Ni sahihi watoto kupelekwa ‘twisheni’ wakati wa likizo?
- Licha ya mfumo wa elimu kuweka kipindi cha likizo, wazazi wengi hupeleka watoto wao kwenye masomo ya ziada.
- Wadau waeleza kuwa mfumo wa maisha, usalama vyatajwa kama sababu ya watoto kupelekwa twisheni.
- Wadau washauri likizo ipewe nafasi yake chini ya usimamizi.
Dar es Salaam. Mtoto wako anafanya nini akiwa likizo? Jaqueline Kichamo (6) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Moga iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam hutumia likizo yake kwa michezo na kutembelea ndugu jamaa na marafiki.
Awapo likizoni, Jaqueline huchora picha mbalimbali, huangalia katuni, humsaidia mdogo wake Janelle kujifunza kuhesabu na hujisomea vitabu vya riwaya.
Na kwa siku isiyo na jua kali, mtoto huyo huchora miraba ya mchezo wa dama nje ya nyumba yao. na yeyote atakujiunga naye yaani hata kaka yake.
Hali ya Jaqueline ni tofauti na watoto wengine kwani katika kipindi cha likizo, baadhi yao huandikishwa kwenda madarasa ya mafunzo ya ziada almaarufu kama “tuition” jambo ambalo haliwapi tofauti ya likizo na kipindi cha shule.
Mara zote watoto hao hulazimika kuamka mapema ili kuwahi madarasa hayo, ratiba ambayo haitofautiani sana na miezi wanayokuwa masomoni. Hali hiyo inaacha maswali kwa walimu na wadau wa elimu juu ya umuhimu wa likizo kwa wanafunzi.
Mmiliki wa shule ya Stars Academy ya jijini Arusha ambaye pia ni mwandishi wa vitabu (The color of life), Ritha Tarimo amesema anaielewa hofu ya wazazi juu ya elimu za watoto wao.
Hofu hiyo ni ipi?
Tarimo amesema wapo wazazi katika baadhi ya maeneo hasa vijijini ambao watoto wao hupata elimu kutoka kwa walimu wa shuleni pekee na mara zingine, walimu hao hawakidhi mahitaji ya watoto kielimu.
Wazazi hao huona kipindi cha likizo kama muda unaofaa watoto wao kuongeza maarifa hasa ya teknolojia na mambo mengine yanayohusu mtaala ili kuongeza ushindani na ufaulu wakirudi shuleni.
Hata hivyo, Tarimo amesisitiza kuwa inatakiwa kufikia hatua, uelewa na ujuzi wa watoto usipimwe na elimu ya darasani pekee, kwani hata Messi asingekuwa mcheza mpira mzuri, kama asingekuwa mwerevu.
“Tunafikiri watoto wakipata ufaulu wa asilimia 100 au alama A ni uerevu na ndiyo maana tunaogopa kuwaacha wachunguze vitu vingine kwa sababu tunapima uelewa kama rula. Wazazi wajue kuwa watoto wanahitaji kufahamu mambo mengine kwani siyo tu elimu ya darasani inayomfanya mtu kuwa mwerevu,” amesema Tarimo
Kukosa mapumziko siyo kitu kizuri hasa kwa ukuaji wa akili ya mtoto na wengi wanashindwa kulielewa hilo wakidhani shule ndio kitu pekee ambacho mtoto anatakiwa kuwaza mara zote. Picha| Santi Vedrí/Unsplash.
Tarimo anaungana na wadau wengine wa elimu kwa kusema bado ipo haja ya watoto kupata muda wa kupumzika kwani kipindi cha shule mtoto anasoma muda wote kiasi cha kukosa muda wa kupumzika na kujihusisha na shughuli zingine.
“Muda wote ikiwa mtoto anawaza elimu ya darasani tu hata wakati wa likizo, atachoka mapema,” amesema Tarimo.
Naye Mwalimu wa somo la ushairi kutoka Shule ya Msingi ya Dar es Salaam Independent School (DIS), Hilda Mwani amesema “wazazi wengi wanadhani kuwa watoto hawana stress (msongo wa mawazo).”
Dhana hiyo inawapelekea wazazi kuwaamulia watoto na kuwaandikisha kwenye masomo ya wawapo likizoni.
Mwani amesema kukosa mapumziko siyo kitu kizuri hasa kwa ukuaji wa akili ya mtoto na wengi wanashindwa kulielewa hilo wakidhani shule ndiyo kitu pekee ambacho mtoto anatakiwa kuwaza mara zote.
