Maswali magumu kwa wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa Tanzania-2
- Baadhi ya wazazi wamesema harusi za watoto wao lazima zifane hataka zitakuwa gharama kubwa.
- Viongozi wa dini wasema kuwe na kiasi katika kufanya harusi ili kuepuka mambo yasiyo ya msingi.
Dar es Salaam. Leo tunaendelea na mjadala kuhusu gharama za harusi na jinsi makundi mbalimbali yanavyolitazama suala hilo ambalo ni hatua muhimu ya wanandoa kufunga mbingu za maisha.
Wakati baadhi ya vijana wanaotarajia kuingia kwenye ndoa wakipendekeza harusi zao ziwe za kawaida, baadhi ya wazazi wa watoto wanaoa na kuolewa wana mtazamo tofauti.
Wazazi hao harusi ni tukio muhimu linalofanyika mara moja katika maisha, hivyo linatakiwa lifanyike kwa heshima zote na ili kulifanikisha ni lazima fedha zitumike hata kama wahusika hawana uwezo.
Hali hiyo inatokana na watu kutaka kukidhi matakwa ya jamii na tamaduni zao kufanya sherehe ya harusi yenye viwango vinahitajika na jamii husika.
Mkazi wa kata ya Nzovwe jijini Mbeya, Veronica Mwakaje anasema ni utamaduni wa kawaida kufanya sherehe hata kama muoaji au familia haina pesa.
“Yaani mwanangu anaoa halafu kuwe kimya, haiwekani! Itababidi afanye mipango pesa ipatikane na harusi ifanyike kulingana na bajeti itakayopangwa na ndugu,” anasema Veronica (65) ambaye watoto wake watatu waliooa aliwafanyia sherehe.
Wakati mwingine, watu hulazimisha kufanya harusi zenye gharama kubwa ili kupata michango kutoka kwa marafiki na ndugu ambao wamekuwa wakiachangiana kwenye matukio mbalimbali.
“Nataka harusi ya mwanangu iwe supa! Nimewachangia sana watoto wa marafiki zangu na harusi zao zilikuwa nzuri sana. Rafiki zangu wote wawepo, waumini wa kanisani na wajomba zake na babu zake,” anasema Monica Ludaila ambaye ni mfanyabiashara mkoani Shinyanga na mama wa watoto watatu.
Mtazamo huo wa kuendesha mambo kutokana na mazoea ya jamii, huwaletea changamoto watu wanaoingia kwenye ndoa kufanya sherehe ambazo wanalazimika kutumia gharama kubwa ili kuwapendesha wazazi.
Hali hiyo huchangia kuwatumbukiza wanandoa katika majuto na migogoro kutokana na kukabiliwa na madeni ya fedha walizotumia kufanikisha harusi zao.
Lakini wapo baadhi ya wazazi ambao wanaamini kuwa wanandoa wanapaswa kuisaidiwa gharama zote za harusi na ndugu au familia kwa sababu peke yao hawawezi kuzikamilisha.
“Unaweza kuwaletea matatizo watoto ambao wanaenda kuanza maisha, kama hawana hela ni heri muwachangie au mfanye sherehe ndogo itakayowapa amani,” anasema John Nzenga wa jijini Dar es Salaam.
Wapo baadhi ya wazazi ambao wanaamini kuwa wanandoa wanapaswa kuisaidiwa gharama zote za harusi na ndugu au familia kwa sababu peke yao hawawezi kuzikamilisha. Picha| Daughters of Africa.
Waandaji wa sherehe watakosa kazi?
Ili sherehe ya harusi ifanikiwe inahitaji watu wenye utaalam tofauti ikiwemo upambaji, upishi, upigaji picha, vyombo vya muziki na usanifu wa mavazi. Mambo yote haya huwasaidia watu kuishi mjini kwa kufanya shughuli hizo.
Baadhi ya waandaji wa sherehe wamesema, hata kama sherehe ya harusi itakuwa ya kawaida bado kuna umuhimu wa kuifanya iwe nzuri na waandaaji hawawezi kuepuka gharama.
“Huenda kuna watu hawana uwezo wa kifedha lakini kila kitu kinawezekana hata kwa fedha kidogo. Kikubwa ni kujua unataka nini kwenye sherehe yako, na sisi ni hii ni kazi inayotupatia kipato,” anasema Mariam Herry, mpambaji wa kumbi za sherehe jijini Dar es Salaam.
Anasema harusi ndiyo ajira yake, kwa hivyo kama watu hawatafanya sherehe kwa kuogopa gharama, basi watazuia mnyororo wa thamani wa kupata kipato kwa watu wengi.
Soma zaidi
- Maswali magumu wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa Tanzania
- Unaandaa sherehe ya harusi wakati wa corona? Zingatia haya
- Jinsi wajawazito wanavyoweza kuepuka vitu visivyofaa mwilini
Viongozi wa dini wawatoa hofu vijana
Viongozi wa dini ambao Nukta (www.nukta.co.tz) imefanikiwa kuongea nao wanasema ndoa ni zaidi ya kufunga harusi yenye gharama kubwa na kuwataka vijana kupanua uwezo wa kufikiri kuhusu jambo hilo kwa kutekeleza mambo ya msingi yatakayowapa furaha hata baada ya harusi.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Sheikh Khamis Mataka anasema harusi inakuwa na baraka zote kama imetimiza sheria zinazohitajika kidini.
Kwa imani ya kiislamu, Sheikh Mataka anasema ili harusi ifanyike, kinachohitajika ni mwanaume na mwanamke wanaooana, msimamizi wa harusi hiyo, mahari na tamko la kufungisha ndoa, mengine yote ikiwemo sherehe ni mambo ya ziada.
“Ni vyema kufanya mambo kwa wastani. Dini inahimiza kufanya mambo yote kwa wastani na hakuna sababu ya kujipa gharama zilizo nje ya uwezo wako,” anasema Sheikh Mataka ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Vijana wanaoingia kwenye ndoa wametakiwa kutumia hekima na busara wakati wa kufunga harusi zao na kuepuka mambo ambayo yataharibu mstakabali wa ndoa zao.
Mchungaji wa kanisa la Friends of God Ministry (The promise Mountain) la Nyamagana Mkolani jijini Mwanza, Moses Manguzu amesema harusi za Kikristo zina taratibu zake ambazo zikifuata kikamilifu haziwabebeshi gharama kubwa waoaji.
“Ndoa za sasa hivi zimekuwa na mambo mengi. Mungu aingilie kati. Kwa ambao wanatarajia kuingia kwenye ndoa, ni maombi yangu Mungu awajalie hekima ya kukabiliana na hofu ya maisha,” amesema Mchungaji Manguzu.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ambapo katika sehemu ya tatu tutaangazia kwa undani mitazamo ya watu wa nchi mbalimbali duniani kuhusu dhana ya gharama kwenye harusi.
Ripoti hii imeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Rodgers George na Tulinagwe Malopa.