Kabla ya kuingia katika biashara ya ushirika, zingatia haya

June 20, 2020 8:00 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Fahamu sheria zinazosimamia aina hiyo biashara.
  • Malengo na muda mtakaotumia katika ushirika huo.
  • Muhimu ni kuweka mikakati itakayowezesha kupata faida na siyo hasara. 

Biashara hufanyika kwa namna mbalimbali kutoka zile zinazoendeshwa na mtu mmoja hadi zile za ushirika na kampuni. 

Leo tunaangazia biashara inayofanyika kwa mtindo wa ushirika (Partnership) na mambo ya kisheria ya kuzingatia ili ifanikiwe. 

Partnership ni muungano wa kisheria wa watu wawili au watatu kwa lengo la kufanya biashara. Watu hawa watakua wameungana kwa lengo lakufanya biashara halali kwa lengo la kupata faida. 

Ni ushirika ambao umekaa kibiashara zaidi na sio kisiasa. Sheria za mikataba za Tanzania ndiyo msingi mkubwa wa suala la partnership. Uendeshaji wa partnership unasimamiwa na sheria za mikataba.

Kuzaliwa kwa ushirika huo
Ujio wa ushirika unaletwa kwa mkataba utakaosainiwa baina ya washirika wote. Uwepo wa ushirika unachagizwa na nyaraka inyotambulika kama Partnership Deed (PD) 

PD kimsingi ndIo cheti cha kuzaliwa cha ushirika ambacho kitatoa makubaliano yaliyofikiwa, wajibu na haki za kila mdau. Kisheria partnership ina ukomo wa wanachama wanaotakiwa kisheria ambao hawatakiwi kuzidi 20. 

PD  ili iwe halali mbele ya macho ya sheria inatakiwa kukidhi vigezo vyote vya kisheria vilivyowekwa na sheria ya mikataba na ikatokea imeshindwa kukidhi basi PE itakua batili mbele ya sheria na haitakubalika kwenye macho ya sheria.


 Soma zaidi: 


Aina za ushirika

Ushirika umegawanyika katika aina mbalimbali kutokana na mahitaji ya wadau wa ushirika huo.


1. Kwa lengo maalum
Ushirika huu unakua umeanzishwa kwa ajili ya shughuli fulani ya kibiashara tu. 

Wanachama wanakua wameweka lengo maaulum kwa ajili ya ushirika wao na lengo hilo linakua kufanya biashara fulani yenye faida.

Lengo lao ndiyo linakua msingi mkubwa wa ushirika wao. Kwa mfano Partnership kwa ajili ya kampuni ya usafarishaji, kwa hiyo lengo litakua kuanzisha ushirika wenye kushughulika na usafirishaji. 


2. Muda maalum
Ushirika huu unaweza kuwa na lengo lolote kwa uanzishwaji wake lakini  inaanzishwa kufanya kazi kwa muda maalumu tu. Mfano washirika hawa wataamua kuwa ushirika wao uwe wa miaka miwili tu.

Hii inamanisha kuwa baada ya miaka miwili hiyo tangu kuanzishwa kwake ushirika wao utakua umefika mwisho.


3. Usio na lengo wala muda
Ni aina ya ushirika ambao unaanzishwa pasi na kuwa na lengo maalumu wala  muda maalumu. 

Hii ina maana kuwa ukomo wake ni matakwa ya washirika hao kuamua lini iwe mwisho wa ushirika wao na pia malengo ya ushirika wao hayako bayana hivyo basi wanaweza kufanya bishara yoyote ile  halali kwa mujbu wa mkataba wao yaani PD. 

Wanachama wake wakisema leo tunahitimisha maisha yake basi itakua hivyo.

Biashara ya ushirika hutegemea zaidi utashi na uelewa wa sheria zinazosimamia ili kuepuka hasara mbeleni. Picha|Whelehan Solicitor. 

Jinsi ya kujitoa katika ushirika

Suala la kuondoka kwa mshirika kwenye ushirika  linaruhusiwa kisheria bila shida yoyote. Uondokaji kwa kiasi kikubwa unategemea ni aina ya mkataba walioingia wahusika.

PD itatoa namna ya mtu anavyotakiwa kufanya kabla ya kuondoka kwenye ushirika. Lakini kitu cha muhimu ikiwa mmoja anataka kuondoka basi atapaswa kutoa notisi kwa wenzake kuwa anataka kuondoka na pia atalazimika kuchapisha kwenye gazeti.

Maana ya hii notisi ni kuwajulisha wenzake na umma kuwa yeye sio mwanachama tena na hatowajibika kwa shughuli zozote za ushirika.


Kushitaki na kushitakiwa
Washirika au wadau wa ushirika kila mmoja anaweza kushitakiwa au kushitaki kwa jina lake halisi. Ushirika wao siyo kiumbe hai mbele ya uso wa sheria hivyo basi yenyewe haina uwezo wa kushitaki wala kushitakiwa kama ilivyo kwa kampuni.

Kila mmoja atashitaki na kuhsitakiwa kwa jina lake na siyo jina la partnership. Kivuli cha ushirika hakitatumika kumkinga mtu dhidi ya kesi ya madai au jinai.

Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo tutaendelea kuangazia kwa undani biashara ya ushirika (partnership).

Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule, Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini. Kwa msaada wa kisheria wasiliana naye kupitia Twiter: @Hamzaalbhanj  Simu; 0717521700

Enable Notifications OK No thanks