Maonyesho ya wafanyabiashara kupata msukumo mpya Afrika Mashariki
- Serikali yaagizo kutafutwa eneo jipya la maonyesho mkoani Mwanza.
Mwanza. Serikali Mkoani Mwanza imeiagiza Chemba ya Wafanya Biashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kutafuta eneo maalum kwa ajili ya kufanyia maonyesho ya Afrika Mashariki tofauti na ilivyo sasa ambapo wanafanyia kwenye viwanja vya Nyamagana.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima ametoa maagizo hayo wakati akifungua mafunzo ya 17 ya chemba hiyo yanayofanyika katika viwanja vya mpira vya Nyamagana na kutoa siku 14 kwa wakuu wa wilaya za Nyamagana na Ilemela kukaa chini kuangalia ni eneo lipi sahihi la kudumu litakalofaa kwa maonyesho.
“Tuamue huu ni uwanja wa mpira, kwa heshima ya Mwanza tunatakiwa kuwa na uwanja wa maonyesho, nataka tukubaliane mwakani hatutakuwa hapa tutakuwa na eneo la maonyesho linalokidhi mahitaji, kupita maonyesho haya tulitangaze jiji letu,” amesema Malima.
Maonesho hayo ya 17 yanafanyika jijini Mwanza yakijumuisha mabanda zaidi ya 100 ya wafanyabiashara wa ndani na 55 kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Malima ambaye amesema atakagua mabanda yote Jumatano wiki hii ameahidi pia kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizotajwa na TCCIA ikiwemo ya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kucheleweshwa mipakani wanapokuwa wanavusha bidhaa zao kuja kwenye maonyesho hayo jambo ambalo ameliita ni kuitia doa Tanzania.
“Mwanza inatakiwa tuitangaze kama mji wa biashara na viwanda, wakuu wa wilaya hizi wakae ndani ya wiki mbili waje waniambie eneo gani tulitumie, haya maonyesho yana heshima kubwa yanatakiwa yalete watu lakini katika mazingira haya hatuwezi tunalipua,” amesema Malima.
Makamu wa Rais Chemba ya Biashara upande wa viwanda, Clement Boko amesema wanajitahidi kuleta pamoja makundi ya wafanyabiashara, kilimo, wenye viwanda na ufugaji ili kuonyesha bidhaa zao.
“Tungeomba tuwe na eneo maalum kwa ajili ya maonyesho ambalo tuko tayari kushirikiana na taasisi za Serikali kuweka miundombinu ambayo itaturahisishia kuendesha maonyesho yetu kwa ufanisi,” amesema Boko.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mugimi ametaja changamoto mbalimbali zinazoyakabili maonesho hayo ambazo ni kukosa sera ya kuwafanya wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo kujiunga na chemba, na utitiri wa kodi na ukiritimba wa baadhi ya taasisi za Serikali.
“Tunaiomba Serikali kutengeneza sera ya wafanyabiashara kujiunga na chemba ya wafanyabiashara, ianzishe sera ya sekta binafsi kutatua changamoto zinazoikabili na wafanyabiashara wanaotoka nje wapewe kipaumbele cha clearing kuwahisha bidhaa,” amesema Mugimi.
Latest