Mfahamu Fatma Karume mwanamke aliyeshika kiganja cha historia ya Zanzibar 

September 22, 2026 2:25 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  •  Alikuwa ‘first lady’ wa kwanza, na mama wa Rais wa 6 wa Zanzibar, Amani Abeid Karume
  • Ameondoka duniani akiwa na miaka 97.

Dar es Salaam. Mama Fatma Karume, mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, amefariki dunia Jumatatu, Septemba 21, 2026, akiwa na umri wa miaka 97.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametangaza taarifa za msiba huo usiku wa kuamkia leo Septemba 22, 2026 akieleza kuwa Mama Fatma alifariki dunia akiwa Mbweni, Zanzibar.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Mama Fatma alikuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hususan katika harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema Taifa litaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wake katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wa Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Lakini swali kubwa kwenye masikio ya watu wengi hasa vizazi vilivyozaliwa baada ya historia ya mapinduzi ni mama Fatma Karume ni nani hasa licha ya kuwa mke wa Rais na mama wa Rais wa 6 wa Zanzibar, Amani Abeid Karume?

Mama Fatma, ambaye jina lake kamili ni Fatma Gullam Hussein Jamal, alizaliwa Februari 2,1929 Bumbwini Misufini, Kaskazini Unguja.  

Katika kumbukumbu zake za mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari mwaka 2023, alieleza kuwa alikulia katika mazingira ambayo watoto wa jamii tofauti waliingiliana na kukua pamoja. 

Baba yake Gullam Hussein Jamal alikuwa akiishi maisha ya mjini na familia yake mizizi Bumbwini.

Elimu yake haikuwa ndefu kwa viwango vya leo. Mama Fatma alipata elimu ya msingi Bumbwini, na baadaye kwa mujibu wake mwenyewe sehemu ya elimu yake iliendelea kupitia kujifunza nyumbani. 

Ndoa iliyomuingiza katikati ya historia 

Mwaka 1944, akiwa na umri wa miaka 15, Fatma aliolewa na Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar.

Katika mahojiano yake aliyoyafanya na Crown media aliezeza kuwa mara ya kwanza kuonana na Abeid Amani Karume ilikuwa Dumbwini Zanzibar. 

Wakati huo kulikuwa na ubaguzi mkubwa wa rangi jambo lililomfanya Hayati Karume kupata tabu sana kumpata mrembo huyo mwenye asili ya kihindi.

 Mama Fatma alisema licha ya ubaguzi huo baba yao aliridhia yeye kuolewa na harusi yao ikafanyika Bumbwini Misufini, na baada ya ndoa wakaishi mjini Unguja.

Ndoa ya Fatma na Karume ilijenga familia ambayo baadaye iliendelea kuwa sehemu ya historia ya Zanzibar.

Mtoto wao wa kwanza wa kike, Asha, alifariki siku ya pili baada ya kuzaliwa mwaka 1946.

Miaka miwili baadaye, Novemba 1,1948, wakapata mtoto wa kiume, ambaye ni Amani Abeid Karume huku mwaka 1950, wakipata mtoto mwingine, Ali Abeid Karume.

Amani akaja kuwa Rais wa Zanzibar kati ya mwaka 2000 na 2010 huku Ali akiingia katika utumishi wa kidiplomasia. 

Hivyo, hata maisha yake ya nyumbani yalikuwa yamezungukwa na matukio ambayo baadaye yakawa sehemu ya historia ya Zanzibar.

Kabla ya kuwa ‘First Lady’

Hapa ndipo simulizi ya Mama Fatma inabadilika.

Kwa mujibu wa mahojiano yake na Daily News yaliyochapishwa Oktoba 30, 2023 Mama Fatma alijiunga na kundi la wanawake lililokuwa likishiriki katika harakati za kudai uhuru, akiwa karani wa kundi hilo wakati akiwa bado binti mdogo.

Miongoni mwa mambo aliyoyakumbuka kwa msisitizo ni harakati za wanawake kudai haki ya kupiga kura yaliyochochewa na fursa ya ujio wa ujumbe kutoka Lancaster House, London, kuwasilisha madai yao. 

Lakini mada hiyo ilikuwa ngumu kuliko inavyoweza kusikika leo.

