Namna ya kudhibiti matumizi mabaya ya pesa mwisho wa mwaka

December 3, 2019 8:30 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Tengeneza na fuata bajeti itakayoongoza mipango yako.
  • Hakikisha matumizi yako inaendana na kipato chako.

Dar es Salaam. Ni wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka. Watu katika maeneo mbalimbali wanajiandaa kufanya manunuzi ya bidhaa na zawadi kwa ajili ya kusheherekea katika familia zao.

Katika kipindi hiki umakini unahitajika hasa katika matumizi ya pesa zako. Usipokuwa makini unaweza kujikuta umetumia pesa nyingi kwa muda mfupi bila kuzingatia hali ya kipato chako, jambo linaloweza kukutumbukiza katika madeni mengi. 

Lakini unaweza kukwama katika kufikia malengo yako na hata kutoa huduma muhimu za familia na watoto kwenda shule.

Ili kuepuka kadhia hiyo, unashauriwa kuzingatia baadhi ya mambo ili kuhakikisha unakuwa na matumizi mazuri ya pesa katika kipindi hiki kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kufungua mwaka.

Tengeneza bajeti 

Siku zote unatakiwa kuipa pesa majukumu mara baada ya kuipata. Maana yake ni kwamba pesa unayoipata kabla ya kuanza kuitumia unatakiwa kuiwekea malengo au kazi inayotakiwa kufanyika.  Na bajeti utakayopanga iendane na kipato chako.  

Simamia matumizi yako. Unaweza kutengeneza bajeti lakini ikawa kazi bure pale unaposhindwa kusimamia matumizi yako kwa kutumia pesa uliyojiwekea malengo fulani. Hivyo ni muhimu mara baada ya kutengeneza bajeti, ukasimamia matumizi ili kuhakikisha kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa kwa wakati sahihi.

Kupanga vizuri matumizi na kuepuka matumizi yasioyo ya lazima kila kitu kitaenda sawa. Picha | Mtandao.

Matumizi yako yaendane na kipato chako

Kitu kingine kizuri cha kuzingatia ni uwezo wa kuishi ndani ya uwezo ulionao. Maana ya kwamba kila wakati unapotumia pesa unajua ni kipi cha kufanya na kwa wakati gani ili tu kuendana na kipato unachokipata.

Usifanye manunuzi ya vitu ambavyo huwezi kumudu gharama au bei zake. Hii itakufanya ukope pesa na kuingia katika mdeni. Jitahidi kutumia vizuri kile ulichonacho ili kuepuka msongo wa mawazo. 

Achana na matumizi yasiyo ya lazima

Mara nyingi unaweza kupata matumizi au matamanio ya kitu fulani ambacho kiko nje ya bajeti uliyojiwekea, unapaswa kuchukua tahadhari. Hakikisha unazingatia bajeti yako ingawa inaweza kuwa ni changamoto lakini hauna budi kuifuata. 

Hata hivyo, kuzingatia bajeti binafsi bado imekuwa changamoto inayowakumba watu wengi, jambo linalowaweka katika hatari ya kuingia katika madeni. Lakini baadhi yao wanasema wameanza kupata muamko wa kutengeneza bajeti katika familia. 

Mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Luckson Hamissi anasema kutokana na tatizo hilo kujirudia mara kwa mara atajitahidi sana mwaka huu kuhakikisha anaweza kufikisha pesa anayopata mpaka mwaka mwingine unapoanza.

“Katika mwezi wa mwisho wa mwaka, mishahara inatoka mapema. Lakini sio hoja ya kwanini tunashindwa kupangia pesa zetu matumizi mazuri. Binafsi tatizo la kuishiwa ada ya mwanagu linanipata sana, ila mwaka huu ntajitahidi kupanga matumizi yaliyo sahihi,” amesema Hamissi. 


Soma Zaidi:


Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasemaje?

Baadhi ya wataalamu wa  uchumi wanasema suala la matumizi ya pesa ni la mtu binafsi hivyo kila mtu anatakiwa kuhakikisha anajua kuweka uwiano wa kipato chake na matumizi anayofanya.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Debrabant iliyopo jijini Dar es Salaam, John Ndimbo anasema kwa kujua kipato ulichonacho ndiyo hatua ya kwanza ya kujua majukumu uliyonayo na malengo uliyojiwekea.

“Katika uchumi tunasema matumizi ya pesa lazima yaendane na kipato, hivyo pale unapotumia zaidi ya kile unachoingiza lazima kuna hasara,” amesema Ndimbo.

Anashauri kuwa watu wawe makini kipindi hiki ili matumizi yaliyo nje ya bajeti zao yasiharibu furaha wanayokusudia kuipata. 

Enable Notifications OK No thanks