Matumizi ya Bajaji za gesi asilia yazidi kushika kasi Dar 

December 5, 2024 9:18 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Wauzaji wanatarajia mauzo kuongezeka kitaifa vituo vitakapojengwa.
  • Wateja wanapata faida mara mbili ikilinganishwa na modeli za mafuta peke yake.

Dar es Salaam. Huenda umekuwa ukitumia usafiri wa Bajaji (pikipiki ya matairi matatu) na kudhani zizinatumia nishati ya mafuta pekee, fahamu kuwa hali imebadilika! 

Gesi asilia imekuwa nishati muhimu kuendesha vyombo hivyo hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam. 

Kwa nini nishati hiyo inayozalishwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara inachangamkiwa na madereva wa vyombo vya moto? Bei yake iko chini ikilinganishwa na petroli, jambo linalowapunguzia gharama za maisha wamiliki wa Bajaji.

“Zinapendwa zaidi za gesi kwa sababu zina faida kubwa mfano ukijaza ya Sh6,000 unaweza ukapata Sh50,000 na huyo wa mafuta akitumia ya Sh20,000 ndio anaweza kupata hiyo faida lakini inawezekana pia asifikishe hiyo faida,” anasema Alex Shirima, dereva Bajaji eneo la Uwanja wa ndege jijini hapa.

Kuongezeka kwa mahitaji ya Bajaji za gesi asilia kumechangiwa pia na wazalishaji kuzitengeneza kwa wingi ili kuitikia wito wa matumizi ya nishati safi na salama inayosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi duniani. 

Mnamo mwezi Mei kampuni ya Watu Credit inayohusika na mikopo iliweka wazi mpango wa kukopesha pikipiki 1,000 za miguu mitatu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2024.

“Kwa sasa hata kampuni za kukopesha babaji zinakopesha za gesi, ukiniambia nirudi kuendesha bajaji ya mafuta peke yake kuna ugumu kwenye hilo maana napata zaidi kwa sasa,” anasema Nelson Milika, dereva wa Bajaji anayefanyia shughuli zake Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Hali ya uzalishaji wa gesi asilia Tanzania

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji nchini, (Ewura), Tanzania imekuwa ikifanya utafiti wa gesi asilia kwa zaidi ya miaka 50. Ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia nchini ulifanyika mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichopo Mkoa wa Lindi na kufuatiwa na ugunduzi wa pili katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara mwaka 1982. 

Gesi asilia kutoka Songo Songo iliuzwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na ya kutoka Mnazi Bay mwaka 2006. Ugunduzi huo umechochea kufanyika utafiti zaidi wa gesi asilia kwa maeneo ya nchi kavu na majini.

Wapo watoa huduma wanne wanaotekeleza shughuli za gesi asilia  katika mkondo wa kati na wa chini. Watoa huduma hao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Songas Limited, Pan African Energy Tanzania Limited (PAET), na Maurel & Prom (M&P). 

Zipo kampuni zinazoendelea kufanya utafiti baharini na nchi kavu ni Ophir Energy plc, Shell/BG Group plc (BG), Statoil, ExxonMobil, na Ndovu Resources (Aminex).

Hadi kufikia Machi 2016, Wizara ya Nishati ilithibitisha kuwa, hifadhi ya gesi asilia iliyogunduliwa inafikia futi za ujazo trilioni 57.25.

Miezi miwili iliyopita Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert alibainisha kuwa idadi ya magari yanayotumia mfumo wa gesi nchini ni zaidi ya 4,800, wakati vituo 3 vilivyopo vinaweza kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500 kwa siku.

Taarifa ya idadi ya pikipiki za miguu mitatu zinazotumia gesi asilia hazijawekwa wazi, lakini idadi yake inaongezeka kutokana na taarifa za wamiliki na wauzaji. 

Ni fursa kwa vijana na kampuni

Baadhi ya wamiliki wa Bajaji zinazotumia petroli nao wameendelea kubadili mifumo ya vyombo vyao kutumia gesi asilia (CNG kwenye karakana za mafundi wazawa maarufu kama ‘conversion center’.

Saido Masaka, fundi wa kubadili mfumo wa nishati kwenye karakana iliyopo Ubungo, amesema hadi sasa Disemba 3, 2024 wameboresha zaidi ya Bajaji 400 zilizokua zikitumia petroli peke yake na kuziongezea mfumo wa nishati ya gesi.

“Mwaka huu wamiliki wanaboresha wengi zaidi ya mwaka jana, wasio fahamu kuhusu CNG ukiwaelimisha wanakubali kuingia kwenye mfumo wa gesi,” anasema Masaka wakati akifanya mahojiano  na mwandishi wa makala haya. 

Mtendaji wa Mauzo ya Moja kwa Moja ‘Direct sales executive’ wa Bajaj Auto iliyopo chini ya Mohamed Enterprizes Tanzania Limited, Jilala Jitabo, anasema hivi sasa kampuni yao inazalisha pikipiki za miguu mitatu zinazotumia mifumo yote miwili ya nishati za gesi asilia na petroli tofauti na ilivyokua awali.