Kwa simulizi yake, hata baada ya wanawake kupata mwanya wa kushiriki katika uchaguzi, kulikuwa na masharti yaliyofanya zoezi hilo kuwa gumu, miongoni mwa masharti aliyoyataja ni uwezo wa kusoma na kuandika pamoja na kuwa na shilingi tatu.

Mama Fatma alisisitiza kwamba shilingi hizo tatu zilikuwa fedha nyingi sana kwa wakati huo. Kwa kulinganisha, alisema hata mshahara wa mwezi wa mumewe, Karume, ulikuwa shilingi tatu.

Wanawake, kwa mujibu wa simulizi yake, wakatafuta njia ya kukabiliana na kikwazo hicho.

Kwa msaada wa mashine za kushonea na vitambaa kutoka mataifa rafiki, ikiwemo China, waliunda shughuli za kushona na upishi ili kuonyesha uwezo wa kiuchumi na kuwasaidia wanawake kukidhi masharti ya usajili wa wapiga kura.

Na hapo Mama Fatma akaweka wazi jambo alilotaka historia ikumbuke ya kuwa Wanawake hawakuwa kwenye harakati kwa ajili ya kuwahudumia waume zao pekee, walikuwa sehemu ya siasa hai.

Siku ambayo Zanzibar ilibadilika

Kisha likaja tukio ambalo lingemweka Mama Fatma moja kwa moja ndani ya historia, Januari 12,1964 , Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea.

Abeid Amani Karume akawa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

Miezi michache baadaye, Zanzibar iliungana na Tanganyika Aprili 26, 1964, na kuundwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania huku Karume akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri hiyo.

Na Mama Fatma, katika mahojiano yake mwenyewe, alieleza kuwa alikuwa mshiriki wa moja kwa moja wa Mapinduzi hayo. 

Pia alisema kila mwaka alihakikisha anakuwa Zanzibar wakati wa maadhimisho ya mapiinduzi hayo yanayofanyika Januari 12 kila mwaka  kwa sababu yalikuwa sehemu ya kumbukumbu zake za ndani kabisa.

‘First wa lady wa kwanza’

Baada ya Mapinduzi, Mama Fatma akawa Mama wa Kwanza wa Zanzibar, nafasi aliyoshikilia wakati Abeid Karume akiwa Rais kuanzia 1964 hadi 1972.

Lakini utafiti wa mwanahistoria Jessica Ott, uliochapishwa katika jarida la International Journal of African Historical Studies mwaka 2024, unaonyesha kwamba nafasi yake ilikuwa kubwa zaidi kuliko taswira ya kawaida ya mke wa kiongozi.

Alikuwa mlezi wa Umoja wa Akina Mama wa Afro-Shirazi Party, Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), na alitembelea Unguja na Pemba kuwahamasisha wanawake kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa zilizokuwa zikionekana zaidi kuwa za wanaume.

Kwa hiyo, wakati Karume akijenga taasisi za Serikali ya Mapinduzi, Mama Fatma alikuwa pia akitumia nafasi yake kuhamasisha wanawake kuingia katika maisha ya kijamii na kisiasa.

Kwa Mama Fatma, nafasi hiyo ilikuwa na mamlaka ya kijamii, kisiasa na hata kidiplomasia.

Mwaka mmoja baada ya Mapinduzi, historia yake ilivuka Bahari ya Hindi.

Utafiti wa kitaaluma uliochapishwa mwaka 2025 kuhusu safari za wanawake wa Tanzania kwenda China unathibitisha kwamba Mama Fatma Karume alitembelea China mwaka 1965.

Katika safari hiyo, mkalimani wa Kiswahili Shen Zhiying alihudumu katika mawasiliano ya Mama Fatma na wenyeji wa China.

Safari hiyo inaonyesha namna Mama Fatma alivyokuwa sehemu ya mazingira mapana ya diplomasia ya wakati huo, wakati Zanzibar na Tanzania zikiingia katika uhusiano mpya na mataifa mbalimbali ya dunia.

Mwaka 1966, alionekana pamoja na Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ufunguzi wa Kituo cha kulea Wazee cha Sebuleni, Zanzibar.

