MV Logos Hope: maktaba inayoelea inavyohamasisha usomaji wa vitabu duniani

November 7, 2023 12:16 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Watanzania 45,453 waitembelea ndani ya siku 14.
  • Imeondoa mtizamo hasi kuwa Watanzania hawapendi kusoma.
  • Mbioni kutengeneza meli mpya maalumu kwa kila bara.

Dar es Salaam. ‘Maarifa yamefichwa kwenye vitabu someni’ ni miongoni mwa kauli maarufu sana ulimwenguni, ikiwa na lengo la kuhamasisha watu kujisomea vitabu ili kuvumbua hazina za maarifa, busara na hekima zilizohifadhiwa.

Wakati nyanja za upatikanaji wa maarifa zikizidi kuongezeka kutokana na maendeleo ya teknolojia baadhi ya watu bado wanaamini kusoma vitabu ndio njia bora zaidi wakiwamo waanzilishi wa meli ya MV. Logos Hope.

Meli ya MV Logos Hope huzunguka katika mataifa mbalimbali ulimwenguni ikiwa imesheheni maelfu ya vitabu na kuwapa fursa wakazi wa mataifa hayo, kujisomea na kujifunza tamaduni mpya.

Miongoni mwa vitabu vilivyosheheni katika meli hiyo ni vile vinavyohusu uongozi, mapishi, masomo ya watoto, dini, pamoja na vitabu vya hadithi vilivyoandikwa na waandishi kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Afrika, Asia na Ulaya.

Hatimaye, mara baada ya miaka sita kupita, Oktoba 11, 2023, MV Logos Hope au kwa jina la utani ‘maktaba inayoelea’ iliwasili tena jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania na kuwapa nafasi zaidi ya Watanzania 45,453 kusoma vitabu.

Alessandro Del Corso, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka kampuni ya meli ya GBA inayomiliki meli hiyo, ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa sababu za meli hiyo kuzunguka katika nchi mbalimbali ni kuwawezesha wazawa kununua vitabu kwa bei nafuu huku wakiongeza maarifa.

“Logos Hope tupo Tanzania kwa lengo la kusambaza maarifa na kukutana na watu wengi, tunatumaini kuwa kupitia meli hii tunaweza kuongeza ari ya usomaji vitabu kwa wazawa,” amesema Alessandro.

Mbali na Tanzania, hivi karibuni meli hiyo imetembelea nchi za Kenya,Ushelisheli,Oman, Dubai, Iraq na nyingine 81 tangu mwaka 2005. 

Meli ya Loges Hope kiundani

Iliundwa mwaka 1970, ina upana wa mita 21.06 na urefu wa mita 132.50 ambapo zaidi ya watu 442 kutoka mataifa zaidi ya 70 wanajitolea katika meli hiyo kuishi wakipokea maelfu ya wasomaji wa vitabu kila siku.

Kwa nje meli hiyo imenakshiwa kwa rangi nyeupe na maandishi makubwa ya rangi ya bluu yaliyoandikwa “Logos Hope’ yakibeba utambulisho wa meli hiyo kutoka kampuni ya meli GBA.

Kwa ndani ina sehemu kubwa ya vitabu, mgahawa, eneo la wazi lililonakshiwa kwa picha zinazoelezea historia ya maisha ya vijana, sehemu ya burudani ya muziki, maliwato na maeneo mengine ya kufulia, kuoka (bakery) pamoja na chumba cha uendeshaji.

Ni fursa ya kujipatia vitabu kwa bei rahisi

Bakari Hussein Mkazi wa jiji la Dar es Salaam aliyetembelea meli hiyo kwa mara ya pili amebainisha kuwa ubora na unafuu wa bei ya vitabu vilivyopo katika meli hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyowavutia watu wengi zaidi kutembelea meli hiyo.

