Mwakyembe, wabunge wavutana TBC 1 kurusha matangazo kwa ‘upendeleo’

May 14, 2019 8:37 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amewataka wote ambao hawaamini kuwa TBC 1 inaweza kupokea na kurusha maudhui ya kila mtu, basi wampelekee yeye waone kama hayatarushwa. Picha|Mtandao.


  • Amesema hakuna upendeleo unaofanyika kwa runinga hiyo ya Taifa katika urushaji wa maudhui kwa umma.
  • Amesema kila mtu anaruhusiwa kupeleka maudhui yake, kama kuna mtu ana wasiwasi ampelekee yeye atayarusha. 
  • Wabunge waonyesha wasiwasi wao kuhusu usawa wa maudhui ya TBC 1.

Dar es Salaam. Kutokana na kuwepo kwa madai kuwa runinga ya Taifa ya TBC 1 inatoa matangazo yake kwa upendeleo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amekana madai hayo na kusema watu wenye maudhui wampelekee yeye ili yatolewe kwa umma. 

Dk Mwakyembe ametoa ufafanuzi huo bungeni leo (Mei 14, 2019) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Sophia  Mwakagenda ambaye alitaka kufahamu TCRA inaisimamia vipi TBC kuweza kuonyesha habari kwa uhakika bila upendeleo kwa vyama vyote na wananchi wote ikizingatiwa kuwa runinga hiyo ni ya umma. 

Wakati akijibu swali hilo, Mwakyembe amesema suala la maudhui ya TBC 1  liko wazi na hakuna upendeleo unaofanyika na watu wote wanakaribishwa kupeleka maudhui yao yaonyeshwe kwa umma.  

“Suala la maudhui ya TBC ni wazi kama una maudhui yako peleka hakuna upendeleo wowote unaofanyika, wewe kama unamini ni upendeleo shauri yako, leta maudhui yako yaonyeshwe,” amesema.

Baada ya kutoa ufanunuzi huo, baadhi ya wabunge walionekana wakiguna ikiashiria hawakuridhishwa na majibu ya Dk Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kyela mkoani Mbeya. 


Zinazohusiana:


Lakini amewataka wote ambao hawaamini kuwa TBC 1 inaweza kupokea na kurusha maudhui ya kila mtu, basi wampelekee yeye waone kama hayatarushwa. 

“Kama kuna mtu ana wasiwasi, maana wanaoongea hawajawahi kupeleka maudhui, nileteeni mimi kama maudhui hayo hayataonyeshwa,” amesisitiza Mwakyembe.  

Hata hivyo, amesema TBC 1 kama vituo vyote vya Taifa duniani vina hadhi ya ‘must carry’ (kubebwa) na kila kisimbuzi lazima kibebe na huo siyo utaratibu wa Tanzania pekee bali unatumika duniani kote.

Oktoba, 2017, wakati akizungumza katika mdaharo ulioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Dutch Velle (DW), Dk Mwakyembe alisema watanzania wanapaswa kufahamu kuwa TBC 1 ni chombo cha Serikali na ni lazima kitatoa maudhui ynayoendana na shughuli za Serikali. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW