Polisi: Tunachunguza tuhuma za kuchukuliwa, kurejeshwa dada wa Polepole

July 18, 2025 2:40 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Jalada la uchunguzi tayari limefunguliwa kufuatia maelezo yaliyotolewa na Christina katika kituo cha polisi.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la kuchukuliwa na kurudishwa na watu wasiojulikana dada wa Humphrey Polepole katika eneo la Bahari Beach, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliyekuwa akizungumza na wanahabari amesema mwanamke aliyetambulika kama Christina Hezron Polepole Kinyangazi (52) ambaye ni dada wa aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole, ameripotiwa kujitokeza Julai 18, 2025 katika Kituo cha Polisi Kawe.

Kwa mujibu wa Muliro, Christina emesema alichukuliwa na watu wasiojulikana, lakini alirudishwa nyumbani usiku huohuo.

Taarifa za tukio hilo zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii baada ya Humphrey Polepole kupakia video kwenye ukurasa wake wa Instagram akieleza kuwa dada yake alichukuliwa na watu waliovamia nyumbani kwake saa tano usiku baada ya kuruka ukuta na kumchukua bila kujitambulisha.

“Simu yake haijapatikana. Watu walioshuhudia wamesema kulikuwa na magari aina ya Land Cruiser na Noah eneo la tukio,” alisema Polepole katika video hiyo.

Hata hivyo, Kamanda Muliro amesema, jalada la uchunguzi tayari limefunguliwa kufuatia maelezo yaliyotolewa na Christina katika kituo cha polisi.

Tukio hili linajitokeza katika kipindi ambacho kumekuwa na ongezeko la matukio ya watu kuripotiwa kuchukuliwa au kupotea kwa mazingira ya kutatanisha, hali inayozua maswali kuhusu usalama wa raia na wajibu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Wadau wa haki za binadamu wamekuwa wakitaka uchunguzi huru na wa kina kufanyika kila mara panaporipotiwa matukio kama haya, huku wakisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria.

Juni 27, mwaka huu wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya kuvunja Bunge la 12 la Tanzania aliliagiza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks