Mambo ya teknolojia unayotakiwa kuzingatia ukiwa katika safari za kibiashara

June 6, 2019 7:51 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Safari ya kibiashara hutegemea zaidi mipango na maandalizi mazuri.
  • Matumizi ya vifaa vya kidijitali kama kompyuta na upatikanaji wa intaneti navyo ni muhimu. 
  • Kuwa tayari kukabiliana na usiyoyatarajia.
  • Hakikisha unaelewa aina ya soketi za umeme zinazotumika kwenye nchi husika kabla hujaenda ili ujue aina ya multi plug utakayotumia.

Kusafiri ni sehemu muhimu ya biashara ya kisasa. Pamoja na kuwepo kwa mifumo ya masoko ya kidijitali inayokua kwa kasi, watendaji na wamiliki wa biashara wanahitaji kusafiri mara kwa mara kuwafikia wateja wapya, kuwalinda waliopo na kukuza soko.

Safari za kibiashara zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na zamani. Mfanyabiashara anaweza kutumia ndege, treni na hata boti kutoka eneo moja kwenda nyingine bila vikwazo vya miundombinu. 

Lakini safari wakati mwingine huleta uchovu, msongo wa mawazo na kukupotezea kabisa ari ya kufanikisha dili zako za kibiashara. Ukitaka safari yako iwe ya mafanikio zaidi, zingatia dondoo hizi za kiteknolojia zifuatazo ili kujipanga kabla na wakati wa safari:-

Beba vifaa vya kielektroniki

Vifaa hivi vinajumuisha kompyuta mpakato (laptop), chaja ya simu na ikiwezekana hata benki ya kutunzia umeme (power bank) endapo unaenda eneo ambalo halina uhakika wa umeme. 

Kampyuta itakusaidia kufanya shughuli zako ukiwa safarini hata katika vituo vya mapumziko ikiwemo ‘airport’ wakati ukisubiri ndege. Lakini unaweza kuhifadhi nyimbo au filamu (movies) ambazo unaweza kuburudika nazo ukiwa njiani. 

Usisahau kubeba ‘headphone’ ili utakachosikiliza kisiwape tabu watu walio karibu yako. Lakini kumbuka ‘multi plug’ kwa ajili kupata nguvu ya umeme kwenye kompyuta na simu inayoweza kutumika katika nchi mbalimbali ikizingatiwa zinatofautiana. 

Hakikisha unaelewa aina ya soketi za umeme zinazotumika kwenye nchi husika kabla hujaenda ili ujue aina ya multi plug utakayotumia.

Vifaa vya kielektroniki kama kompyuta na simu vitakusaidia kutekeleza majukumu yako ukiwa safarini. Picha|Mtandao.

Hakikisha simu yako ina ‘Apps’ muhimu

Wakati mwingine utahitaji kufahamu mitaa na miji mbalimbali. Programu tumishi ‘Apps’ kwenye simu yako ikiwemo ya ‘Google map’ itakusaidia kuyajua maeneo mengi kwa urahisi.

Beba kadi za benki

Ni vizuri kama utakua na kadi ya kutolea pesa (ATM card) ya benki iliyounganishwa na mifumo ya kifedha ya kimataifa inayokuwezesha kutoa fedha sehemu yoyote duniani kama Visa au Mastercard. 

Safari itakuwa na mafanikio kama umejikikishia usalama wa pesa kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Pia inakurahisishia kulipia huduma au bidhaa kwa njia ya kielektroniki bila kubeba fedha nyingi mfukoni. 

Upatikanaji wa Intaneti ya uhakika

Kama shughuli zako zinahitaji kuunganishwa na mtandao wa intaneti kwenye simu au kompyuta yako, ni vema kabla hujaanza safari kufahamu kama ndege au hoteli utakayofikia inatoa huduma ya intaneti ya uhakika (Wi-fi).

Itakurahisishia mawasiliano ambayo unaweza kufanya kwa njia ya Skype au WhatsApp na utendaji wa shughuli zako za kibiashara. 


Inayohusiana: 


Jiandae kwa yasiyo tarajiwa

Safari yenye mafanikio hutegemea zaidi maandalizi na mipango mizuri. Lakini zipo changamoto zinazoweza kuibuka wakati ukiwa safarini. Unapaswa kujifunza kubadilika na kuendana na mazingira unayokutana nayo kwa wakati husika. 

Mfano, ndege inaweza kuchelewa kuondoka au kuahirisha safari kwa sababu za kiufundi, na wakati huo huo tayari ulipanga miadi na muda wa kuonana na wateja wako. 

Unatakiwa kutulia na kuzikubali changamoto na kisha kutafuta njia ya haraka ya kuzitatua. 

Hata hivyo, teknolojia ni sehemu ndogo ya kufanikisha safari yako. Jipange na zingatia matumizi sahihi ya muda kwa kila hatua ya safari yako ya kibiashara. 

Safari yenye mafanikio hutegemea zaidi maandalizi mazuri. Picha| Mtandao.

Enable Notifications OK No thanks