini Lagos Nigeria Novemba 2018. Picha| Dk Mgaywa Magafu.

Nukta: Wakati huo unapata taarifa za kuwa umekuwa mwanafunzi bora kitaifa ulijisikiaje? Kuwa mwanafunzi bora kwa miaka ya 1990 ilikuwa ina tafsiri ipi kwa jamii?

Dk Magafu: Nilijisikia vizuri sana japo sikutegemea. Nilijua wanafunzi bora wote wangetoka Dar es salaam na Pwani kwa sababu kulikuwa na habari za wizi wa mitihani katika mikoa hiyo mwaka 1990 ambao nilifanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Wakati huo kule kijijini kwetu, familia zenye watoto sekondari zilikuwa zinahesabika. Achilia mbali kuwa mwanafunzi bora, kuwa na sekondari halikuwa jambo la kawaida. Hili la kufanya vema kitaifa lilikuwa jambo la furaha kubwa. 

Jambo ili lilinitambulisha kwa jamii hususani jamii ya wanafunzi wenzangu. Lilinifanya nijulikane sana. Watu wengi walinijua japo mimi sikuwajua. Ilikuwa sawa na kumjua msanii wa maigizo kupitia runinga wakati yeye hakujui. Lakini pia niseme kuwa, tofauti na sasa hivi, sisi tulikuwa hatuandikwi katika magazeti ama kutangazwa katika vyombo vingine vya habari.

Nukta: Umesema wakati huo shule za sekondari zilikuwa chache. Tuambie ulikumbana na changamoto gani ambazo zilikuwa kikwazo kufikia ndoto zako lakini ulizishinda. Unafikiri zinawakumba wanafunzi wa wakati huu ambao nao wana ndoto za kufika mbali kimasomo?

Dk Magafu: Changamoto kubwa ilikuwa ni umasikini. Nimetoka katika familia masikini. Wazazi wangu wote walikuwa wakulima. Haikuwa rahisi kupata karo na pesa ya matumizi mengine ya shule hasa nilipokuwa sekondari. Mathalani sikuweza kulipa karo yote ya sekondari mpaka namaliza elimu hiyo. 

Baada ya kumaliza shule, nilipata kazi za vibarua na kupata pesa ndipo nilipokwenda kulipa karo iliyokuwa imebaki na kupewa cheti changu. Wakati huo tuliruhusiwa kufanya mithani ya mwisho hata kama karo ilikuwa haijakamilishwa. Kwa upande wa chuo kikuu, sikuwa na changamoto hii kwa vile nilibahatika kupata udhamini.

Changamoto nyingine zilikuwa ndogo ndogo kama vile mazingira magumu katika shule zetu za sekondari ikiwemo kidato cha kwanza kuonewa sana, shule kutokuwa na maji ya bomba, kukosa umeme wa uhakika, kula chakula cha aina moja kwa mhula mzima, kutokuwa na vitabu na walimu wa kutosha. 

Dk Mgaywa Magafu akiwa na mke wake pamoja na watoto wake mwaka 2014. Picha|Dk Mgaywa Magafu.

Nukta: Uliwezaje kupenya katika mazingira magumu kama hayo?  au ni juhudi binafsi ulizokuwanazo?  

Dk Magafu: Kama nilivyosema hapo awali, mazingira ya shule nyingi za msingi na sekondari Tanzania hayakuwa mazuri. Asubuhi wakati wa kwenda shule tulibeba miti, mfagio, makete, jembe, vidumu vya maji, nk. Fikiria mtoto wa miaka 7 hadi 12 kubebeshwa mizigo kama hii kila siku. 

Rwamkoma shule ya msingi nilikoanzia ndiyo iliyokuwa kinara wa mambo haya. Walimu walikubaliana na wanakijiji ili twende katika mashamba ya wanakijiji kuwalimia kwa ujira ambao uliwafaidisha walimu. Ilifika wakati tukawa tunaonana kwenye mashamba kuanzia saa moja asubuhi. 

