NHIF yaanika viwango vipya vya afya toto kadi
- Viwango hivyo vinaanzia Sh150,000 hadi Sh658,000
- Waziri Mhagama awahimiza wazazi kusajili watoto ili kuokoa maisha.
Arusha. Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) umetangaza viwango vipya vitakavyotumika kulipia kadi za bima ya afya kwa watoto maarufu kama afya toto kadi mwaka mmoja baada ya kufuta kabisa kifurushi hicho.
NHIF iliunda kadi ya bima ya afya kwa mtoto ‘Toto Kadi’ mwaka 2016 ikilenga kutoa kutoa huduma za afya kwa wa watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 waliopo shuleni na vyuoni kwa gharama ya Sh50,400.
Mwaka 2023 huduma hiyo ilisitishwa kwa sababu zilizotajwa kuwa ni kujiendesha kwa hasara ambapo ilidaiwa kuwa mtoto mmoja alitumia wastani wa mara sita zaidi ya kiwango ananchochangia.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dk Irene Isaka aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa mfuko huo jijini Dodoma leo Disemba 17, 2024 amesema viwango hivyo vilivyotangazwa leo ni vile vitakavyotumika kwa ajili ya matibabu ya mtoto mmoja mmoja au makundi ambayo awali yalitolewa katika mfumo huo.
“Watoto wataendelea kuandikishwa kupitia makundi yao ya shule kwa michango ya awali ya shilingi 50,400.00 kwa mwaka,”amesema Dk Isaka.
Kwa mujibu wake vifurushi hivyo vimegawanyika katika makundi matatu kundi la kwanza watalipia Sh 658,000 ambapo wanufaika watakaolazwa wanaweza kupata matibabu ya hadi Sh 22 milioni huku wagonjwa wa nje wakipata matibabu ya Sh 3 milioni.
Kundi la pili watalipia Sh287, 000 ambapo kwa wanaolazwa watapata matibabu ya Sh8 milioni na wagonjwa wa nje Sh 2 milioni na kundi la tatu watalipia Sh150,000 na kupata matibabu ya nje ya Sh1 milioni na yale ya kulazwa Sh 2 milioni.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Jenista Mhagama aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi huo ameipongeza NHIF kwa kufanyia kazi maoni ya Watanzania waliotaka kurejeshwa mfumo huo kutokana na umuhimu wake katika kuokoa maisha.
Pia amewataka wazazi kuitumia fursa hiyo kuwaandikisha watoto wao kupitia mfumo mpya wa kidigitali ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia bima ya afya.
“Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kuwasajili watoto wao ili waweze kuhudumiwa kwa utaratibu wa bima ya afya lakini pia kuhakikisha mnakuwa walinzi wa hizi huduma ili Mfuko usiibiwe kupitia huduma za watoto watakaojiunga kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa sehemu ya kulinda uhai wa Mfuko.”amesema waziri Mhagama.