Maoni: Hiki ndicho kitakachoua vyombo vya habari Tanzania
- Iwapo mwenendo wa kuporomoka kwa mapato utaendelea, ubora wa habari upo hatarini kuteketea.
- Wananchi wanawajibu wa kuanza kuviunga mkono vyombo angalau kuchangia kununua habari za mtandaoni.
- Kampuni za ndani zinaweza kutenga bajeti zao kiduchu kuunga mkono ukuaji wa vyombo vya habari vya ndani.
Jioni ya Mei 14, 2019 kampuni ya habari ya New Habari Corporation ilitangaza kuwa inataka kufanya “mabadiliko ya muundo wa kiuendeshaji na kiuzalishaji na kubadili mwelekeo wake wa kibiashara kutoka uchapishaji wa magazeti (print) kwenda dijitali.
Kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba, Rai na The African ilieleza kuwa katika zoezi hilo litaenda sambamba na kupunguza idadi ya wafanyakazi.
Hata hivyo, uamuzi mgumu zaidi ambao kampuni hiyo imeuchukua ni kusitisha uchapishaji wa gazeti la Mtanzania kwa mwezi mmoja kuanzia jana Mei 20 na kurejea tena baada ya kipindi hicho.
Tangazo la New Habari linakuja ikiwa ni majuma takriban matatu tu tangu kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kutangaza kwa mara nyingine kuboresha muundo wake na miongoni mwa hatua itakazochukua ni kupunguza wafanyakazi.
MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mtandaoni ya Mwananchi Digital, ni moja ya kampuni kubwa za habari Tanzania ambazo zilikuwa za kwanza kutangaza kubadilisha mwelekeo na kwenda dijitali mwaka 2017.
Hatua hizo zilizotangazwa na kampuni hizi kubwa za habari nchini ni dalili kuwa vyombo vya habari nchini vinakabiliwa na changamoto kubwa ya kimapato katika siku za hivi karibuni hasa baada ya ukuaji wa habari za mtandaoni.
Kwa sasa kiwango cha usomaji wa magazeti kinashuka. Hata kama kampuni za magazeti haziweki takwimu bayana tukafahamu hali ya siku za hivi karibuni, hatua zinazochukuliwa za kubadilisha miundo ya kiuendeshaji zinaonyesha biashara ya uuzaji magazeti haipo sawa.
Unalikumbuka gazeti la Financial Times la IPP Media, lililokuwa na maudhui kedekede yenye ubora kuhusu biashara na uchumi, halipo tena sokoni kwa muda sasa. Gazeti hilo lilitoweka takriban miezi sita tu baada ya kurudishwa tena sokoni.
Teknolojia ya habari mtandaoni siyo tu imevuruga tasnia ya habari nchini bali ulimwenguni kote hadi katika nchi za Magharibi ambako vyombo vya habari vinasifika kwa kuingiza mapato na faida.
Kwa sasa, njia iliyobaki kwa vyombo vingi vya habari nchini ni kwenda dijitali ili kuendana na kasi ya mahitaji ya teknolojia yaliyofanya walaji wa habari kuwa mtandaoni.
Hata hivyo, safari ya kwenda dijitali inakumbana na changamoto lukuki ambazo huenda zikazidi kunyong’onyesha uzalishaji wa habari zenye ubora.
Habari za kwenye tovuti za magazeti hayo au stesheni za televisheni kwa sehemu kubwa zilikuwa ni zile zilizochapishwa ama kutangazwa jana yake. Uchapishaji wa habari mtandaoni haukuwa wa kasi kama sasa. Picha|Mtandao.
Safari ya dijitali bado changamoto
Sehemu kubwa ya vyombo vya habari nchini vinatumia muundo wa biashara wa kiasili unaotegemea matangazo katika kuleta mapato (Traditional advertising model).
Utegemezi huo wa matangazo unatokana na ukweli kuwa Watanzania hatukuzoeshwa tangu awali kuwajibika kulipia habari za mtandaoni kulingana na chimbuko la mfumo huo wa usambazaji habari nchini.
Ikumbukwe kuwa wakati teknolojia ya tovuti inaingia nchini, vyombo vya habari vilikuwa vikichapisha habari mtandaoni kama nyongeza ya habari zilizotokea kwenye magazeti yao. Kuchapisha habari mtandaoni ilikuwa ni kama fasheni siyo chanzo kikuu cha mapato.
