Mfahamu bosi mpya wa Vodacom Tanzania
Sitholizwe Mdlalose, Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni ya Vodacom Tanzania. Picha| Tech Financials.
- Ni Sitholizwe Mdlalose ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji.
- Anachukua nafasii iliyoachwa na Hisham Hendi.
- Mdlalose alijiunga na kampuni hiyo nchini Afrika Kusini mwaka 2017.
Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania imemteua Sitholizwe Mdlalose kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo akichukua nafasi iliyoachwa na Hisham Hendi aliyemaliza muda wake.
Hendi alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mapema mwezi huu na Novemba Mosi, 2021 itakuwa siku yake ya mwisho baada ya kuitumikia kampuni hiyo kwa miaka mitano.
Mdlalose, kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya juu ya utendaji alikuwa mkurugenzi mtendaji wa fedha wa kampuni hiyo nchini Afrika Kusini
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania, Jaji mstaafu Thomas Mihayo katika taarifa iliyotolewa leo Agosti 25, 2021 amesema Mdlalose alijiunga na Vodacom ya nchini Afrika Kusini mwaka 2017 kama mkurugenzi wa fedha.
Wakati wote aliokuwepo ndani ya kampuni hiyo ya mawasiliano inayokuwa kwa kasi Afrika ameshikilia nafasi mbalimbali za utendaji ikiwemo afisa mkuu wa fedha wa biashara ya kimataifa.
“Kabla ya kujiunga na kampuni dada ya Vodacom, alikuwa akifanya kazi na kampouni ya Vodafone kwa zaidi ya miaka sita akishikili nafasi za juu ndani ya kampuni hiyo,” amesema Jaji Mihayo.
Mdlalose ambaye ni raia wa Afrika Kusini ana uzoefu wa miaka 19 katika tasnia ya fedha, utawala na ushauri ambapo kwa miaka 13 amekuwa katika sekta ya mawasiliano pepe katika masoko yanayoibukia na yanayoendelea.
Kwa mujibu wa Jaji Mihayo, bosi huyo mpya wa Vodacom Tanzania ana Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Uhasibu (BCompt) kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.
pia ni mhasibu aliyehitimu (ACCA) na amekamilisha programu ya mtendaji mwandamizi ya Afrika katika shule ya biashara ya Chuo Kikuu cha Harvard.
Anatajwa kuwa kiongozi wa biashara aliye imara, mwenye upeo mkubwa na uwezo wa kuongoza katika mashirika ulimwenguni, hivyo anatazamiwa kuwa chachu ya mabadiliko na maarifa mapya ndani ya Vodacom Tanzania.
“Ana rekodi ya kipekee ya biashara zinazokua na kutoa mabadiliko ya kimkakati, hivyo uteuzi wake unaonyesha azma ya Bodi ya Vodacom Tanzania katika kukuza msimamo wetu na kuendelea kutekeleza kusudi la Vodacom la kuungana na maisha bora ya baadaye,” amesema Jaji Mihayo katika taarifa yake.
Mdlalose atakuwa na kibarua kigumu cha kuendeleza kazi nzuri aliyofanya Hendi ambaye anakwenda kuwa mkuu wa biashara wa Vodafone nchini Hispania baada ya kuitumikia na kuikuza kampuni hiyo ya mawasiliano Tanzania.
Hendi ambaye ni raia wa Misri amekuwa ni msukumaji mkuu katika kufanikisha uwekezaji wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania ambao awali hawakufikiwa na hawajaunganishwa huduma za simu.
Latest