Maana yake ni kwamba tulitumia muda wa masomo huko mashambani. Sekondari nazo hazikuwa tofauti sana. Pamoja na mazingira haya magumu, ni lazima niseme kuwa kulikuwa na walimu waliokuwa wamejitoa sana, walitimiza wajibu wao barabara na waliipenda kazi yao. 

Niseme pia kwamba japo nilitoka kwenye familia ya wakulima, nilichukia sana kulima. Nyumbani nilijulikana kama “mvivu” katika kilimo. Kwa hiyo ilinilazimu nitafute mbadala wa kulima. Hakukuwa na njia nyingine ila kusoma kwa bidii.

Kwa hiyo mafanikio yangu ya kielimu yametokana na walimu wa aina hii, wazazi wangu na juhudi zangu kama mwanafunzi mwenye nia ya kufanikiwa. Namshukuru Mungu pia kwa mafanikio yote niliyowahi kupata maishani mwangu. Bila yeye nisingeweza.


"Nakumbuka siku moja niko darasa la 5 mwalimu wa hesabu alituambia kuwa shule yetu ilikuwa kongwe sana lakini ilikuwa na mwanafunzi mmoja tu aliyepata kufika chuo kikuu. Nilimwambia kuwa asipojitokeza mwingine basi mimi nitakuwa wa pili. Nia hiyo niliitimiza nilipokwenda chuo kikuu mwaka 1995." - Dk Mgaywa Magafu.



Nukta: Kuna walimu au watu ambao walikuvutia kuwa katika nafasi uliyonayo na kwa namna gani walijenga matumaini ya kufikia hapo ulipo?

Dk Magafu: Naam! Katika maisha kuna watu ambao kila mtu huwaangalia kama mfano mzuri ama mbaya. Kwa mtu mwenye kutafuta mafanikio, hutamani kuwa kama walivyo wale anaowaona kama mfano wa kuigwa. 

Mwaka 1982 nikiwa katika Shule ya Msingi Mugara wilayani Bunda, nilionana na Mwalimu Mkuu Nyakerega Eliakim Wambura (kwa sasa ni marehemu). Mwalimu huyu alijua mambo mengi sana na alipenda sana sisi pia tujue mambo mengi. Alijitahidi kiasi chake kutufanya wanafunzi wake tuelewe masomo. 

Huyu mwalimu alijenga msingi wa elimu yangu ya msingi na alisaidia sana kunifanya niendelee na masomo ya sekondari. Sekondari pia kulikuwa na baadhi ya walimu waliojitoa sana na kufanya masomo waliyokuwa wanafundisha yaonekane marahisi.

Mathalani, mwalimu Hella aliyenifundisha kemia kidato cha tano shule ya sekondari Kibaha kabla sijahamia Ilboru. Niseme ukweli kuwa walimu wangu wa chuo kikuu hawakuwa kivutio kwangu. Waliishi maisha magumu sana kwa sababu ya mishahara midogo iliyokuwa inalipwa wakati huo. Baadhi yao walitumia muda mwingi kulalamika kuhusu maisha magumu hata walipokuwa darasani wakifundisha.

La tatu, ni nguvu niliyoipata kutoka kwa maneno ya baba yangu mzazi wakati wa uhai wake. Wakati akiwa kijana alikuwa akitumia pombe. Alipokuwa kilewa alipenda sana kujitapa kuhusu mimi japo nilikuwa hata sijaanza shule. 

Alipenda sana kuwaambia wanakijiji wenzie kuwa mtoto wake (yaani mimi) atasoma hadi Ulaya. Miaka mingi baada ya baba kufariki, nilijisikia nawiwa kutimiza huu unabii wa baba yangu. Namshukuru Mungu kuwa mwaka 2008 na 2011 niliutimiza kwa kupata shahada za uzamili nchini Ubelgiji na Italia.

Mbali na shughuli za kitaaluma, Dk Magafu hupenda kujumuika na jamii ikiwemo kutembelea vivutio vya utalii.  Picha|Dk Mgaywa Magafu.