“Hii ni mara yangu ya pili nakuja na kila nikija sikosi vitabu vya kuchukua,binafsi naona ni fursa nzuri kupata vitabu kwa bei rahisi na vyenye ubora wa hali ya juu,”

Kwa upande wake mwandishi mkongwe wa vitabu nchini aliyejitambulisha kwa jina la Bibi Subira anasema meli hiyo imekuja kukosoa usemi wa kwamba watanzania hawapendi kusoma vitabu kutokana na wingi wa watu waliohudhuria.

“Hiyo inaonyesha kuwa lile wazo la kwamba watanzania hawapendi au hawajihusishi vitabu siyo kweli, nimekutana na watu wengi ambao wanasema kila wakija wanakuta meli imejaa…nawasihi watanzania wenzangu tuendelee kusoma na kuandika vitabu,” amesema bibi Subira.


Soma zaidi:Faida, hasara za kupungua kwa wakulima Tanzania


Vitabu vya Watanzania adimu

Licha ya wingi wa vitabu uliopo, baadhi ya watembeleaji wa meli hiyo wamelalamikia kutokuwepo kwa vitabu vingi vilivyoandikwa na waandishi wa kitanzania na kutoa ombi kwa uongozi wa meli hiyo kuhakikisha upatikanaji wa vitabu hivyo ili kuvutia watu wengi zaidi.

Hata hivyo, Alessandro amesema miongoni mwa sababu inayozuia upatikanaji wa vitabu vya waandishi wa kitanzania katika meli yao ni makontena ya vitabu hivyo kutokufika kwa wakati katika nchi wanazozitembelea.

“Tuna washirika mbalimbali ambao hujitolea kutupa vitabu au kutuuzia kwa bei nafuu  ndiio maana unaona nasisi tunauza kwa bei nafuu zaidi…changamoto ni kwamba makontena ya vitabu huwa yanachelewa kufika…

…Mfano kama kontena la vitabu vilivyoandikwa na watanzania lipo njiani unakuta mpaka lifike huenda sisi tutakuwa tumeshaondoka kwenye nchi nyingine,” ameongeza Alessandro.

Meli ya Logos Hope ina jumla ya wafanyakazi 250 wanaojitolea kutoka mataifa zaidi ya 70 duniani.Picha|Logos Hope

Serikali yajipanga kuongeza usomaji wa vitabu Tanzania

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Waziri Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24, alisema kuwa Serikali imeanza kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa kuanza na wanafunzi na wanajamii.

Prof Mkenda alieleza kuwa Serikali imefanya uhamasishaji wa usomaji wa vitabu kwa jamii na shule kupitia programu mbalimbali ikiwemo programu ya ‘Outreach’ kwenye vituo 43 vinavyotoa huduma za maktaba na maonesho ya kimataifa ya vitabu yaliyohusisha wadau takribani 858 kutoka shule na vyuo.

Shughuli nyingine ni uendeshaji wa warsha kwa Chama cha Wachapishaji (PATA) pamoja na kuendelea kuandaa mwongozo wa uanzishaji na matumizi ya maktaba shuleni.

“Serikali imesambaza nakala za vitabu 21,200 katika maktaba za mikoa 20 ambayo ni Kagera, Mwanza, Mtwara, Kilimanjaro, Ruvuma, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Singida, Tabora, Tanga, Shinyanga, pamoja na maktaba za wilaya 19 zilizopo nchini.

Tutarajie nini miaka ya baadae

Ikiwa umekosa kutembelea meli hii ambayo iling’oa nanga Oktoba 22, 2023 jiandae kwa ajili ya ujio wake kwa mara ya tatu hivi karibuni, kwani wamiliki wa meli hiyo wanatamani kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kujenga meli nyingine katika kila bara ili kuongeza safari za mara kwa mara katika nchi wanazozitembelea.

“Mipango yetu  ya baadae ni kuwa na meli nyingine ili iwe rahisi kutembele nchi nyingi zaidi kwa haraka na kwa karibu…miaka sita ni mingi tunatamani tuwe tunatembelea nchi kila mwaka,” amesema Alessandro.

Enable Notifications OK No thanks