Jitabo anasema mwitikio ni mkubwa kutokana na unafuu wa gharama, akimaanisha kuwa mwanzo madereva wa Bajaji walikua wanatumia petroli ambayo kwa lita moja ilikua inatembea umbali wa kilomita 25, huku gesi asilia kilo1 ni unatembea kilomita 45.

“Kwa hiyo baada ya mfumo wa gesi kuja, watu wameamua kuupokea vizuri,” anasema Jitabo. “Asilimia 70 ya wanunuaji wote sasa hivi wanatamani gesi, kwa mfano miongoni mwa bajaji 10, wanunuzi nane au saba watahitaji zenye mfumo wa gesi.”

Edmond Coutinho, Meneja Masoko na Mauzo wa kampuni ya Cars& General Trading Ltd, ya Dar es Salaam anabainisha kwamba uuzaji wa pikipiki za miguu mitatu zinazotumia gesi asilia umekua sehemu ya mpango mkakati wao kutokana na faida za kiuchumi wanazopata wateja wao.

“Mpango wa kuwa na kuuza bidhaa zinazotumia CNG ulikuwepo wakati wote kwa sababu ya faida zake, usafirishaji rafiki kiuchumi umekua jambo ambalo tunaliangalia sana ili wateja wapate fursa ya kuboresha maisha,” anasema Coutinho. “Pesa yoyote watakayopata itaongezeka kwa asilimia 20, kitu ambacho tunakipenda sana na kinatufanya tujivunie kuzileta Tanzania kwa mara ya kwanza.” 

Mwonekano wa mtungi wa gesi na “dashboard” ikionesha kiasi cha gesi kilichomo. Picha |Mr Gesi Asili

Upatikanaji rahisi na haraka wa petroli umeendelea kuvutia wamiliki wa vyombo vya moto kutumia nishati ya mafuta, licha ya mwamko chanya wa Bajaji za gesi asilia. 

Kwa mujibu wa Coutinho timu za mauzo za kampuni hiyo zinaripoti modeli zote mbili kuwa na umaarufu sawa, japo anatarajia ongezeko la mauzo ya modeli mpya zilizoboreshwa kutumia gesi siku zijazo ikiwa mikoa mingine pia itafikishiwa nishati ya hiyo.

“Tunaongeza mauzo siku hadi siku, kwa kawaida tunauza mamia kwa mwezi, nadhani itaongezeka kwa elfu kwa mwezi endapo vituo vya kujaza gesi vikiongezeka, tuna mipango mingi inakuja,” anasema Coutinho.

Jitabo anasema uchache wa vituo vya kujazia gesi asilia unakwamisha mauzo zaidi kwa sababu kumekua na mwitikio chanya tangu walipoanza uuzaji wa Bajaji mpya.

“Changamoto kubwa iliyokuwepo ambayo bado inaendelea na itaendelea pasipo kuchukua hatua ni uchache wa vituo vya kujazia gesi…hata hapa Dar es Salaam kuna sehemu tatu tu, gesi ikiisha dereva akienda mfano pale kituo cha TAZARA anaweza kujikuta akisubiri kwa masaa matatu kwenye foleni,” anasema Jitabo.

Hadi sasa kuna jumla ya vituo vitatu pekee vya kujaza gesi asilia vinavyopatikana maeneo ya Tazara, Uwanja wa ndege na Ubungo.

Suluhu hii hapa

Alex Shirima, dereva Bajaji anapendekeza wazalishaji kuongeza ukubwa wa tenki la kuwekea gesi asilia ili waweze kuendesha vyombo hivyo kwa muda mrefu zaidi ya sasa.

“Ningependa kuona maboresho zaidi waongeze mtungi uwe hata kilo 6, nikijaza saa 10 alfajiri nafanya kazi mpaka saa 12 jioni, huu wa kilo 4 nikijaza mpaka kufikia saa 9 mchana inakua imeisha yote,” anasema Shirima. “Serikali ingetuongezea vituo kama cha TAZARA vya kuchukua na kupeleka gesi huku na huku, vikishakua ni vingi hatupati tabu.” 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Balozi Ombeni Sefue  Agosti 21, 2024 mwaka huu alisema ujenzi wa kituo mama cha gesi asilia kilichopo barabara ya Sam Nujoma eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaendelea.

Kituo hicho kitakachotumika kuhudumia vingine chenye gharama ya Sh14.5 bilioni kinataraji kukamilika mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Emmanuel Gilbert, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), alipokuwa akiongea na wanahabari kuhusu changamoto ya foleni kubwa kwenye vituo vya kujaza gesi Oktoba 4, 2024 alibainisha kuwa Serikali imetoa leseni za ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia vinavyotarajiwa kuanza kazi baada ya kukamilika kwa kituo mama.

Huenda kukamilika kwa vituo hivyo kutasaidia kupunguza changamoto iliyopo sasa na kufungua zaidi fursa kwa vijana kujiajiri kwa kazi hiyo.

Enable Notifications OK No thanks