Misingi 10 iliyowezesha Kiswahili kuadhimishwa Julai 7
- Ni lugha ya mawasiliano inayozungumzwa na watu wengi.
- Inatumika katika taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo UN.
- Kimebeba historia ya ukombozi wa bara la Afrika.
Dar es Salaam. Baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Julai 7 kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, limesema uamuzi huo wa kihistoria umetokana na misingi 10 ikiwemo ni lugha hiyo ni nyenzo muhimu ya kufanikisha ajenda za maendeleo duniani.
Mkutano mkuu wa 41 wa UNESCO uliofanyika Novemba 23, 2021 ulipitisha azimio namba 41C/61 la Siku ya Kiswahili Duniani ambapo uamuzi huo umetokana na misingi mikuu 10.
-
Kiswahili na mawasiliano
Lugha siyo tu njia ya mawasiliano bali ni kielelezo cha utamaduni na huonyesha utambulisho, maadili na dira ya dunia. Ni chombo ambacho kinawasilisha tofauti mbalimbali za tamaduni na mazungumzo ya ustaarabu.
“Ni daraja linalowezesha uhusiano wa karibu baina ya jamii na ni utajiri thabiti wa kujieleza na kubadilishana mitazamo mbalimbali pamoja na kumwezesha mtu,” imesema UNESCO.
-
Umoja wa Mataifa na matumizi ya lugha zaidi ya moja
Matumizi ya lugha zaidi ya moja ambayo ni msingi wa maadili ya Umoja wa Mataifa ni kigezo muhimu cha kujenga mawasiliano bora baina ya watu, kwa kuwa inaimarisha umoja katika utofauti na maelewano ya kimataifa , stahmala na mashauriano.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 71/328 la Septemba 11 mwaka 2017 kuhusu matumizi ya lugha zaidi ya moja, lilikaribisha utekelezaji wa kutengwa kwa siku mahsusi kuadhimisha kila lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa ili kuhabarisha na kupaza sauti kuhusu historia ya lugha hiyo utamaduni wake, matumizi na kuhamasisha
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na taasisi kama vile UNESCO kufikiria kupanua wigo wa mpango huo kwa hata lugha nyingine zisizo rasmi lakini zinazungumzwa duniani.
Kiswahili ni lugha isiyo rasmi inayotumiwa na UN katika shughuli mbalimbali. Picha| iStock.
3. Wazungumzaji wa Kiswahili duniani
Kiswahili ni moja ya lugha zinazozungumzwa zaidi barani Afrika na huzungumzwa na zaidi ya watu milioni 100 duniani.
- Kiswahili Afrika Mashariki, Kati na Kusini
Ni lugha inayotumika zaidi katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini pamoja na Mashariki ya Kati. Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu vikubwa duniani ikiwemo nchini Afrika Kusini, Kenya na Tanzania.
-
Kiswahili na kufanikisha SDGs na AcFTA
Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Ni kwa mantiki hiyo ni nyenzomuhimu sana katika kufanikisha ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na kufanikisha pia ushirikiano wa kikanda hususan katika kutekeleza mkataba wa eneo la soko huru barani Afrika (ACFTA).
-
Kiswahili katika Idhaa za Umoja wa Mataifa
Katika miaka ya 1950, Umoja wa Mataifa ulianzisha Radio ya Umoja wa Mataifa na leo hii Kiswahili ni idhaa pekee ya lugha ya kiafrika kwenye Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (DGC).
Kuadhimisha lugha hiyo Julai 7 kila mwaka ni uamuzi sahihi kwa sababu ni lugha ya kimataifa.
-
Kiswahili na utajiri katika utofauti wa kiisimu
Tofauti ya kiisimu na uzungumzaji wa lugha mbalimbali ni maeneo yenye umuhimu wa kimkakati ambayo UNESCO inaendeleza katika nyanja zote kupitia majukumu yake ya kisekta.
Kuna mafanikio makubwa ya uelewa kuhusu nafasi ya lugha katika maendeleo siyo tu katika kuhakikisha vinafanikisha utofauti wa kitamaduni na mashauriano baina ya watu wa lugha na tamaduni mbalimbali bali pia katika kufanikisha elimu bora kwa wote.
Pia kuimarisha ushirikiano katika kujenga ufahamu kwenye jamii na kuhifadhi urithi wa utamaduni na kusongesha utashi wa kisiasa wa kunufaika na sayansi na teknolojia kwa maendeleo endelevu.
Kiswahili ni lugha muhimu ya kufundishia hasa nchini Tanzania. Pia inaunganisha watu wa makabila yanayozungumza lugha tofauti. Picha| Growing Opportunities.
-
Kiswahili ni lugha rasmi ya SADC
Mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC waliokutana jijini Dar es salaam nchini Tanzaina Agosti mwaka 2019, waliridhia Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kazi katika chombo hicho, Kwa kutambua mchango wake katika kujenga amani na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla.
-
Kwa nini 7/7 na si tarehe nyingine?
Julai 7, 1954 ni siku ambayo chama cha Tanganyika African National Union (TANU) chini ya hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania kilipitisha Kiswahili kama lugha ya kuunganisha harakati za ukombozi.
Naye Rais wa zamani na pia Baba wa Taifa la Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta alitumia lugha ya Kiswahili kupitia kauli yake maarufu, “Harambee” ya kuhamisha watu wakati wa harakati dhidi ya ukoloni.
Zaid ya hapo Julai 7 mwaka 2000, EAC ilianzishwa tena kurejesha ushirikiano na utangamano baina ya wananchi wa Kenya, Tanzania na Uganda ambako Kiswahili kinazungumzwa zaidi. Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zilijiunga katika jumuiya hiyo.
- Kiswahili ni maisha ya kila siku
Siku ya kimataifa itaadhimishwa na wadau kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili duniani kama lugha ya mawasiliano duniani iliyojengwa kwenya maisha ya kila siku ya waafrika kupitia tamaduni zao mbalimbali.
Latest