Matumizi ya SMS yapungua kwa asilimia 3 Tanzania
- Yafikia bilioni 47.6 kutoka bilioni 50.8 iliyorekodiwa kipindi cha robo ya mwaka inayoishia Juni, 2024.
Arusha. Huenda ongezeko la nyanja za mawasiliano na majukwa ya huduma za ujumbe wa papo hapo kama WhatsApp, Facebook Messenger, na Telegram yakaathiri njia za mawasiliano za zamani ikiwemo ujumbe mfupi (SMS) mara baada ya takwimu kuripoti kupungua kwa matumizi ya sms kwa asilimia tatu.
Kwa muda mrefu Watanzania hususan wenye simu za mkononi maarufu kama simu za vitochi wamekuwa wakitumia SMS kuwasiliana na wapendwa wao lakini huenda desturi hiyo ikabadilika hivi karibuni.
Idadi ya SMS inayozungumziwa ni zile zilizotumwa ndani na nje ya mtandao kuanzia mwezi Julai hadi Septemba kupitia mitandao ya Artel, TTCL, Tigo, Vodacom na Halotel.
Takwimu za mawasiliano za robo ya mwaka unaoishia Septemba 2024 zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinabainisha kuwa idadi ya ujumbe mfupi wa maneno uliotumwa ndani ya nchi ni bilioni 47.6.
Kati ya hizo SMS zilitumwa ndani ya mtandao ni blioni 20.2 na nje ya mtandao bilioni 27.4.
Katika kipindi cha robo ya mwaka inayoishia Juni, 2024. Jumla ya SMS 50.8 bilioni zilirekodiwa ikijumlisha SMS 25.1 za ndani na 29.3 za nje.
Huenda kupungua kwa matumizi hayo kumechagizwa na kuongezeka kwa matumizi ya mawasiliano kwa njia ya mtandao yanayowezeshwa na matumizi ya intaneti ambayo TCRA imeripoti kuongezeka.
Kwa mujibu wa TCRA Idadi ya laini za Intaneti imeongezeka kwa asilimia 5 kutoka milioni 39.3 kwa robo ya mwaka iliyoishia Juni 2024 hadi milioni 41.4 kwa robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024.
Matumizi hayo ya intaneti hupimwa kwa kuangalia laini ambazo zimetumia huduma ya Intaneti angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, bila kujali teknolojia iliyotumika.