Rais Tshisekedi ahitimisha ziara ya siku mbili Tanzania

October 24, 2022 12:21 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan akimsindikiza mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilisha ziara nchini Tanzania Oktoba 24, 2022. Picha | IKulu.


  • Akiwa nchini ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano utakao imarisha ushirikiano wa masuala ya Teknolojia.
  • Hii ni ziara ya kwanza ya Rais huyo nchini Tanzania tangu Rais Samia alipoingia madarakani.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Félix Tshisekedi amehitmisha ziara yake ya siku mbili nchini Tanzania iliyolenga   kukuza ushirikiano na uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Tshisekedi aliwasili jana Oktoba 23, 2022 ambapo alishuhudia utiaji  saini wa hati ya makubaliano (MoU) baina nchi hizo mbili  ikilenga kuimarisha  ushirikiano katika masuala ya teknolojia (ICT), posta na mawasiliano.

Utiaji saini  wa mkataba huo unaohusu teknolojia umefanywa na  Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Nape Nnauye, pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya nje wa DRC Christophe Lutundula, IIkulu jijini Dar es Salaam.

“Tanzania na DRC zimekubaliana kushirikiana kuendeleza sekta ya teknolojia na mawasiliano kwa kuwa ni sekta pekee inayozalisha rasilimali pamoja na ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa,” amesema Rais Samia aliyekuwa akihutubia kwenye hafla ya utiaji saini huo.

Mbali na utiaji saini viongozi hao wamejadili mambo mbalimbali yenye tija kwa nchi zote mbili.


Soma zaidi:


Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini huo Rais Tshisekedi amesema wamejadili  suala la mawasiliano kwa nchi zote mbili na kuona ni suala la msingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao.

“Ni suala muhimu sana kuendeeleza sekta hii ya mawasiliano kwa ajili ya nchi zetu mbili. sekta hii si kama tu inazalisha rasilimali  ni sekta ambayo inazalisha ajira nyingi kwa vijana wetu,” amesema Rais Tshisekedi. 

Upande wa kimataifa marais hao wamejadili vita vya Ukraine na Urusi inayoathiri bara la Afrika hasa sekta ya chakula na nishati na jinsi wanavyoweza kutatua.

Suala lingine lilipata kipaumbele cha kujadiliwa na viongozi hao ni msimamo wa Afrika juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi, athari zake na namna ya kukabiliana nazo.

“Na sisi nchi za Afrika tunatakiwa kufanya kama wenzetu walivyofanya tutumie rasilimali tulizonazo kama petroli na kadhalika ili kufikia maendeleo,” ameongeza Rais huyo wa DRC.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais huyo nchini Tanzania tangu Rais Samia alipoingia madarakani.

Ziara ya mwisho ya Rais huyo nchini Tanzania ilikuwa Juni 2019 ambapo alipokelewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Magufuli.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa  ni kuimarisha na kukuza zaidi undugu, urafiki na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na DRC.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW