Mkuchika aeleza rushwa inavyoathiri utoaji wa vibali, leseni kwa wawekezaji Tanzania

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kampteni George Mkuchika (katikati), akiwa katika kongamano la siku maalum dhidi ya rushwa lililofanyika katika Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk Bashiru Ally na kulia ni Mkurugenzi Mkuu Takukuru, Diwani Athuman. Picha|Maelezo.
- Waziri huyo wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema inakwamishwa ukuaji wa uchumi na miradi ya maendeleo.
- Amesema vikwazo vya upatikanaji wa vibali na leseni za biashara vikiondolewa, wawekezaji wanaweza kuongezeka nchini.
- Takukuru yasema itaendelea kushughulika kikamilifu na watoaji na wapokeaji rushwa.
Dar es Salaam. Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika amesema kuwepo kwa rushwa katika idara za Serikali zinazotoa vibali na leseni za biashara, kunaathiri uwekezaji wa kigeni na miradi ya maendeleo nchini.
Akizungumza katika kongamano maalum dhidi ya rushwa katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Saba Saba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam leo (Julai 3, 2019), amesema sekta ya viwanda na biashara inaathiriwa zaidi na ucheleweshaji wa utoaji vibali na leseni ambazo ni muhimu kwa wawekezaji kuendelea na shughuli zao.
Amesema vikwazo hivyo wanavyopata wawekezaji vikiondolewa vinaweza kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali katika kupunguza tatizo hilo ambalo limekuwa likiathiri sekta binafsi ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
“Kwa sasa vyombo vyetu vyote serikalini si Takukuru (Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa) pekee bali pia polisi, TISS(Idara ya Usalama wa Taifa), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na vingine vyote, vimeendelea kuungana katika kusimamia masuala ya utawala bora na hili limeleta msukumo na hamasa mpya katika vita dhidi ya rushwa hapa nchini,” amesema Waziri huyo.
Aidha, amesema kutokana na serikali kutambua mchango wa sekta ya viwanda na biashara katika kukuza uchumi, Serikali imekuwa ikifanya marekebisho mbalimbali ya sheria na sera mbalimbali ambazo zimekuwa ni sehemu ya mianya ya rushwa nchini ikiwemo eneo la kodi.
“Kutokana na kudhibiti rushwa kwa sasa kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya mwezi yameweza kuongezeka kutoka Sh800 bilioni kwa mwezi hadi kufikia Sh1.3 trilioni. Hii inaonyesha kuwa kulikuwa na maeneo ambayo kulikuwa na uvujaji wa mapato ya Serikali kulikochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo rushwa,” amesema Mkuchika.
Soma zaidi: Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kupitia mpango mkakati dhidi ya mapambano ya rushwa (NASCAP III) ili kuhakikisha kuwa mapambano na vita dhidi ya rushwa yanapata mafanikio nchini.
Kupitia NASCAP III, ofisi yake imeendelea kutekeleza masuala mbalimbaliu ikiwemo kufanya tafiti kubaini ukubwa na kiwango cha rushwa nchini, kupokea maoni, kutoa elimu kwa umma kupitia makongamano, rushwa pamoja na kufanya uchunguzi na kufungua mashtaka kwa watu mbalimbali wanaopatikana na hatia dhidi ya rushwa