Njombe kinara maambukizi ya VVU Tanzania

Dar es Salaam. Mkoa wa Njombe umeendelea kushika nafasi ya kwanza nchini Tanzania kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), huku takwimu zikionyesha ongezeko la maambukizi katika mkoa huo ndani ya miaka nane.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania (THIS) inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)mwaka 2016–2017 maambukizi ya VVU Njombe yalifikia asilimia 11.4.
Kasi ya maambukizi katika mkoa huo iliongezeka kwa asilimia 1.3 katika ripoti ya THIS ya 2022–2023 na kufikia asilimia 12.7 hali inayoashiria changamoto endelevu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kati ya idadi hiyo wanawake wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni asilimia 16, mara mbili zaidi ya idadi ya wanaume iliyofika asilimia 8.6 .
Pamoja na idadi hiyo, watu wanaoishi na maambukizi na kutambua hali zao wanawake ni asilimia 92.9, wanaume asilimia 92.0 ikiwa ni chini ya lengo la kitaifa la asilimia 95.
Mbali na Njombe mikoa mingine kinara kwa maambukizi ya VVU ni Iringa uliorekodi kasi ya maambukiizi ya kwa asilimia 11.1 katika ripoti ya mwaka 2022-2023 na Mbeya asilimia 9.
Kwa upande wa Iringa, kiwango cha maambukizi kimeonyesha kupungua kidogo kutoka asilimia 9.3 mwaka 2016–2017 hadi asilimia tisa mwaka 2022–2023.