Mitandao ya kijamii kudhibiti biashara haramu ya pembe za ndovu

November 16, 2018 11:42 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  •  Kampuni za teknolojia na mitandao ya kijamii yaungana kudhibiti biashara haramu ya pembe za ndovu inayoratibiwa mtandaoni.
  • Muungano huo ni kuunga juhudi za Umoja wa Mataifa kuwaokoa wanyamapori ambao wako hatarini kutoweka.
  • Tanzania nayo yaendelea kutekeleza mradi wa kuwafunga kola za satelaiti tembo waliobaki ili kufuatilia mienendo yao.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi Wanyama pori (WWF) ikiendelea kutekeleza mradi wa kuwavalisha tembo kola maalum ili kuwalinda dhidi ya majangili, mtandao wa watumiaji wa teknolojia duniani wameungana kutokomeza biashara haramu ya pembe za ndovu inayofanyika mtandaoni.  

Hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za mashirika ya kimataifa na nchi wahisani ikiwemo Tanzania katika kukabiliana na ujangili unaotishia kutoweka kwa tembo katika maeneo mbalimbali duniani. 

Takwimu za sensa ya tembo zinaeleza kuwa idadi ya tembo barani Afrika imepungua kwa asilimia 30 kati ya mwaka 2007 na 2014. Tanzania nayo imekumbwa na anguko kubwa la idadi ya tembo ambapo inakadiriwa kuwa wamepungua kwa asilimia 80.

Kundi la wafanyabiashara mtandaoni, teknolojia na mitandao ya kijamii duniani wanashirikiana na WWF, Shirika la kimataifa la usafiri na mfuko wa kimataifa wa masuala ya wanyamapori (IFAW) wakiwa chini ya Muungano wa Kutokomeza Biashara Haramu ya pembe za ndovu mtandaoni.

Mashirika na makampuni yaliyojiunga na mtandao huo ni Mall for Afrika, eBay, Alibaba, Etsy, Baidu, Baixing, Huaxia Collection, Qyer, Kuaishou, Pinterest, Ruby Lane, Shengshi Collection, Tencent, Wen Wan Tian Xia, Zhongyikupai, Zhuanzhuan, 58 Group, Google na Microsoft.

Katika orodha hiyo kuna kampuni nyingi kutoka China, sababu kubwa ni kuwa kampuni hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali ya nchi yao ambayo imepiga marufuku na kufunga biashara zote zinazohusika na bidhaa za pembe za ndovu.

Mitandao ya kijamii yenye wafuasi wengi duniani ya Facebook, Instagram nayo inatumia majukwaa yao kuunga mkono kampeni hiyo ya kuwalinda tembo.

Lengo la mtandao huo ni kuzuia na kupunguza biashara hiyo kwenye majukwaa ya mtandaoni kwa asilimia 80 ifikapo 2020 na kuhakikisha biashara ya mtandaoni haihujumiwi na majangiri na wafanyabiashara wasiofuata taratibu za kimataifa.

Kupitia mtandao huo umetengenezwa mfumo wa data wa kufuatilia mienendo ya wanyamapori kwenye hifadhi na biashara ya bidhaa za tembo. Pia miongozo na taratibu za kufuata katika biashara ya wanyamapori inayofanyika mtandaoni ili kuepusha majangili na watu wasio na nia njema kutumia teknolojia kufanya uhalifu dhidi ya wanyamapori.


Zinazohusiana: Biashara ya mtandaoni ni tishio kwa maduka makubwa Tanzania?


Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa WWF duniani, Cawford Allan amesema wahalifu na majangili wanaua na kuuza wanyamapori na bidhaa zake kwasababu hakuna sera za pamoja za mtandaoni za kulinda na kuhifadhi wanyamapori.

“Kukosekana kwa chombo cha pamoja kunatengeneza tatizo. Haya makampuni yameona tatizo na wameungana kuhakikisha intaneti haitumiwi vibaya na wafanyabiashara haramu”, alinukuliwa Allan wakati wa uzinduzi wa mtandao huo Machi mwaka huu.

Tembo bado wanakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na ujangiri na biashara haramu. Picha| WWF

Hata hivyo, kampeni ya kuwafunga kola tembo (Elephant tracking device) inaendelea nchini hasa katika Pori la Akiba la Selous ambalo limeathiriwa zaidi na vitendo vya ujangiri na kupoteza karibu asilimia 90 ya tembo. Kampeni hiyo inawasaidia askari wanyamapori kukabiliana na majangili na kuhakikisha idadi ya tembo inaongezeka katika hifadhi za taifa.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa miezi 12  ambapo tembo 60 katika hifadhi ya Selous watafungwa kola shingoni. Hatua hiyo itawawezesha wasimamizi wa hifadhi kufuatilia mienendo ya tembo, kubaini na kukabiliana na hatari yoyote dhidi ya wanyama hao.

Kola hizo zimeunganishwa na mfumo wa ‘satellite’ ikiwa ni njia iliyohakikiwa na wanasayansi katika kufuatilia mienendo na ulinzi wa tembo. Kabla ya tembo kuvalishwa kola maalumu anapewa dawa ya usingizi na kuchukuliwa taarifa zake za kiafya. Atafuatiliwa kokote aendako na ikiwa atakabiliwa na hatari, askari watajitokeza mara moja kumsaidia.

Kwa miaka 40 iliyopita ujangili wa Tembo katika hifadhi ya Selous ilichochewa na biashara ya pembe za ndovu ambazo zilikuwa zinahitajika sana katika bara la Asia hasa nchini China. Inakadiriwa idadi ya Tembo katika pori hilo ilishuka kutoka 110,000 hadi chini ya 15,000 mwaka 2014.

Mwaka 2014, Shirika la Elimu na Utamaduni (UNESCO) liliiweka Selous katika orodha ya urithi wa dunia ambao uko katika hatari ya kutoweka kwasababu ya matukio yasiyo ya kawaida ya ujangili wa tembo. Lakini wakati huo Serikali iko katika mchakato wa kutekeleza mradi mkubwa wa

Enable Notifications OK No thanks