Hifadhi ya Katavi; mahali unapoweza kushuhudia mapigano ya viboko na mamba

September 3, 2018 6:29 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Asili yake imetokana na mwindaji maarufu wa kienyeji aliyeishi katika maeneo hayo ya hifadhi akijulikana kama “KATABI”
  • Kivutio kikubwa cha hifadhi hiyo ni mapigano ya makundi ya  viboko na  mamba kwenye Ziwa Katavi.
  • Inafikika mwaka mzima kwa kutumia magari ya kukodi, treni na ndege.

Dar es Salaam. Unapozitaja au kuzungumzia hifadhi za taifa Tanzania, basi hutaacha kuitaja Ruaha na Serengeti kutokana na umaarufu wake wa kutembelewa na watalii wengi kutoka nje ya nchi. 

Umewahi kuisikia Hifadhi ya Taifa ya Katavi? Hii ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini baada ya Ruaha na Serengeti ambapo imesheheni vivutio vingi ambavyo huwezi kuvikuta katika maeneo mengine duniani. 

Ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,471 na inapatikana katika wilaya ya Mpanda mkoa wa Katavi ambapo ni miongoni mwa hifadhi tano zinazopatikana  Kusini  Magharibi  mwa  Tanzania   karibu na  Ziwa  Tanganyika .

Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Katavi ilitangazwa  kuwa  Hifadhi ya  Taifa   mwaka 1974 ikiwa  na  ukubwa  wa  kilometa za   mraba  2,253 na ilipofika   1996 iliongezwa eneo na kufikia kilometa za  mraba  4,471.  

Jina la hifadhi hiyo limetokana na jina la asili la mwindaji maarufu wa kienyeji aliyeishi katika maeneo hayo ya hifadhi akijulikana kama “KATABI”. Pia watu wanaamini Katabi ni mzimu maarufu wa kabila la Wabende ambapo mpaka leo watu wanafika katika eneo hilo  na kuelekea kwenye mti ulipo Ziwa Katavi wakiamini mzimu huo ulikuwa unaishi hapo kabla ya hifadhi.

Inaaminika mzimu wa Katabi    una uwezo  wa  kufanya miujiza mbalimbali kama kunyesha kwa mvua, kutatua shida na changemoto mbalimbali hata kuzuia magonjwa ya mlipuko  kama ndui.

Kiboko akiwa na mambo, ni kivutio kikubwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Picha| Jamii moja

Kufika kwako katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi kutakupa fursa ya kujionea wanyama pori wengi yakiwemo makundi  makubwa ya tembo , nyati,  simba ,  pundamilia ,  mbwa  mwitu , kongoni, swala  pala na nyemela.

Huku eneo la mto  Stalike  na   Iku  ikiwa ni kivutio kikubwa cha utalii kutokana na mapigano ya makundi ya  viboko na  mamba. Pia utakutana na idadi kubwa ya vipepeo  na  ndege  wa   aina  mbalimbali.

Achilia mbali uwepo wa wanyama kuna mandhari  pana  ya uwanda  tambarare wa  nyasi  katika  mkondo  wa  bonde  la ufa la Rukwa. Uoto huo wa asili unakupatia aina 226 za miti na mito na vijito zikiingia na kutoka katika eneo la hifadhi.

Hifadhi hii  inafikika  mwaka mzima  kwa kupitia  Mikoa ya  Dar es Salaam, Mwanza , Kigoma   Arusha hadi  Mpanda  kupitia  Tabora kwa kutumia  usafiri wa  ndege  za kukodi “Chartered Planes”  au kwa njia ya  barabara kupitia  mkoa wa Mbeya   na Rukwa. 

Kwa wanaopendelea usafiri wa treni wanaweza kufika kutoka popote walipo ikiwa watapanda treni katika mji wa Tabora .


Vitu ambavyo mtalii anawezafanya kwenye hifadhi.

Mtalii akiwa hifadhi hiyo  anaweza kutazama wanyama kwa kutumia gari hasa nyakati za asubuhi ambapo wanyama wanakuwa wamepumzika. Pia matembezi mafupi yanayojulikana kama “Sitalike walking Trail” kuanzia kilomita moja hadi  hadi tisa.

Kwa wanaopenda kutembea basi yapo matembezi marefu (Chorangwa Hiking Trail) ya  kilomita 10 na kuendelea ambapo mtalii ana uwezo kutembea kwa saa 10.

Pia ndani ya hifadhi ya Katavi, mtalii anaweza kufanya utalii wakati wa usiku  kumuwezesha kuona wanyama ambao mchana hawaonekani kirahisi akiwa kwenye gari la wazi na lenye taa maalumu.

Kuweka kambi ndani ya hifadhi hiyo nayo ni huduma nyingine ambayo hutaikosa ukiwa kwenye hifadhi ya Katavi. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW