Mbunifu anayebadili betri za kompyuta kuwa ‘power bank’, taa za umemejua -2

September 17, 2022 9:43 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ubunifu wake uko katika hatua za majaribio, kipato siyo kikubwa.
  • Ukosefu wa mtaji ni changamoto inayopunguza kasi ya ukuaji wake.
  • Ana ndoto ya kumiliki mji unaotumia nishati ya betri.

Dar es Salaam. Leo tunaendelea na makala kuhusu ubunifu wa kijana Gibson Kawago ambaye anabadilisha betri za kompyuta kuwa taa za umemejua na vitunza umeme kwa ajili ya kuchajia simu au kupata mwanga nyumbani. 

Ubunifu unalipa

Licha ya kwamba bidhaa hizo hazijaingia sokoni rasmi tayari Gibson ameanza kuona matunda ya ubunifu wake kwani kwa sasa jamii inayomzunguka inafurahia ubunifu wa vitunza umeme pale umeme wa  kawaida unapokatika ua kuisha.

Uwepo wa vitunza umeme vyenye uwezo wa kuwasha nyumba nzima hufanya nyumba kuangaza wakati mtaa  mzima anaoishi kijana huyo upo kwenye giza.

Sambamba na hilo hujiingizia kipato kwa kazi ndogo ndogo anazozifanya ikiwemo kufanya marekebisho ya mabetri ya vifaa vya umeme kama redio. 

Ameanza kuzifanyia majaribio bidhaa hizo kwa wateja wake wa awali ambao hupendelea ubunifu anaoufanya kabla hata ya bidhaa hizo hazijarasimishwa.

Gibson ametengeneza ajira kwa vijana na wanawake wengine ambao anashirikiana nao kwenye ukusanyaji, uvunjaji na utafiti wa betri kabla hajazitumia kwenye ubunifu wake.

“Jumla ya ajira nilizozitengeneza mpaka sasa ni zaidi ya 32 zinazohusisha vijana na kina mama ambao wanaokota betri, bodaboda, wanaovunja vunja betri na kusaidia kwenye kutengeneza mifumo,” anasema Kawago.


Soma zaidi:


Ndoto ya ‘Mji wa Waga’

Akaunti za mitandao ya kijamii anazomiliki kijana huyu utayakuta maneno haya ‘The City of Waga’ yenye tafsiri rahisi ya kiswahili kama ‘Mji wa Waga’.

Ndoto hii ni ya kutengeneza mji ambao ndani yake utakuwa na vifaa vinavyotumia mabetri, magari yanayotumia mabetri, na vifaa vyote ambavyo kwa sasa vinatumia teknolojia isiyo rafiki inayochafua mazingira.

“Siku moja natamani kutengeneza magari yenye kutumia mabetri ambayo yatakuwa yanapita vituo vya kuyachaji kama ilivyo sasa hivi yanavyoenda kujaziwa mafuta,” anasema Gibson.

Katika mji huo waga anasema kutakua na mifumo rafiki ya majumbani ambayo haitazalisha hewa ya ukaa ambayo kwa sasa inachafua mazigira.

Hatua kwa hatua uchakataji wa mabetri ya Kompyuta mpakato kupata seli ndogo zinazotumika kubuni vitunza umeme na  taa za umemejua.Picha|Gibson Kawago/Instagram.

Kibarua alichonacho

Licha ya kuwa na ujuzi wa kutosha kutengeneza bidhaa hizo zitakazoikomboa jamii maskini kutoka kwenye giza, mtaji wa kuimarisha biashara yake imebaki kuwa changamoto kwa Gibson.

“Ukuaji wangu unahitaji fedha kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuziweka bidhaa ziwe kwenye mfumo wa kimasoko zaidi,” anasema.

Ili kupata fedha ya kuwalipa wasaidizi na kununua vifaa vya utengenezaji wa bidhaa hizo Gibson hulazimika kufanya kazi nyingine za ziada ambapo hutumia kipato chake hicho kusapoti ubunifu wake.

Mbali na kuwa mhandisi wa umeme Gibson pia ni mzalishaji wa midundo (beats) ambazo huziuza mtandaoni.

Vijana msiwe ‘lele mama’

“Unakuta kijana wa sasa hivi amekaa hana shughuli ya kufanya wakati ana simu janja, kijana angalia nchi nyingine walifanyaje kutatua changamoto kama unazoziona kwenye jamii yako na wewe iga ufanye utajipatia ajira” amesema Gibson ikiwa ni ushauri kwa vijana wa Tanzania.

Pia amewashauri vijana kuwa wadadisi na jicho la kuona fursa ambazo nyingi zimejificha kwenye changamoto za jamii.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW