Maoni mchanganyiko Tanzania kukopa fedha utekelezaji miradi ya maendeleo
- Baadhi waunga mkono wasema itawatua mzigo wananchi.
- Wengine waweka tahadhari kukua kwa deni la Serikali.
- Wasomi washauri uwazi na uwajibikaji matumizi fedha za mikopo.
Mwanza/Dar es Salaam. Watu mbalimbali wakiwemo wasomi na wananchi wa kawaida wameendelea kutoa maoni yao kuhusu Serikali ya Tanzania kuendelea kukopa mikopo kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo huku baadhi wakisema hatua hiyo ni nzuri ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa kugharamia huduma za kijamii.
Rais Samia Suluhu Hassan jana Desemba 28, 2021 alisema itaendelea na miradi yake ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Dar es Salaan na bwawa la Nyerere katika mto Rufiji ili kukamilisha na kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.
Kukamilisha miradi hiyo, Rais Samia aliyekuwa akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora Ikulu Jijini Dar es Salaam amesema Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye masharti nafuu ili kufikia malengo yake.
“Tutaendelea na ujenzi wa miradi, kuna jitihada za kutuvunja moyo katika mikopo, hata hizo nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuzidi ya kwetu…,tutakopa tumalize miradi ya maendeleo,” alisema Rais Samia.
Hata hivyo kauli hiyo ya Rais imepokea kwa hisia tofauti na wananchi, viongozi na wasomi nchini huku wengine wakisema ni jambo jema na wengine wakionya kuwa mikopo inaiweka nchi rehani.
Siku moja kabla ya Rais kutoa kauli yake ya kukopa, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alionya kuwa deni la Serikali limefika Sh70 trilioni na kuna siku “nchi itapigwa mnada”.
“Juzi mama ameenda kukopa Sh1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika Ndugai Desemba 28 katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma.
“Tutembeze bakuli ndio heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku,’ amesema Ndugai akibainisha kuwa “tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.
Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) kwenye bonde la mto Rufiji unaendelea kama kawaida. Picha| Mpekuzi.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Nuhu Emmanuel amesema suala la kukopa linahitaji umakini ili kuepuka mtego wa kujenga miradi ambayo inaweza isifanikishe kurejeshwa wa mikopo hiyo na baadaye kuiweka nchi katika wakati mgumu.
“Tujitegemee sisi wenyewe, mikopo inaleta utumwa. Tutumie vizuri rasilimali zetu kufanya maendeleo,” amesema Emmanuel.
Wakati baadhi wakitofautiana na mtazamo wa kukopa, wengine wanaona suala hilo halina shida ilimradi mikopo haitumbukizi nchi katika madeni yasiyolipika.
“Ni sawa itawatua mzigo wananchi”
Baadhi ya wakazi jijini Mwanza wamesema kauli ya Rais iko sahihi kwa kuwa itapunguza mzigo mkubwa wa mwananchi kubebeshwa kodi kubwa ili kukamilisha miradi ya maendeleo.
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa) Mkoa wa Mwanza, Anwar Said amesema kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa ikiwemo ya SGR na ujenzi wa meli haziwezi kuendeshwa kupitia fedha za walipa kodi pekee.
“Ni lazima Serikali iangalie namna ambapo itapata mikopo yenye riba nafuu ili iweze kukopa kukamilisha miradi hiyo kisha deni hilo lilipwe kidogo kidogo kupitia fedha za walipa kodi,” amesema Said.
Amesema wananchi wanatakiwa kutofatisha kauli za kisiasa na maendeleo iwapo watafuata kauli za kisiasa zitasababisha wananchi hususani wa kawaida kuumia.
“Kwa mantiki hiyo utakuta mwenye saluni ya kunyoa anapewa kodi ya mtu anayemiliki duka kubwa, mambo yataenda ndivyo sivyo na bidhaa za ndani zinaweza kupanda mara dufu ya hivi ilivyo sasa,” amesema Said.
Soma zaidi:
-
RC Mwanza aagiza haki itendeke ulipaji fidia ujenzi reli ya kisasa
-
Wizi wa mafuta reli ya kisasa wamkera waziri
-
Rais Sami: Reli ya kisasa itajengwa kwa mkopo
Mkazi mwingine wa jiji la Mwanza, Thomas Tukay amesema siyo Tanzania pekee inayokopa lakini jambo muhimu ni kukopa katika taasisi zinazotoa mikopo yenye riba nafuu.
Amesema zipo nchi ambazo zina madeni makubwa kama Japan, China na nyingine na kwamba miradi mikubwa inayotekelezwa katika nchi zao haitegemei kodi moja kwa moja.
“Ushauri wangu ni kuwa fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na pia tozo ziongezwe ili kuweza kulipa madeni haya ambayo Serikali inakopa kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza kama kutaifishwa kwa rasilimali muhimu,” amesema Tukay.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitembea kwenye mfano wa reli ya Kisasa itakayojengwa kutoka Mwanza hadi Isaka mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza leo tarehe 14 Juni, 2021. Rais amesema Serikali itaendelea kukopa kutekeleza miradi ya maendeleo. Picha| Michuzi.
Wasomi wanena
Edwini Soko, mwanasheria mkazi wa jijini hapa amesema kunapotokea mivutano ya kauli kutoka kwa viongozi wa Serikali kunaibua hisia na mijadala kwa wananchi kuwa huenda yapo mambo ambayo hayaendi sawa kutokana na fedha zinazokopwa.
Amesema ni halali ya watu kujadili na kwamba hiyo ni hatua ya kuikumbusha Serikali kuwa na umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na kile kinachofanyika.
Amesema ni vema mihimili yote ikiwemo Serikali na Bunge ikae na isikilizane ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi kuhusu mikopo kwa kuwa lengo la mihimili hiyo ni kujenga Tanzania.
“Wasipofanya hivyo wanaoumia ni wananchi wa kawaida ambao wataendelea kupandishiwa tozo na bei za vitu kupanda,” amesema Soko.
Kauli ya Soko haitofautiani na ya James Nungwana ambaye amesema kuna haja ya kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia matumizi ya fedha za mikopo na kukopa pale inapohitajika.
Amesema Bunge linapaswa kufanya kazi yake kuishauri Serikali katika mambo muhimu kwa sababu wabunge wanawakilisha wananchi kuhusu mambo yao ya kujiletea maendeleo.
Habari hii imeandikwa na waandishi: Daniel Samson na Mariam John.