Mbunge aiponza Manispaa ya Temeke, Serikali yakaa kuilipia mkopo wa Sh12.9 bilioni
- Ni sehemu ya Sh19 bilioni za mkopo iliyokopa benki ya CRDB.
- Ilitumia fedha hizo kulipa fidia kwa watu ambao maeneo yalichukuliwa ili kujenga shule, zahanati na barabara.
- Serikali yasema haitalipa fedha hizo kwa sababu haihusiki.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali haitalipa Sh12.9 bilioni ambazo ni sehemu ya mkopo wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaodaiwa na benki ya CRDB ilizokopa kwa ajili ya kulipa fidia kwa watu ambao maeneo yao yalichukuliwa ili kujenga miundombinu ya shule, zahanati na barabara miaka ya nyuma.
Licha ya kukataa, Rais ameagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru) kufanya uchunguzi wa kina juu ya matumizi ya fedha za mkopo huo maana kuna harufu ya ufisadi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Temeke, Doroth Kilave kumuomba Dk Magufuli aisaidie manispaa hiyo kulipa kiasi hicho fedha kilichobaki kati ya Sh19 bilioni ilizokopa katika benki hiyo ya biashara.
“Sisi kama Halmashauri ya Temeke miaka ya nyuma tulikopa toka (Sh19 bilioni) CRDB kwa ajili ya kulipa mafao ya wale ambao tunakwenda kubomoa sehemu zao ya kujenga maendeleo yale ambayo tumepewa DMP (mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam).
“Deni lile limekuwa kubwa kwetu, tumeweza kulipa kwa awamu na tunalipa kila mwaka Sh4.8 bilioni kutokana na makusanyo yetu ya ndani. Tunalipa kwa awamu nne. Deni hili limekuwa changamoto Mheshimiwa Rais naomba ulipokee,” amesema Mbunge huyo mbele ya Rais leo Februari 26, 2020 wakati wa uzinduzi wa majengo ya Chuo Cha Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, ikawa tofauti na matarajio ya Mbunge huyo, baada ya Dk Magufuli kusema Serikali haiwezi ikalipa deni la mkopo ambao haikuhusika wala haijui masharti yake.
“Mbunge wa Temeke anataka Serikali ikalipe Sh4 bilioni kwa mkopo ambao Serikali haikuhusika. Unajua ni mambo ya ajabu sana. Nyinyi Manispaa mmekaa mkaenda kuzungumza na CRDB, mazungumzo yale hayajulikani mlikuwa mnazungumza nini.
“Inawezekana mazungumzo yalikuwa ya kificho, labda kuwa asilimia, mmeshindwa kulipa manataka Serikali ilipe hilo deni? Hiyo msahau, deni mtalibeba wenyewe,” amesisitiza Rais.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema kitendo hicho kilichofanywa na Temeke kukopa fedha katika benki ya biashara ili kulipa fidia ni kukosa nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali.
Soma zaidi:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
- Kigamboni, Temeke kutumia mfumo wa kielektroniki utoaji hatimiliki ardhi kuanzia Julai 1
Badala yake, ameiagiza Takukuru ichunguze fedha zilivyotumika ili kubaini kama kuna viashiria vya ufisadi ili wahusika wachukuliwe hatua.
“Hakuna hela itakayotolewa na Serikali, sana sana itachunguza hizo fedha zilikwenda wapi na kamanda wa Takakukuru naomba ufuatilie hilo wamenisaidia kujieleza hapa ili tujue hiyo hela nani alikwenda kufanya majadiliano na CRDB? Je maeneo hayo yalikuwa ya nani? Je hizo fedha zilizokuwa zinalipwa ndiyo zilikuwa zinastahili?,” amehoji Rais wakati akitoa maagizo ya kufanyika kwa uchunguzi.
Kutokana na suala hilo, Rais ameihirisha mpango wake wa kuipatia manispa hiyo eneo la Wakala wa Barabara Tanzania (TBA) ambalo iliomba kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Rais Magufuli amehitimisha ziara yake ya siku tatu jiji hapa aliyoanza Februari 25 ambayo ililenga kutembelea na kuzindua miradi ya maendeleo ikiwemo daraja la juu la Ubungo, stendi mpya ya mabasi ya mikoani ya Mbezi Luis, soko la Kisutu na majengo ya Chuo cha Polisi Kurasini.
Latest