Maswali magumu wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa Tanzania
- Kuolewa zamani ilihitaji mahali, chakula na wawili wanaopendana.
- Kwa sasa gharama zimeongezeka hasa upande wa sherehe na vinginevyo.
- Viongozi wa dini waelezea misingi ya ndoa na ukamilifu wake.
Dar es Salaam. “Siku ya harusi yangu, mambo yalikuwa rahisi sana. Baada ya kufunga ndoa kanisani, tulirudi nyumbani kupumzika kidogo na baadaye kukawa na sherehe iliyofanyika hapo nyumbani,” anasema Esther Lunyalu aliyefunga ndoa mwaka 1959.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 71 anasema baada ya sherehe hiyo iliyohusisha wanakijiji na ndugu wa familia zote mbili ya kwake na mume wake, walianza rasmi maisha ya ndoa katika nyumba ya mume wake.
Esther mwenye watoto tisa na wajukuu 37, anasema licha ya kuwa alitolewa mali ya ng’ombe 10 lakini sherehe ya harusi yake haikuwa na gharama kubwa kwa sababu kilichokuwa kinazingatia ni wanandoa kuishi vizuri na amani.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa wakati huu ambapo sherehe za harusi huambatana na matukio mbalimbali ikiwemo “Engagement”, “kitchen party”, “send-off” na harusi yenyewe.
Matukio yote hayo huihitaji fedha ili kuyatimiza, jambo ambalo limeibua mjadala kwenye jamii kuhusu gharama zinazotumika kufanikisha harusi za kisasa Tanzania.
Siyo ajabu kusikia harusi moja inagharimu Sh50 milioni au hata Sh100 milioni, licha ya kuwa zipo ambazo hutumia kiasi kidogo cha fedha.
Baadhi ya watu wanaamini kuwa suala la gharama siyo hoja bali ni kuhakikisha tukio la harusi ambalo linafanyika mara moja tu linafana huku wengine wakitaka suala la gharama zinazotumika kwenye harusi liangaliwe upya ili kuwapunguzia mzigo waoaji (vijana wa kiume).
Ni muhimu kufahamu kuwa suala la harusi kutumia fedha nyingi au chache hutegemea zaidi na tamaduni, hali ya kipato ya familia na waoaji/waolewaji, hulka ya jamii husika, msimamo na mitazamo tofauti ya watu kuhusu harusi.
Harusi zinazojadiliwa katika makala haya ni zile zinazofungwa kanisani, msikitini na zile za kitamaduni.
Mambo yamebadilika kwa wakati huu ambapo sherehe za harusi huambatana na matukio mbalimbali ikiwemo “kitchen party”, “send-off” na harusi yenyewe. Picha| Believe. Aspire. Experience.
Msingi wa watu ambao wanapenda kuona gharama za harusi zikiwa ndogo ni kuwapunguzia mzigo waoaji ambao kwa tamaduni za Afrika ndiyo hutakiwa kutoa mahari na kugharamia shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika harusi.
Kutokana na changamoto za ajira na kipato, gharama hizo zinazotumika kwenye harusi huwatisha vijana kutimiza ndoto zao za kuingia kwenye ndoa kwa wakati.
“Kuoa siku hizi kumekuwa na mambo mengi, utakuta mwanamke anataka gauni la milioni ambalo anavaa siku moja tu binafsi kama mchumba wangu hatokuwa tayari kuwa na harusi ya kawaida, najiona bachela wa maisha,” anasema Michael Mbelwa (26), mkazi wa Mkoa wa Morogoro.
Baadhi ya vijana wa kiume ambao wameongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanasema gharama za harusi kuwa kubwa ni kutokana na wenza wao wa kike kulazimisha mambo makubwa ambayo wakati mwingine kuyamudu inakuwa ni changamoto.
“Niliwahi kuwa na mpenzi na mara zote alikuwa akinisimulia jinsi angependa harusi yetu ifanyike. Alikuwa anataka gauni kubwa na la bei ya juu, kupambwa saluni, kuwashonea nguo wasindikizaji wake. Hatukudumu,” anasema Mbelwa ambaye anasubiri kumpata mwenza wa maisha atakayekubali kufunga ndoa inayoendana na kipato chake.
Wakati Mbelwa akiwa na hofu hiyo, Paulo Mashauri ambaye amefunga ndoa miaka mitatu iliyopita, pesa haikuwa changamoto kumzuia asifunge ndoa, licha ya harusi yake kutafuna Sh36 milioni.
Mashauri ambaye ana mtoto mmoja anasema harusi yake iligharamiwa na wazazi, marafiki, wafanyabiashara wenzake na ndugu wa karibu huku akibainisha kuwa mafanikio ya harusi hutegemea ni watu gani waliokuzunguka.
Soma zaidi
- Utajiri uliojificha kwenye harusi za kisasa Tanzania
- Unaandaa sherehe ya harusi wakati wa corona? Zingatia haya
- Jinsi wajawazito wanavyoweza kuepuka vitu visivyofaa mwilini
Harusi ni ya mume na mke
Wakati baadhi ya wanaume wakiogopa gharama za harusi, wanawake bado wapo katika kuhitaji ndoa za ndoto zao hata kama uwezo wa kufanya hivyo ni mdogo kifedha.
Mtaalam wa masula ya masoko, Kim Ahmed, yeye anahitaji ndoa ya historia kwa sababu anasema “unaolewa na kufunga ndoa mara moja tu maishani.”
Kim ameiambia Nukta Habari kuwa yeye anatamani harusi ambayo rafiki zake watakuwepo, kupata chakula pamoja na muziki utakaokonga nyoyo ili kumsindikiza katika maisha mapya ya ndoa.
“Hadi sasa, ninafahamu kila kitu kuhusiana na harusi yangu kasoro mume tu. Kwenye harusi yangu nitapenda kuwaona ndugu zangu wa karibu na marafiki zangu wote wa karibu,” anasema Kim anayetarajia harusi yake ihudhuriwe na watu wasiopungua 200.
Hata hivyo, binti huyo anasema anafanya hivyo kwa sababu anaamini kuwa bajeti hiyo itakuwa ndani ya uwezo wake.
“Hakuna haja ya kuanza kukopa, unaweza kufanya sherehe ya kawaida na bado ikawa supa” anasema Kim huku akibainisha kuwa “siwezi kuacha kuweka pesa kwa ajili ya siku yangu maalaumu kwa bajeti yoyote itakayofikiwa, mimi na mume wangu mtarajiwa tutachangia asilimia 35.”
Usikose kufuatilia sehemu ya pili ya ripoti hii ambayo tutaangazia mtazamo wa wazazi na watu mbalimbali kwenye jamii kuhusu gharama za harusi.
Ripoti hii imeandaliwa na Waandishi wa Habari: Rodgers George na Tulinagwe Malopa