Mbunifu anayebadili betri za kompyuta kuwa ‘power bank’, taa za umemejua

September 16, 2022 1:28 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Gibson Kawago, mhitimu wa chuo kikuu aliyebadili changamoto ya ukosefu wa umeme kijijini kuwa fursa.
  • Anawasaidia watu kupata mwanga, kuchaji simu maeneo yasiyo na gridi ya Taifa. 
  • Amekuwa miongoni mwa wadau wa kutunza mazingira.

Dar es Salaam. Kompyuta mpakato (laptops) ni teknolojia pedwa zaidi ulimwenguni tangu kugunduliwa kwake karne ya 20.

Imekuwa kifaa muhimu kwa shughuli zinazofanyika mtandaoni ikiwemo biashara, elimu na hata burudani.

Swali la kujiuliza ni kuwa kompyuta hizi zikiharibika zinatupwa wapi? Na endapo zikitupwa hovyo ni athari zipi zitatokea kwenye mazingira?

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kufikia mwaka 2025 miji mingi duniani itazalisha  tani 2.2 bilioni za uchafu unaothari afya za watu na mazingira.

Hata hivyo, athari hizo zinaweza kupungua kwa kurejeleza taka za kielektroniki ikiwemo mabetri  yapatikayo kwenye kompyuta mpakato na  kutumika kutengeneza bidhaa nyingine zisizo na athari kwenye mazingira.

Gibson Kawago ni kijana aliyemua kupunguza athari hizi za mazingira  zitokanazo na mabetri ya kompyuta mpakato kwa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo  vitunza umeme (power bank), taa za umemejua na vitunza betri (battery pack).

“Mchakato mzima tunaoufanya unaokoa kusambaa kwa carbon (hewa ya ukaa) ambazo zingesambazwa kama watu wasingetumia nishati mbadala,” anasema Gibson.

Kijana huyo ambaye ni mhandisi wa umeme kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) alipata wazo la kutunza mazingira kwa kuzirejeleza betri mwaka 2019 alipokuwa mwaka wa kwanza chuoni akitokea mkoani Iringa.

“Wakati nimekuja Dar nikaona chuo wote tuna laptop (kompyuta mpakato) na betri zinakufa kila siku lakini hizi betri zinatupwa hovyo nikaangangalia jinsi gani naweza kuzitumia tena na kubuni power bank zangu,” anasema Gibson.

Mabetri ya kompyuta yakiwa tayari kwa ajili ya mchakato wa kuvunjwa vujwa ili kupata seli ndogo zinazotumika kutengeneza vitunza umeme na taa za umemejua. Picha|Gibson Kawago/ Instagram.

Kwanini mabetri ya kompyuta?

Akiwa katikati ya kundi la watu Gibson hakusita kunihadithia jinsi ukosefu wa umeme kijijini kwao ulimsukuma kubuni njia mbadala za kupunguza tatizo hilo na kuhakikisha watu wanapata nishati ya umeme mbadala.

Kijiji alichokulia Gibson, hakijapitiwa na umeme wa gridi hivyo hutumia taa zinazotumia mafuta ya taa na iliwalazimu wakazi wake kukusanya simu za kijiji kizima na kumpa mtu mmoja apeleke kuchaji ng’ambo ya pili ambapo huchukua hadi masaa 12 kujaa.

Hali hiyo imemuachia kumbukumbu ya kusikitisha Gibson kwani bibi yake alifariki dunia kabla hajaona video ya harusi kwenye simu yake siku alipowasili kijiji kwa sababu ilikuwa imezima kwa kukosa chaji.

Huu ndiyo ukawa mwanzo wa kutafuta suluhu ya tatizo la umeme kijijini kwao. 

“Tangu hapo nikaona kwamba kwanini tusipate kitu kitakachotusaidia sisi kuchaji, kwahiyo nilivyofika chuo nikaanza kufanya utafiti nikagundua kuwa nina uwezo wa kutengeneza vifaa hivi,” anasema Gibson.

Taratibu ndoto ya Gibson  ikachanua  kwa kuanza kutengeneza vitunza umeme vidogo vyenye uwezo wa kuchaji simu mara moja, mpaka sasa tayari ana vifaa kamili vyenye uwezo mkubwa.

Ni miaka mitatu sasa tangu aanze ubunifu huu na sasa ana uwezo wa kutengeneza aina mbalimbali za vitunza umeme, vinavyoweza kuwasha nyumba nzima kama umeme ukikatika.


Soma zaidi:


Hatua kwa hatua utengenezaji wa vitunza umeme

“Mchakato unaanza kwa kukusanya betri za laptop ambazo zinakuwa zimetupwa au naenda kwa mafundi wa laptop ambao huwa wananikusanyia,” anasema Gibson.

Baada ya mabetri hayo aina ya lithium kukusanywa huvunjwa vunjwa ili kupata seli ndogo ndogo.

Seli hizo zilizovunjwa hupitia mchakato wa kuzipa nguvu mpya na kuziunganisha kwa pamoja kwa ajili ya kutengeneza bidhaa tofauti tofauti kama vitunza umeme, betrii kubwa zenye uwezo wa kutoa mwanga nyumba nzima.

Gibson mwenye uwezo wa kukusanya betri 100 kwa siku hutengeneza bidhaa zinazotumia teknolojia ya “lithium ion batteries” zenye uwezo wa kukusanywa kwenye eneo dogo, hivyo ni rahisi kwake kubuni bidhaa zenye ubora na rahisi kubebeka.

“Mbali na teknolojia hiyo natumia teknolojia ya ICT ambayo ni mfumo ambao nimeuprogramu mwenyewe na michoro mabayo nimeizalisha ili iweze kusaidia utumiaji wa hizi betri na kutoa nguvu ambao unahitajika” anasema Gibson.

Gibson ni miongoni mwa wabunifu nchini Tanzania ambao wanatoa suluhu ya matatizo katika sekta ya nishati. Picha| Gibson Kawago.

Usalama wa bidhaa hizo upoje

Ni jambo lilizoeleka kwa jamii kuwa na hofu juu ya usalama wa bidhaa yoyote wanayoinunua hususani bidhaa za umeme, kwa bidhaa za Gibson usalama ni kipaumbele kuanzia ukusanyaji mpaka inaaenda kwa mteja.

“Kwenye utengenezaji huwa najaribu usalama nimeshajaribu kuziweka kwenye maji, kuziangusha na kuziweka kwenye joto kubwa kwa hiyo najua inajibu vipi na mabadiliko yaliyotokea nimeyarekebisha kabla ya kumfikia mtumiaji,” anasema Gibson.

Bidhaa hizo zimetengenezwa kwa tekolojia inayoweza kihisi na  kupunguza madhara wakati wa janga lolote la kimifumo au moto litakapotokea hivyo kuhakikisha usalama kwa watumiaji wanapotumia bidhaa hizi.

“Wengi wanahofia kwamba hii mifumo inaweza kuungua inapotokea moto, nina mifumo inayoweza kugundua na kukiwa na dalili ya moto yenyewe inajizima,” anasema Gibson.

Suala la usalama pia linazngatiwa wakati wa ukusanyaji wa mabetri haya ambapo mtaalamu huyo hutoa elimu kwa wasaidizi wake wanaomsaidia kuzikusanya kuzivunja na kuzifanyia utafiti betri hizo kabla ya kuendelea na ubunifu wa bidhaa husika.

Bidhaa hizo zinamlipa? Masoko yake yako wapi? Anafanya nini kuboresha teknolojia ya utengenezaji vifaa hivyo? Tukutane katika sehemu ya pili ya makala haya tukiangazia ugunduzi wa Gibson.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV