Namna ya kutibu mafua ukiwa nyumbani
- Tumia njia za asili ikiwemo maji ya uvuguvugu, matunda.
- Inashauriwa kuonana na daktari hata baada ya kupata ahueni.
Dar es Salaam. Kila mtu ana kitu ambacho kinachochea kupata mafua akiwa nyumbani. Kwa wengine ni vumbi, marashi makali na wengine ni kuambukizwa na mtu mwenye mafua.
Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Mapafu la Marekani, mafua yanasababishwa na virusi vinavyoitwa influenza ambavyo huathiri koo, pua na mapafu.
Shirika hilo limesema mafua yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu anayeumwa kupitia kuongea, kupiga chafya na hata kukohoa.
Hata hivyo, zipo njia mbalimbali unazoweza kutumia mtu mzima kupambana na mafua awapo nyumbani kabla ya kwenda hospitali:
Tumia maji ya uvuguvugu yenye tangawizi
Tangawizi ni kati ya mizizi ambayo ina faida nyingi kiafya. Kwa mujibu ya tovuti ya masuala ya kiafya ya Healthline, kikombe cha maji ya moto yenye tangawizi kinaweza kumsaidia mtu kupooza mafua.
Tangawizi pia inaweza kumsaidia mtu ambaye anakohoa au anayejisikia kichefu chefu.
Kwa baadhi, mafua ni shambulio linalowapata kutokana na mzio wa vitu ikiwemo vumbi na malashi makali. Picha| Parents
Vyakula vyenye vitamin C
Ni pamoja na matunda yote jamii ya machungwa na mboga za majani. Vitamin C inachukua nafasi kubwa katika ujenzi wa kinga ya mwili. Kinga inapoimarika, baadhi ya magonjwa ikiwemo maambukizi ya kooni yanaweza kupungua.
Unaweza kukamua juisi ya machungwa na kunywa au kutengeneza chai yenye limao na kuweka asali.
Maji yenye chumvi
Unachohitaji ni maji ya uvuguvugu kwenye glasi na kisha weka kijiko kimoja cha chai chenye chumvi na kisha kuchanganya mchanganyiko huo vizuri.
Baada ya hapo utagogomoa (Gargling) mdomoni na kisha kutema.
Kwa mujibu wa Healthline, hiyo inasaidia kupunguza maambukizi kooni na kumpatia ahueni mtu ambaye ana mafua.
Endapo utapata mafua, inashauriwa kunywamaji mengi. Picha| Shutter Stock
Kunywa maji mengi
Kabla ya kufikiria kunywa dawa, huenda unayachukulia maji poa. Wasichokijua baadhi ya watu ni kuwa, endapo mwili ukiwa na maji itakusaidia kuondoa bakteria mwilini wakati ya kukohoa na kupiga chafya na ndiyo sababu ya watu wenye mafua kushauriwa kutokuzibana chafya zao.
Tovuti ya masuala ya lishe ya Nutritionnews inaeleza kuwa, mtu anayekunywa maji ya kutosha itamsaidia kukabiliana na vijimelea ikiwemo virusi kwa kuwa vitakuwa vinatoka hata kwa kupumua peke yake.
Endapo kunywa maji ni changamoto, unaweza kuangazia maji ya nazi, juisi, chai, matunda yenye maji na supu.
Tumia mafuta muhimu
Wamombo wanayaita “essential oils” ambayo mara nyingi hutumika kwa ajili ya urembo na tiba.
Mathalan, tovuti ya Sciencedirect imeyataja mafuta ya mti wa Mkalatusi. Huzuia virusi kuzaliana pale vinapomfikia mtu ingawa ni ndani ya saa mbili ya maambukizi.
Healthline inashauri, kuweka matone machache ya mafuta hayo kwenye mafuta yako ya kupaka, losheni na hata sabuni za kunawia zilizo kwenye mfumo wa kimiminika.
Mafuta mengine yanayoweza kumsaidia mtu mwenye mafua ni pamoja na mafuta ya mdalasini, mnanaa (mint) na mafuta ya limao.
Hata hivyo, mafua pia yanaweza kuwa dalili ya magonjwa mengine ikiwemo nimonia. Inashauriwa kufika kwenye kituo cha afya ili kupata vipimo na dawa stahiki kwa ajili ya kupata matibabu.
Latest
