Mfumo wa malipo wa QR Code unavyosaidia kupunguza gharama za maisha

March 15, 2019 9:04 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumo huo wa malipo unafanya kazi kwa kutumia kamera ya simu janja ambayo inaskani msimbo (CODE) na kisha kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi.
  • Baadhi ya Watanzania wameziomba kampuni kama Visa na Mastercard kutoa elimu zaidi kwa umma kwa kuwa huduma hiyo ni nzuri lakini bado haitambuliki na watu wengi.
  • Huduma hii huenda ikaondoa kabisa haja ya mtu kutembea na fedha kwani huduma nyingi muhimu zimefikiwa nayo. Maduka makubwa, sheli na hata migahawa.

Dar es Salaam. Kwa kila mtanzania anayefanya manunuzi kwa kutumia teknolojia ya simu janja, neno “QR code” sio kitu kigeni kwa kuwa limekuwa likisika kila kukicha. 

Kampuni nyingi zimekuwa zikitumia neno hilo katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia mpya ya kufanya malipo baada ya kununua bidhaa au huduma. 

Mfumo huo wa malipo unafanya kazi kwa kutumia kamera ya simu janja ambayo ina skani msimbo (CODE) na kisha kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi.

Ili kuendeleza ushindani, kampuni kubwa duniani na nyumbani zinazotoa huduma ya kufanikisha malipo zimejitahidi kubuni njia mbadala ili kutoa huduma bora lakini kubaki katika soko kutokana na kukua kwa teknolojia.

Katika ubunifu huo, kampuni hizo zimekuwa zikishirikiana na taasisi za huduma za kifedha kama benki na kampuni za simu zinazotoa huduma za kifedha ili kufanikisha miamala ya manunuzi kupitia teknolojia hiyo ya kulipa kwa QR Code. 

Hivi karibuni kampuni ya kimataifa ya Visa yenye makao makuu yake nchini Marekani inayojihusisha na huduma za kifedha ilizindua huduma ya kuskani QR Code hapa nchini Machi 12, 2019 ili kurahisisha malipo ya huduma na bidhaa mbalimbali.

Visa imeungana na taasisi 15 zinazotoa huduma za kifedha zikiwemo benki za CRDB, NBC, NMB, na kampuni ya  simu ya Halotel kumpa mteja mawanda mapana zaidi ya kuchagua namna ya kulipa. Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana katika sheli na maduka ya jumla ya watoa huduma zaidi ya 2,000.

Mteja anaweza kuskani QR Code kwa kutumia simu janja na kulipia bidhaa na huduma kirahisi |Picha na Rodgers George

Kuna teknolojia nyingi za malipo zinaendelea kubuniwa duniani, je mfumo huu wa malipo wa QR Code una maana gani kwa wateja na watoa huduma?

Wafanyabiashara ambao sio tu wametumia mfumo huo wa Visa bali hata mingine ambayo ilikuwepo awali wamesema mfumo mpya wa kampuni hiyo una kasi kuliko njia ya kadi na hata ile ya kulipa kwa waleti za mitandao ya simu.

Meneja Mkuu wa maduka ya Shoppers, Mahesh Venkatesh amesema imepunguza foleni ya malipo kwa wateja wake wanaotumia malipo ya kadi kwa kuwa ilikuwa inachukua muda mrefu kukamilisha malipo ya mtu mmoja hapo awali.

 “Kama mtu mmoja anakaa kwenye foleni kwa dakika 5, inaweza kusababisha mtu kuahirisha kufanya manunuzi kama ana haraka lakini kwa mfumo huu wa QR Code mtu analipa kwa dakika 2 tu. Inarahisisha uharaka wa kutoa huduma na zaidi inaongeza mauzo,” amesema Venkatesh.

Mbali na kupunguza foleni, watumiaji wa mfumo huu wanaeleza kuwa unaondoa usumbufu wa kutafuta chenji ambayo mara kadhaa husababisha baadhi ya wauzaji wasio wavumilivu kuahirisha mauzo.

