Rais Mwinyi: Hayati Mkapa ni mfano wa kuigwa kizazi cha sasa na kijacho
- Asema Mkapa ndiye aliyeasisi Dira ya Maendeleo ya 2025.
- Ahimiza Watanzania kuendeleza urithi wa Mkapa kwa kudumisha mshikamano na utulivu wa kitaifa.
Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Hayati Benjamin Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa.
Dk Mwinyi amesema Serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Mkapa ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani na mshikamano wa Watanzania, pamoja na nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni.
Akizungumza katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya miaka mitano tangu kufariki kwa Hayati Mkapa, iliyofanyika Julai 23, 2025 katika kijiji cha Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara, Dk. Mwinyi amesema Hayati Mkapa aliamini katika ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi huku akihakikisha maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.

“Hayati Mkapa ndiye aliyeasisi Dira ya Maendeleo ya 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu cha mageuzi ya maendeleo. Mafanikio ya dira hiyo sasa yamekuwa msingi wa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050,” amesema Rais Mwinyi.
Mbali na mchango wake wa kitaifa, Rais Mwinyi ameeleza kuwa Hayati Mkapa alikuwa mtetezi wa maslahi ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa na sauti ya amani katika mizozo mbalimbali barani, ikiwemo Sudan Kusini, Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hata hivyo, Rais Mwinyi amehimiza Watanzania kuendeleza urithi wa Mkapa kwa kudumisha mshikamano na utulivu wa kitaifa, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha, amewataka viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa mstari wa mbele katika kulinda tunu ya amani kama sehemu ya kumuenzi Mkapa.
“Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo ambao wanaendeleza maono ya viongozi waasisi na kuipeleka Tanzania mbele katika nyanja zote za maendeleo,” ameongeza Rais Mwinyi.

Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi akiwa na miaka 81 na ikiwa ni mwaka mmoja tu umepita tangu alipozindua kitabu cha maisha yake binafsi kinachoitwa ‘My life, My purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu).
Katika kuhitimisha maadhimisho hayo, Rais Mwinyi amezuru kaburi la Hayati Mkapa na kuweka shada la maua, akiambatana na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Filipe Nyusi na mkewe, pamoja na mjane wa Mkapa, Mama Anna Mkapa.
Latest