Mfumuko wa bei mwaka 2019 washuka, ada shule binafsi juu
Ukiachana na kushuka kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula, NBS imesema wastani wa mfumuko wa bei za bidhaa zisizojumuisha vyakula na nishati umepaa hadi asilimia tatu mwaka 2019 kutoka asilimia 1.9 iliyoripotiwa mwaka juzi. Picha|Arturo Rivera/Unsplash.
- NBS yasema wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2019 ulishuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.5 ya mwaka juzi.
- Hata hivyo, ada katika shule binafsi za msingi na sekondari ziliongezeka mwaka jana.
- Bei za kumuona daktari katika hospitali binafsi nazo zilipanda.
- Mwaka 2019 ulikuwa ni mwaka wa maumivu na tabasamu kwa baadhi ya Watanzania.
Dar es Salaam. Wastani wa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka 2019 umeshuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.5 iliyorekodiwa mwaka juzi ukichangiwa zaidi na kushuka kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula.
Licha ya wastani wa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma nchini kushuka mwaka jana, taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kuwa wastani wa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula ulipaa hadi asilimia 4.3 mwaka jana kutoka asilimia 3.7 ya mwaka 2018.
Kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa za vyakula hupeleka maumivu kwa familia nyingi nchini hususan zenye kipato cha chini.
“Wastani wa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za vyakula umepungua hadi asilimia 4 mwaka 2019 kutoka asilimia 4.3 mwaka 2018,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ukiachana na kushuka kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula, NBS imesema wastani wa mfumuko wa bei za bidhaa zisizojumuisha vyakula na nishati umepaa hadi asilimia tatu mwaka 2019 kutoka asilimia 1.9 iliyoripotiwa mwaka juzi.
“Baadhi ya bidhaa zilizochangia kuongezeka kwa wastani wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwaka 2019 ni pamoja na gharama za kumuona daktari hospitali binafsi kwa asilimia 4.1, mavazi kwa asilimia tatu, samani (asilimia 3.4), vyombo vya jikoni (asilimia 4.7)…na vitabu vya shule kwa 2.2,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mtakwimu Mkuu, Dk Albina Chuwa.
Mbali na bidhaa hizo, wazazi na walezi mwaka jana walitoboa zaidi mifuko yao baada ya NBS kubainisha kuwa gharama za ada kwa shule binafsi za msingi ilipanda kwa asilimia 2.5 huku shule binafsi za sekondari ikipanda kwa asilimia 3.2.
Zinazohusiana:
Mfumuko wa Desemba wang’ang’ani pale pale
Wakati wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2019 ukishuka kidogo, mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Desemba 2019 umeendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 3.8 kama ilivyokuwa katika mwaka ulioishia Novemba ukichagizwa zaidi na kupanda na kushuka kwa bei za baadhi ya bidhaa za chakula na zisizo za chakula.
NBS inaeleza kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei ikilinganishwa na ilivyokuwa Desemba 2018 ni mchele uliopanda kwa asilimia saba, maharage (asilimia 7.7), mtama (asilimia 3.3), viazi mviringo (asilimia 2.7) na nyama kwa asilimia 2.3.
Desemba ni mwezi ambao hutawaliwa na sikukuu za mwisho wa mwaka na kupanda kwa bei huwa ni maumivu kwa familia nyingi hususan zenye kipato cha chini.
Hata wakati baadhi ya bidhaa za chakula zikipanda bei, NBS imesema kuna baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilishuka bei na kuleta nafuu kwa walaji.
Baadhi ya bidhaa hizo zilizoshuka bei katika mwaka ulioishia Desemba 2019 ikilinganishwa na ilivyokuwa Desemba mwaka juzi ni mafuta ya taa kwa asilimia 7.1, mafuta ya petroli na dizeli (asilimia 8.7), gesi ya kupikia (asilimia 2.1), na jiko la gesi la kupikia kwa asilimia 1.6.
“Mfumuko wa bei wa bidhaa za chakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Desemba 2019 umeongezeka hadi asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 kwa mwaka ulioishia Desemba 2018,” imesema taarifa hiyo ya NBS.
Latest