Habari za kwenye tovuti za magazeti hayo au stesheni za televisheni kwa sehemu kubwa zilikuwa ni zile zilizochapishwa ama kutangazwa jana yake. Uchapishaji wa habari mtandaoni haukuwa wa kasi kama sasa.
Kwa kuwa habari za mtandaoni zilikuwa kama bakshishi, walaji wa habari hatukulelewa kwenye mazingira ya kugharamia habari hizo kama baadhi ya wenzetu wa magharibi. Nani anunue habari moja ya mtandaoni kwa Sh100? Bado mtihani.
Ujio wa mitandao ya jamii umerahisisha utafutaji, uchakataji na usambazaji wa habari Tanzania lakini umezidi kuongeza maumivu katika upatikanaji wa mapato ya uhakika kuzalisha habari zenye ubora wa hali ya juu. Picha|CFM strategic Communications.
Vyombo vya habari navyo wakati biashara zao zikienda vizuri havikuona kama uzalishaji wa habari hizo ulikuwa ukitafuna vibubu vyao na ungekuwa hatari kwa ukuaji wa biashara zao kutokana na teknolojia kubadili tabia ya ulaji habari.
Kadri teknolojia inavyozidi kuathiri uendeshaji wa vyombo vya habari nchini na kupunguza mapato, wakati gharama za uzalishaji zikipaa, ndivyo ambavyo vigogo wa taasisi hizo wamejikuta wakikuna vichwa kutafuta suluhu.
Hadi sasa hakuna chombo cha habari kinachofahamika nchini ambacho kinatoza fedha wasomaji wa habari zake mtandaoni isipokuwa vile vya kimataifa pekee The New York Times, The Economist au Financial Times.
Kama hakuna kampuni ya habari maarufu inayouza habari zake mtandaoni hapana shaka vyombo vyote vinategemea matangazo kujiendesha.
Ulimwengu wa Google na Facebook
Hata hivyo, kwa sasa utegemezi wa mapato ya matangazo mtandaoni siyo endelevu kutokana na ukweli kuwa kampuni kubwa za teknolojia na habari ulimwenguni za Google na Facebook wanachukua zaidi ya nusu ya matangazo ambayo vyombo vya habari vya ndani vingepata.
Benki, kampuni za simu na nyinginezo ambazo zilikuwa watangazaji wakubwa kwenye blogs and vyombo vyetu vya habari kwa sehemu kubwa zimehamishia matangazo yao Facebook, Google, Instagram na Twitter.
Vyombo vya habari vinapata mapato kiduchu yanayowekwa kwenye tovuti zao au Youtube baada ya kupitia kwa “madalali” hao.
Watangazaji wanaenda katika mitandao hiyo mikubwa duniani kwa kuwa bei ni nafuu na kuna nyanja nyingi za kufuatilia thamani ya fedha za matangazo husika.
Hata Serikali ambayo ndiyo mtangazaji mkubwa nchini kwa sasa amepunguza bajeti ili kubana matumizi.
Changamoto hiyo ya kutokuwepo uhakika wa mapato yatokanayo na matangazo inatishia mustakabali wa vyombo vyetu ambavyo vingi vinaelekea mtandaoni kwa sasa ili kuendana na mabadiliko ya tekonolojia.
Hali hii imeshaanza kutokea katika vyombo vikubwa vya habari mtandaoni hadi huko Marekani.
Zinazohusiana:
- Uganda kuwatoza kodi watumiaji wa mitandao ya kijamii
- Fahamu haya kuhusu matumizi ya intaneti, mitandao ya kijamii duniani
Hata huko ughaibuni mambo hayajakaa sawa
Mapema mwaka huu kampuni ya habari za mtandaoni ya Marekani ya Buzzfeed ilitangaza kupunguza asilimia 15 ya wafanyakazi wengi wakiwa wanahabari ikiwa ni zaidi ya watu 200.
Wakati huo huo, Verizon inayomiliki Yahoo, AOL na The Huffngton Post nayo ilitangaza kupunguza wafanyakazi takriban 800. Ndani ya muda mfupi wafanyakazi zaidi ya 1,000 katika tasnia ya habari kwa vyombo vya Magharibi walipoteza ajira zao.
