Mifuko ya plastiki kuondolewa kwa hatua: Makamba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba amesema marufuku ya mifuko ya plastiki itaibua uchumi mpya wa mifuko mbadala ambao utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia maendeleo ya Taifa. Picha| Mtandao.
- Amesema zoezi hilo litaenda hatua kwa hatua kabla ya kuondoa kabisa mifuko hiyo nchini.
- Amesema mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku ni vibebeo na siyo vifungashio.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba amesema zoezi la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki litaenda hatua kwa hatua kabla ya kuondoa kabisa mifuko hiyo nchini.
Makamba aliyekuwa akizungumza leo (Mei 27, 2019) wakati wa mkutano wa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kuhusu marufuku ya mifuko ya plastiki, amesema safari ya kuondoa mifuko ya plastiki nchini lazima iwe hatua kwa hatua na sasa ni vibebeo vya plastiki pekee ndiyo havitaruhusiwa.
“Safari ya kuondoa mifuko ya plastiki hapa nchini lazima iwe kwa hatua, haiwezi kukwama kwa wakati mmoja, mnapiga marufuku kila kitu! kwa hiyo tumeanza na mifuko ya plastiki, taratibu kadiri miaka inavyoenda tutaenda hatua kwa hatua,” amesema Makamba na kuongeza;
“Wale waliokuwa na wasiwasi kwamba bidhaa za vyakula na nyingine zinazofungwa kutoka kiwandani kwamba zitapigwa marufuku hapana! kilichopigwa marufuku ni mifuko ya plastiki tu na wala siyo packing (vifungashio) nyingine za plastiki.”
Amebainisha kuwa hatua hizo za kuondoa mifuko ya plastiki zitaenda sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mifuko mbadala na kuachana na mifuko ya plastiki.
Soma zaidi:
- Makamba awatahadharisha wafanyabiashara wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki
- Kanuni za kuzuia mifuko ya plastiki zakamilika
- Serikali kudhibiti mifuko ya plastiki kwa awageni wanaoingia Tanzania
Katika hatua nyingine, Makamba amesema marufuku hiyo itaibua uchumi mpya wa mifuko mbadala ambao utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Tumeona vijana wengi wamejitokeza na wanahamasika kufundishana kutengeneza mifuko mbadala baada ya jambo hili kuonyesha litatikisa uchumi na uzalishaji. Tunaona ni jambo ambalo litaibua uchumi mpya na kuleta maendeleo hapa nchini,” amesema Makamba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema watendaji katika wilaya yake wanaendelea kutoa elimu na mpaka sasa wameanzisha vituo 15 vya kukusanya mifuko ya plastiki iliyotumika na isiyotumika bado ili kuwaondolewa wananchi usumbufu wa kulipa faini ifikapo Juni Mosi mwaka huu.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amesema wanatumia njia mbalimbali kuwaatarifu wananchi kuhusu marufuku ya mifuko ya plastiki ikiwemo mabango sita yaliyosambazwa katika wilaya hiyo.
Aprili 9, 2019 Waziri mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza rasmi marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ifikapo Juni 1 mwaka huu ambapo marufuku hiyo itahusisha utengenezaji, ununuzi na kuuza ili kunusuru uharibifu wa mazingira, vifo kwa wanyama na kuziba kwa mitaro.