Namna ubunifu unavyokuza ‘brand’ na kuiongezea thamani

January 19, 2019 5:05 pm · Charles
Share
Tweet
Copy Link
  • Ubunifu ni kufanya jambo nje ya mazoea na utaratibu unaofanana na wengine.
  • Iwapo utafanywa vyema, ubunifu unasaidia kukuza nembo yako ya biashara na kuiongezea thamani kila uchao.

Ubunifu ni kitu gani? Watu wengi wamekuwa wakijiuliza na kudhani kuwa ubunifu huletwa na kufanywa na watu walioenda shule pekee. Hii siyo kweli.

Neno ubunifu linasimama katika maana ya kufanya vitu nje ya mazoea na utaratibu wa kufanana.

Ukijua namna ya kufanya kitu kile kile kwenye njia tofauti tayari wewe tunakuita mbunifu na mwenye kuiletea tija biashara yako.

Ubunifu ni sahani muhimu sana katika biashara kwani ukiwa mbunifu kuna manufaa yake makubwa yanayosaidia biashara kukua kila siku.

Mfano mdogo sana wa kibunifu ni pale unapokuwa sokoni au gengeni na wote mnauza mchicha wenye kufanana bei na sifa zake nyingine kama mboga.

Ukiweza kuuchambua na kuuosha vema na kurahisisha mchakato wa uoashaji na uchambuaji kwa mteja, hapana shaka utapata wateja wengi kuliko wengine.

Kitendo hicho kina maana wewe ni mbunifu na umeongeza thamani zaidi katika biashara yako na thamani soko lako itakua kwa kasi na kukupeleka katika kilele cha mafanikio.

Kwa nini ubunifu uwepo kwenye biashara?

Zifuatazo ni tija zinazopatikana baada ya mfanyabiashara kuwa mbunifu au kuwa na huduma na biashara ya kibunifu;


Uhakika wa wateja

Kila uchao mteja anatafuta kitu cha tofauti na chenye urahisi na wafanyabiashara wanatakiwa kulifahamu hili na kuliishi kwenye mioyo yao.

Kuna msemo wa Kiingereza husema “a customer is always looking for an  improvement of the service or product” (mteja siku zotye hutafuta huduma au bidhaa iliyoongezwa thamani).

Hii ina maana ukifanya mabadiliko kidogo tu juu ya bidhaa na huduma yako wateja wataongezeka kwako maradufu na kukuza biashara kwa muda mfupi sana.

Thamani utakayoongeza italeta manufaa na kuishi ndani ya mioyo ya watumiaji wa bidhaa au huduma zako.

Moja ya michoro ya Sanaa iliyopo katika Kituo cha MS-TCDC Jijini Arusha. Utengenezaji wa mazingira bora ya biashara ni nguzo muhimu inayotofautisha bidhaa au huduma moja kutoka nyingine. Picha|K15 Photos.


Ubunifu huzaa mabalozi wa biashara

Ubunifu humfanya mteja kuhisi alichokitoa hakilingani na thamani kubwa ya kile alichokipokea.

Jambo hili humfanya awe mteja wa kudumu na kugeuka kuwa balozi wa biashara yako bila yeye kujua kutokana na kuguswa zaidi na huduma au bidhaa.

Kama nilivyoeleza hapo awali mteja hapendi mambo mengi tena yale yale ya kila siku. Mteja anahitaji vitu vizuri na vipya.


Soma zaidi:


Mahitaji yanalazimu kuanzishwa kwa dawati au timu ya wabunifu katika biashara zetu ambayo kazi yao kubwa ni kukaa na kutafuta njia zitakazotufanya kuwa mbele ya soko hili la leo na kesho.

Hii itafanya tusitumie pesa nyingi kukuza biashara zetu kwa kuwa mambo tunayofanya yatakuwa ni matokeo ya kutumia muda mwingi kufikiri namna ya kuifanya nembo (brand) yangu kusimama sokoni.

Ubunifu pia unaleta mahusiano ya karibu sana ya kihisia baina ya mteja na bidhaa au huduma “product emotional intelligence”.  

Muuza wa matunda Jijini Arusha akimhudumia mteja hivi karibuni. Ubunifu unasaidia kujenga brand yako ya kibiashara na kuiongezea thamani. Picha|K15 Photos.

Biashara inayojiboresha huongeza hisia za karibu kwa wateja

Hii huja pale mteja anapotumia huduma na bidhaa husika kama sehemu ya maisha yake.  Wapo ambao bila kusoma tovuti ya nukta.co.tz hawajisikii vizuri kwa kuwa imekuwa sehemu ya maisha yao.

Hali hiyo inajengwa sana na bidhaa kuwa yenye tabia za kubadilika na kuweka vionjo vya mlengo wa mteja.

Kama wafanyabiashara yatupasa tujue mahusiano ya bidhaa na huduma zetu na wateja.

Je, wananunua kwa sababu zipi? Je, wananunua kwa sababu hawana sehemu nyingine ya kununua au mahitaji yao lazima wanunue?

Je, wananunua huduma au bidhaa kwa sababu ni sehemu ya furaha na faraja kwao?

Maswali haya yatakupa majibu sahihi na kuweza kukusaidia uanzie wapi na kukuza utofauti katika ya biashara yako na wenzio wanaofanya kitu kinafanana.

Biashara, bidhaa na huduma bila kuchanganywa na ubunifu thamani yake itabaki kuwa yenye kufanana na nyingine kutokukua.

Sisi tulioamua kuingia kwenye ulimwengu huu wa kibiashara lazima tujibebeshe huu mzigo wa kuwa wabunifu na wenye kutafuta utofauti kila siku.

Charles Nduku maarufu kama Mr Brand ni mkufunzi wa wajasirimali katika masuala ya masoko na uhamasishaji wa kimaisha. Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana naye kupitia +255762918153 au baruapepe mrbrandtz@gmail.com.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...