“Zamani mteja alikua anakuja na pesa inayohitaji chenji na nikikosa chenji inanilazimu kuahirisha mauzo,” amesema Neema Charles ambaye ni msimamizi wa duka la nguo la Jaim lililopo Sinza.

Maduka mengi jijini Dar es Salaam sasa yamefikiwa na huduma ya QR ya kampuni ya Visa kuwarahisishia wateja wao kufanya malipo ya bidhaa. Picha|Rodgers George.

Sambamba na hayo, miaka ya zamani kulikua na matukio mengi ya uvamizi kwenye maduka au sheli mbalimbali jijini Dar es salaam na uvamizi huo ulilenga kupora pesa kwenye vituo vya mafuta. Kupitia mfumo wa QR, wafanyabiashara wa sheli wamesema utasaidia kuondoa tatizo hilo.

“Inaondoa changamoto za usafirishaji wa fedha baada ya mauzo ya siku nzima kwa sababu baada ya malipo pesa inaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya mtoa huduma. Pia inaondoa uwezekano wa kuibiwa kwa sababu ya kutembea na maburungutu ya pesa,” amesema Mohamed Omar Meneja wa kituo cha mafuta cha Puma, Upanga jijini Dar es Salaam. 


Soma zaidi: Vodacom, Mastercard zaangazia biashara kupitia Virtual Card


Pamoja na uzuri wa teknolojia hiyo bado elimu haijawafikia watu wengi katika kubadilisha mfumo wa malipo kutoka kwenye fedha taslimu kwenda kwenye malipo mtandao. 

Baadhi ya Watanzania ambao wameweza kutumia huduma hiyo wameziomba kampuni kama Visa na Mastercard kutoa elimu zaidi kwa umma kwa kuwa huduma hiyo ni nzuri lakini bado haitambuliki na watu wengi.

“Asilimia kubwa ya watanzania hawatumii huduma ya kadi wakijua njia za kulipia huduma kwa simu zinarahisisha malipo. Elimu itolewe kwani huduma hii ni nzuri,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha mafuta cha Engen cha Mikocheni, Paul Muhato.

Baadhi ya  huduma za aina hii mara nyingi huwa kuna makato pale mteja anapolipia huduma yoyote kwa kulingana na kiasi anacho kitumia. 

Mwandishi alijaribu mara tatu kununua bidhaa kupitia mfumo wa malipo ya QR Code chini ya Visa na kubaini kuwa hakuwa amekatwa kutokana na miamala aliyokuwa amefanya katika kununua bidhaa hizo. 

Pamoja na uzuri wa teknolojia hiyo bado elimu haijawafikia watu wengi katika kubadilisha mfumo wa malipo kutoka kwenye fedha taslimu kwenda kwenye malipo mtandao. Picha| Rodgers Raphael.

Hata hivyo, huduma ya malipo  haimkati mteja tozo ya malipo jambo ambalo limeacha maswali ni namna gani kampuni hiyo inanufaika na huduma hii.

Kupitia mfumo huo hakuna haja tena ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda kwenye akaunti za mitandao ya simu ili kufanya malipo. Mteja atalipa moja kwa moja bila makato kutoka benki au mtandao wake wa simu kama Tigo Pesa au M-Pesa bila uwepo wa dalali. 

“Ukilipa shilingi elfu tano, ni elfu tano tuu itakayokatwa. Hakuna ada ya malipo anayotozwa mteja,” amesema Meneja wa Visa ukanda wa Afrika Mashariki, Kevin Langley.

Huduma hii huenda ikaondoa kabisa haja ya mtu kutembea na fedha kwani huduma nyingi muhimu zimefikiwa nayo. Maduka makubwa, sheli na hata migahawa.

Kupitia malipo ya QR, muuzaji anauwezo wa kuongeza mauzo na hata kupata wateja ambao ni waaminifu kwani imetoa uwanda mpana zaidi wa kulipia manunuzi na huduma. 

Msimamizi wa mgahawa wa Samaki Samaki, Saum Wengert amesema mfumo huu umewezesha wateja kutumia pesa zaidi kwani anaamini mteja hutumia pesa nyingi anapolipa kwa kutumia benki na sio kwa fedha taslimu.

Enable Notifications OK No thanks