Iwapo mwenendo huu utaendelea hivi, tutarajie vyombo vingi vya habari kupunguza operesheni zao ikiwemo wafanyakazi katika siku za mbeleni hata baada ya kuingia dijitali.
Kasi ya kupunguza wafanyakazi na kushusha kiwango cha uzalishaji wa maudhui kinazidi kutoa mwanya kwa watu wenye nia ovu kuzalisha habari zisizo na ubora hususan feki (Fake news) ili kuziba kiu ya watumiaji mtandaoni.
Je, vyombo vya habari vinatakiwa vianze kutoza habari mtandaoni kujinasua?
Kwa hali ilivyo sasa jibu ni “Ndiyo”. Hata hivyo, utozaji huo wa habari uendane na ubora wa habari husika.
Habari za mtandaoni zitakazotakiwa zilipiwe lazima ziwe na ubora wa hali juu unaoendana na thamani ya fedha husika. Vichwa vya habari kama vinavyoandikwa Youtube vya marehemu kueleza namna alivyokufa ili kuvutia watazamaji ilihali hakuna maudhui ya msingi vitaua ari ya ununuzi wa habari hizo. The New York Times na baadhi ya vyombo vingine huko Magharibi vimefanikiwa kwa kuongeza ubora wa habari wanazozalisha.
Kuendelea kutoa habari bure katika kipindi ambacho kiwango cha mapato ya matangazo kinashuka kwa kasi ni kuzidi kuhatarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Ili kulinda uhuru huo, hapana budi wananchi wenye uwezo wa kulipia habari wakawajibika kuhakikisha uzalishaji wa habari bora Tanzania ambazo zinaweza kuchagiza maendeleo.
Mbinu nyingine itakayofanya vyombo vya habari kuendelea kutoa huduma ni kuchangamanisha teknolojia na maudhui bora yakiwemo mengine ya nje ya habari za kawaida kwa kutengeneza programu za simu ambazo mtu anaweza kulipia kutazama kama ilivyo kwa Netflix.
Uzalishaji wa makala za uchunguzi za televisheni na nyinginezo mtandaoni za kulipia unaweza kusaidia kuongeza mapato yanayoweza kutumia kugharamia uzalishaji wa habari bora zikiwemo za uchunguzi.
Ni wakati sasa kwa vyombo vya habari kuzalisha habari bora na zenye mashiko zitakazoweza kulipiwa na wasomaji ikiwa ni hatua ya kujipatia mapato. Picha|Mtandao.
Wanahabari bora, timu bora ya teknolojia
Hata hivyo, jambo hili litahitaji vyombo vya habari kuwekeza katika teknolojia na maudhui yenye ubora wa hali ya juu jambo ambalo kwa kampuni nyingi ni changamoto kutokana na uhaba wa mitaji.
Suluhu nyingine ni kwa kampuni nchini hasa benki, kampuni za simu na nyinginezo kujiwekea kiwango fulani cha bajeti zao za matangazo kutangaza na vyombo vya ndani ili kuvifanya viwe endelevu.
Kampuni za simu ni miongoni mwa wanufaikaji kubwa wa vyombo vya habari nchini kwa kuwa wanahabari tunazalisha maudhui yanayoongeza matumizi ya intaneti.
Iwapo vyombo vya habari vitapunguza uzalishaji wa maudhui zikiwemo video na picha hapana shaka mijadala mtandaoni itapungua na kampuni za simu zitaathirika pia. Mpango wa kutangaza na vyombo vya habari vya ndani utafanya biashara zote mbili kuwa endelevu.
Nimalizie tu kueleza kuwa baada ya sheria zisizo rafiki kwa vyombo vya habari, tishio kubwa kwa uhuru wa habari nchini kwa sasa ni kuporomoka kwa mapato katika vyombo vya habari. Hakuna habari za uchunguzi bora bila mapato. Hakuna waandishi bora au habari bora za kina bila mapato.
Mwandishi wa maoni haya ni Mwanahabari mwandamizi wa kampuni ya Nukta Africa aliyejikita katika habari za biashara, teknolojia na takwimu. Mfuate Twitter: @nuzulack.