Kwa hiyo, urithi wake wa miaka hiyo haukuwa kwenye majukwaa ya kisiasa pekee. Pia alikuwa akionekana katika shughuli za kijamii zilizohusiana na ujenzi wa huduma za taifa jipya

Kifo cha Karume 

Siku iliyokuwa na maumivu makubwa ya kumpoteza mume, rafikina ndio siku liyobadlisha kila kitu.

Aprili 7, 1972, Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa bado Rais wa Zanzibar. Kwa Mama Fatma, hilo halikuwa tu tukio la kitaifa.

Lilikuwa ni tukio la kumpoteza mume wake, baada ya miaka 28 ya ndoa na miaka minane ya kuishi katika kilele cha uongozi wa Zanzibar. Kutoka hapo, maisha yake yaliingia katika sura mpya.

Lakini utafiti wa Jessica Ott unaonyesha kwamba baada ya kifo cha Karume, nafasi yake ya kisiasa nayo ilibadilika. 

Zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuuawa kwa Abeid Amani Karume , Mama Fatma aliondolewa katika uongozi wa UWZ. Miaka iliyofuata ushawishi wake uliendelea kupungua ndani ya siasa za Zanzibar.

ALiyekuwa Makamu wa Rais kabla ya kujiuzulu Emmanuel Nchimbi akimtakia kheri ya kumbukizi Mama Fatma Karume alipotimiza miaka 93. Picha| Global Publisher

Karne ilipobadilika, jina la Karume likarudi tena kileleni mwa siasa za Zanzibar.

Mwaka 2000, mtoto wake Amani Abeid Karume alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na baadaye akaongoza hadi mwaka 2010.

Hivyo Mama Fatma alikuwa ameishi kuona mambo mawili ambayo si ya kawaida katika historia ya kisiasa, kwanza alikuwa mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar na baadaye mama wa Rais mwingine wa Zanzibar.

Utafiti wa Ott unaeleza kwamba uchaguzi wa Amani mwaka 2000 uliambatana pia na kurejea kwa Mama Fatma katika nafasi ya kutambulika zaidi kama mama wa taifa, baada ya kipindi kirefu cha kutokuwa na nafasi yake ya awali ya kisiasa

Mwisho wa safari, mwanzo wa kumbukumbu

Mwaka 2026, Mama Fatma aliendelea kuonekana katika kumbukumbu za taifa.

 Aprili 7, 2026 , alishiriki katika dua ya kumuombea Hayati Abeid Amani Karume katika kumbukumbu ya miaka 54 tangu kifo chake.

Miezi mitano baadaye, Septemba 21, 2026, safari yake ikafika mwisho.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeeleza kwamba atabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hasa katika kipindi cha kabla na baada ya Mapinduzi. 

Na pengine hapo ndipo swali linapojibiwa, Mama Fatma Karume alikuwa nani?

Hakuwa tu mwanamke aliyesimama pembeni ya Rais. Alikuwa mmoja wa wanawake waliokuwa ndani ya safari yenyewe, kabla ya Mapinduzi, wakati wa Mapinduzi, na katika kizazi kilichokuja baada yake.

Na sasa, akiwa ameondoka duniani akiwa na miaka 97, kinachobaki si jina pekee.

Kinachobaki ni sauti ya mwanamke aliyeshuhudia historia, akaishi ndani yake, na akaondoka akiwa ameibeba sehemu yake katika kumbukumbu zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
22 Sep, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
22 Sep, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
22 Sep, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MAMA FATMA KARUME: Sikuolewa na Rais, niliolewa na kiongozi

MAMA FATMA KARUME: Sikuolewa na Rais, niliolewa na kiongozi

Nukta TV

Mama Fatma Karume, kuzikwa leo Septemba 22, 2026 saa 10 alasiri

Mama Fatma Karume, kuzikwa leo Septemba 22, 2026 saa 10 alasiri

Nukta TV

HUU HAPA mwenendo wa ujenzi wa Mradi wa Gesi Asilia Kimiminika (LNG) Lindi

HUU HAPA mwenendo wa ujenzi wa Mradi wa Gesi Asilia Kimiminika (LNG) Lindi

Nukta TV