Nukta: Unafikiri nini kifanyike kuwavutia wanafunzi wengi kusoma masomo ya sayansi kama wewe ulivyopenda masomo hayo na ukafika hapo ulipo sasa?

Dk Magafu: Masomo ya sayansi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hususani kipindi hiki ambacho lengo ni kujenga Tanzania ya viwanda. Ili mtu akipende kitu, ni muhimu akakutanishwa nacho mapema katika maisha yake. Sayansi ianze kufundishwa katika madarasa ya awali. 

Na vipaji vya sayansi vitambuliwe na kuendelezwa tangu hatua hizi za awali. Watoto watayapenda masomo ya sayansi iwapo walimu wao watayafanya yaeleweke. Ili yaeleweke, inabidi tuwe na walimu wa sayansi waliobobea na wapewe vitendea kazi vya kutosha kama maabara na vifaa vyake. 

Walimu walipwe vizuri ili wapende kazi yao. Na wanafunzi nao wanaweza kupewa motisha mbalimbali. Mathalani, wanafunzi wa udaktari kuhakikishiwa na Serikali mkopo kwa ajili ya masomo yao ya elimu ya juu.  

Nukta: Mafanikio hayo uliyoyapata wakati ukiwa sekondari kwa namna gani yalikusaidia kufikia ndoto za maisha yako? Kwa mtazamo wako elimu uliyoipata imekusaidia kutafsiri uwezo na ubunifu katika kutekeleza majukumu ya kikazi na maisha ya kawaida?

Dk Magafu: Elimu ya sekondari ni kiungo kuelekea elimu ya juu. Kwa hiyo kufaulu vizuri sekondari kuliniwezesha kuendelea hadi chuo kikuu na kutimiza ndoto zangu za kupata elimu ya juu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ya kweli ni yenye kumsaidia mwenye nayo kutawala mazingira yake. Elimu yangu imeniwezesha kutawala mazingira yangu. 

Elimu hii imeniwezesha kuiona sayari hii kuwa ni moja na watu wake ni wamoja. Mipaka imewekwa na wanadamu tu. Mungu aliumba sayari ya dunia moja. Elimu yangu imeniondolea mipaka katika akili yangu. Nimeishi na kufanya kazi Tanzania, Trinidad na Tobago, Botswana, Cambodia, Ghana, Liberia, Malawi, Nigeria na Ethiopia. Ni elimu na ubunifu wangu ndivyo vinavyoniwezesha kukubalika nchi zote hizi.

Nukta: Mbali na taaluma uliyonayo ni mambo gani mengine ya kijamii unayofanya ambayo yanachangia kukamilisha furaha ya maisha yako?

Dk Magafu: Mimi ni Mkristo. Napenda kukusanyika na kuabudu na jamii ya Wakristo wenzangu. Pia napenda sana kusaidia watoto wenye uwezo kimasomo lakini kwa sababu moja ama nyingine, wanakosa uwezo kifedha. 

Kwa bahati mbaya watoto wenye mahitaji haya ni wengi sana kiasi kwamba mtu mmoja hawezi kuwatimizia mahitaji yao wote. Nipatapo muda, hupenda kusafiri na familia. Waswahili tunasema, tembea ujionee.

Nukta: Wanafunzi na vijana wajifunze nini kutoka kwako ambao wana ndoto na wanatamani kufika kwenye kilele cha mafanikio yao kama wewe ulivyopambana licha ya mazingira magumu uliyokulia?

Dk Magafu: Kitu cha kwanza ni nia. Wawe na nia ya kufika mbali. Penye nia pana njia. Cha pili ni kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao. Tatizo la wanafunzi wengi ni kuchanganya masomo na mapenzi. Wanafunzi wanaofanikiwa ni wale wanaomaliza masomo kwanza na kuingia katika mapenzi baadae. 

Katika kazi yoyote unayoifanya, anza kwanza na mambo muhimu. Uwezo wa kuahirisha ama kupuuzia starehe katika maisha ya awali kama vile shuleni ni hatua ya mwanzo ya kutumia muda vizuri.

Related Post