“Wanataka akiamka amkute anasoma, akirudi kutoka kazini amkute kainama anasoma daftari. Asimuone tu kwenye Televisheni, ni kosa la jinai, atasema hadi jua lizame. Mtoto kuangalia Tv akiwa likizo ni sawa na mzazi kwenda kupumzika na wadau viwanja baada ya kazi.
“Wawaache watoto wapumzike, kusoma masomo zaidi ya saba kila siku ya wiki sio kitu rahisi. Akiwa likizo, mwache aangalie TV, mwache acheze, mwache alale, unachoweza kumpa mtoto kama zawadi, ni kumwacha afurahie likizo yake,” Mwalimu Mwani.
Zinazohusiana
- Twaweza: Wazazi wengi hawajui matokeo halisi ya shule za watoto wao
- Sababu za wazazi kuwaongoza watoto kusoma vitabu
- ‘Apps’ za elimu zinavyoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
Wakati hayo yakijadiliwa, mkazi wa jijini Dar es Salaam, Verediana Mwashi ameibua suala la mtindo wa maisha kama sababu inayopelekea wazazi wengi kupeleka watoto “tution” ili kuwabakiza katika reli ya shule kwani mara nyingi wazazi wanakuwa na majukumu ya kikazi.
Mwashi ambaye watoto wake wanafurahia likizo zao kwa mapumziko ya nyumbani, amesema kumjaza mtoto elimu ya darasani pekee siyo vizuri lakini kutokana na mfumo wa maisha, wazazi wengi hawajui namna zingine zinazoweza kuwa mbadala wa “Tuition”
“Wazazi hawaelewi kuwa “tuition” hizi ni mifumo tu ya ajira na watu kujiingizia kipato. Kuna haja gani umpeleke mtoto “tuition” wakati January unalipa ada akayasome hayo hayo?,” amehoji Mwashi.
Ni nini mbadala wa masomo hayo ya likizoni?
Mzazi wa watoto watatu ambaye ni mkazi wa Boko jijini Dar es Salaam, Basiaya Benjamin Kichamo amesema kuwatembelea ndugu hasa babu na bibi inaweza kuwa mpango mzuri wa likizo ya watoto wako kwani ndiyo muda anaojifunza kushirikiana na ndugu zake hasa baada ya kukaa shuleni kwa mwaka mzima.
Kichamo ambaye ni mzazi wa Jaqueline amesema endapo hawawezi kusafiri, basi ni vema watoto wakatumia likizo yao kujifunza majukumu ya nyumbani na kazi mbalimbali nje ya kazi za darasani.
“Kama ni mtoto wa kiume anaweza kujifunza shughuli za bustani, ujenzi na zinginezo na kama ni wa kike, muhimu ajifunze kupika hasa ikizingatiwa kuwa hapati muda huo kwenye kipindi cha masomo,” amesema Kichamo anayeamini likizo ni kwa ajili ya mapumziko.
Pia, Mwalimu Mwani ameongezea masomo ya muziki, kuogelea, kuimba, kucheza mpira na kupiga kinanda, inaweza kuwa fursa kwa mtoto kunoa kipaji chake wakati wa likizo.
Masomo ya muziki, kuogelea, kuimba, kucheza mpira na kupiga kinanda kama baadhi ya vitu vyenye umuhimu vinavyoweza kufikiriwa kama masomo ya ziada. Picha| Unsplash.
Nini kifanyike?
Mdau wa elimu kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Alistidia Kamugisha amesema matatizo yote hayo yameanza baada ya watoto kukosa sehemu za kuchezea.
Amesisitiza kuwa Serikali za mitaa zimeshindwa kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya watoto kucheza na hivyo wazazi wengi wanaona “tuition” kama sehemu salama pale wanapokuwa mbali na watoto wao.
“Hayo yote ni matokeo ya familia nyingi za kiafrika kuwa na watu wengi nyumbani na hivyo, ili kumuepushia mtoto na changamoto ambazo zinaweza kumpata, mzazi anaona bora ampeleke mtoto “tuition” amalize masaa yake nane huko,” amesema Kamugisha.
Ametoa wito kwa Serikali kusaidia kupatikana kwa mazingira salama ya watoto kucheza na ndipo wazazi watakapokuwa huru kuwaachia watoto wao wakacheze nje ya nyumbani wakiamini wapo sehemu ambayo magari na pikipiki hayawezi kupita.
“Watoto sasa hivi ni kama wapo kwenye mapipa. Hawezi kupata hata muda wa kufurahi na wenzike. Kushindwa kwao kucheza ni sababu tunaona watoto wadogo wana vitambi, mtoto wa miaka tisa ana hips (nyonga), they don’t play at all (hawachezi kabisa),” amesema.
Latest